KIGUGUMIZI cha serikali kuwabana wawekezaji kuanzisha viwanda vya kuchonga na kuongeza thamani ya madini nchini, kinalikosesha taifa mabilioni ya shilingi.
Waziri Mkuu, Edward Lowassa, akizungumza na waandishi wa habari jana katika Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Mwalimu Nyerere muda mfupi baada ya kuwasili nchini akitokea nchini Vietnam, alisema maelfu ya watu Thailand wanakata madini yanayotoka Tanzania.
“Thailand tumeona utaalamu wa kutengeneza vito, wale ni mabingwa wa kutengeneza vito, kuna madini ya tanzanite, yapo yanayopatikana
Tunduru na Songea, yanasafishwa na kuongezewa thamani tayari kwa kuuzwa.
“Ni jambo la kushangaza, wana viwanda vikubwa vya vito ambavyo madini wanayoshughulika nayo yanapatikana hapa nyumbani, kiwanda nilichoona kimeajiri watu 2,000.
“Tumewaomba waje waanzishe viwanda hivyo hapa nyumbani, pia tumewaomba wafundishe watu wetu utaalamu huo na wamekubali kufundisha watu wawili au watatu kwa mwaka.
“Lakini pia tumemuomba Waziri Msabaha abaki kuona kuna nini, vipi madini yetu yako kwa wingi kule na namna tunavyoweza kufaidika na utalaamu wa wenzetu pamoja na kufikia makubaliano mengine ya msingi katika sekta hii,” alisema Lowassa.
Kwa wenye kumbukumbu, hii si mara ya kwanza kwa Dk. Msabaha kubaki eneo hilo kwa lengo la ‘kujifunza’. Ameshajifunza mara nyingi, lakini kinachokwamisha, ni ahadi ambazo hazizai matunda.
Serikali ilishaahidi kuwa ingepiga marufuku usafirishaji wa madini ghafi miaka mitatu iliyopita. Hakuna kilichofanyika hadi sasa.
Akizungumzia mapinduzi ya kilimo yaliyofikiwa na Thailand, alisema nchi hiyo imepiga hatua kubwa kutokana na kutumia kilimo cha kisasa.
Alitoa mfano wa zao la muhogo ambalo pia linalimwa hapa nchini, kwamba Thailand linazalishwa kwa wingi kwa kutumia kilimo cha kisasa na kuuzwa China ambako muhogo unatumika kutengeneza mafuta mbadala.
“Kiteknolojia wenzetu wako juu, tumewaomba wailete teknolojia yao hapa kwetu, wana trekta lenye uwezo wa kupanda mpunga ekari moja kwa saa moja, trekta hili si aghali sana, tunaweza kununua kwa ajili ya wakulima wetu.
“Kwa ujumla wamepiga hatua kubwa ya maendeleo vijijini, wao wameanza zamani kupeleka vijijini dola 7,000, huko wananchi ndio wanaamua wafanye nini na fedha hizo,” alisema Lowassa.
Akizungumzia ziara yake nchini Vietnam, alisema ingawa nchi hiyo imepigana vita miaka 30, imeweza kupiga hatua kubwa kimaendeleo kwa muda mfupi na kufanikiwa kukuza uchumi wake.
Vietnam ni ya pili duniani kwa uzalishaji wa mazao ya mpunga, korosho na kahawa.