JAMII ya wafugaji wa Wilaya ya Meatu, mkoani Shinyanga wamedai kuwa baadhi ya askari huwabambikizia kesi, ili kujipatia rushwa ya mifugo pamoja na fedha.
Wakizungumza na Tanzania Daima kwa nyakati tofauti, mmoja wa wanakijiji hao, Lucas Masanja alisema kuwa mara nyingi askari wa kijijini hapo huwa wanawabambikizia kesi ili kujipatia rushwa ya fedha na mifugo.
Mbunge wa jimbo hilo, Salum Khamis, alithibitisha kuwapo kwa tatizo hilo na kuahidi kulishughulikia kwa kushirikiana na mkuu wa polisi.
Khamis alisema kumekuwapo na malalamiko mengi ya wananchi kubambikiziwa kesi na kuongeza kuwa, lililomsikitisha zaidi ni lile la mzee wa kijijini hapo kubambikiziwa kesi ya mauaji ya binti yake, ambaye alifia hospitalini.
Alisema kuwa mzee huyo alibambikiwa kesi hiyo na Mkuu wa Polisi katika Kituo cha Meatu na kudai kuwa alimuua mtoto wake kwa kumpiga na fimbo.
“Binti wa mzee huyo alikuwa na ujauzito na alikuwa anaugua malaria kwa muda mrefu na baada ya kumpeleka hospitali alifariki dunia. Baba wa binti huyo alienda na kuuchukua mwili wa marehemu na kurudi nao nyumbani kuzika,” alisema mbunge huyo.
Alisema polisi baada ya kujua hilo, walikwenda nyumbani kwa mzee huyo na kumwamuru awapeleke kwenye kaburi ili kufukua na kuona kama marehemu ana majeraha ya fimbo ambayo wanadai kuwa ndiyo yaliyomsababishia kifo hicho.
“Ilipofukiliwa maiti ile, askari wale walisema kuwa ilikuwa na majeraha na ndipo walipomkamata mzee huyo na kumfungulia mashitaka hayo,” alisema.