TIMU kongwe katika Ligi ya Mpira wa Kikapu Mkoa wa Dar es Salaam (Kili RBA), zimeonyesha kutamba katika michezo ya awali ya ligi hiyo iliyozinduliwa rasmi Jumamosi iliyopita kwenye Uwanja wa TCC Chang’ombe jijini Dar es Salaam.
Katika mchezo uliofanyika juzi kwenye uwanja huo, mabingwa watetezi JKT iliwatoa nishai Tanzania Prisons kwa kuwazamisha pointi 83-49 huku wakongwe wengine wa ligi hiyo, Vijana ‘City Bulls’ ikiwatoa nishai Chui kwa ushindi wa pointi 91-47.
Katika michezo mingine, wakongwe waliorejea kwenye ligi hiyo baada ya mwaka jana kushiriki Ligi Daraja la Pili ya Dream Cup, Chang’ombe Boyz, iliibuka na ushindi mbele ya wakali wengine wa ligi hiyo, Savio ‘Watoto wa Baba Paroko’ huku Oilers nayo ikiitoa nishai Jogoo kwa pointi 64-34 huku mkongwe UDSM Outsiders ikitolewa nishai na Chui kwa pointi 43-30.
Wakongwe wengine wa ligi hiyo waliong’aa katika michezo iliyofanyika jana ni Chang’ombe walioipeleka puta Jogoo na kuibuka na ushindi wa pointi 59-27 huku Pazi ikiwabugiza TM Mkwawa pointi 88-48.
Mchezo wa mwisho uliokuwa upigwe kati ya Chang’ombe Boyz na TM Rocket umeahirishwa hadi Jumamosi ijayo