SERIKALI imesema itaufanyia kazi ushauri uliotolewa na Mbunge wa Mtera na Makamu Mwenyekiti mstaafu wa Chama Cha Mapinduzi (CCM), Dk. John Malecela, kuhusu kuwapatia usafiri wa magari maofisa tarafa wote nchini.
Waziri Mkuu, Edward Lowassa, alikubali kupokea ushauri huo na kusema kuwa ni mzuri kwa kuwa katika baadhi ya maeneo ni vigumu kwa ofisa tarafa kuzungukia kwa usafiri wa pikipiki kutokana hali ya kijiografia ya eneo husika kutofikika.
Lowassa alikiri kuwapo kwa ugumu wa kazi kwa maofisa hao hasa wanapotumia usafiri wa pikipiki katika kutekeleza majukumu yao. Alisema ushauri huo wa kuwapatia magari utafanyiwa kazi hasa katika mazingira magumu kiutendaji.
Akiuliza swali la nyongeza bungeni kutokana na swali la msingi lililoulizwa na Mbunge wa Lushoto, Balozi Abdi Mshangama (CCM), Dk. Malecela alisema kazi zinazofanywa na maofisa tarafa ni nyingi na wengine wapo katika maeneo magumu kufikika kwa pikipiki, hivyo ni vema serikali ikawapa magari watendaji hao.
Katika swali la msingi, Balozi Mshangama lilitaka kufahamu sifa za msingi za ajira za maofisa tarafa na hali yao kiutendaji kwa sababu ndiyo waandaaji na wasimamizi wakuu wa miradi ya wananchi katika maeneo yao.
Katika majibu ya swali hilo, Naibu Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (TAMISEMI), Celina Kombani, alisema sifa ya kuajiri maofisa tarafa ni kuwa mhitimu wa Shahada au Stashahada ya Sheria, Menejimenti, Utawala au Sayansi ya Jamii kutoka kwenye vyuo vinavyotambulika na serikali.
Alisema pia wapo wengine ambao hawajafikia kiwango hicho waliopewa cheo cha uofisa tarafa baada ya kupandishwa vyeo kutoka kwenye kazi zao za awali. Kigezo cha uzoefu kazini hutumika kwa kuangalia kigezo cha miaka isiyopungua mitano kazini.
Alisema hivi sasa kazi ya maofisa hao kiutendaji ni nzuri ingawa awali kulikuwa na utata wakati ofisa tarafa alipokuwa akitaka kutekeleza majukumu yake kutokana na maofisa hao kuwa ni wasaidizi wa wakuu wa wilaya na kuwajibika mojamoja katika Serikali Kuu.
Alisema maeneo yaliyotakiwa kusimamiwa na ofisa tarafa ili atekeleze wajibu wake ni maeneo ya vijijini na katika kata ambayo watendaji wake chini ya serikali za mitaa, hali iliyokuwa ikisababisha ugumu katika utendaji kwa maofisa tarafa hao.
Alisema tatizo hilo kwa sasa limepatiwa ufumbuzi, baada ya serikali kuamua kwamba maofisa tarafa waundiwe utaratibu chini ya utumishi wa umma utakaowafanya wawajibike kwa mamlaka ya Serikali Kuu, wilaya na mitaa.
Alibainisha kuwa kwa maofisa tarafa kuwajibika katika serikali kwa upende mmoja, kumechukuliwa kama kuzipunguzia mzigo serikali za mitaa ambako tatizo lililokuwapo ni maofisa tarafa kutumika kama wanasiasa.