LICHA ya kukiri kwa aliyekuwa Makamu Mwenyekiti wa Chama Cha Mapinzudi (CCM), John Malecela, kuwa kuna mpasuko ndani ya chama hicho, ameshindwa kulizungumzia kundi la wanamtandao ambalo lilitumika kumuangusha mapema katika kampeni za kuusaka urais mwaka 2005.
Malecela ambaye jana alifanya mahojiano na waandishi wa habari nyumbani kwake Mvumi Misheni, Dodoma Vijijini baada ya kumalizika kwa sherehe za kumpongeza kwa kustaafu, zilizoandaliwa na wananchi wa Jimbo la Mtera, alisema kuwa ndani ya CCM kuna mpasuko unaotishia uhai wa chama hicho.
Alisema mpasuko huo ni mkubwa katika ngazi za kata na wilaya, na kwamba safu mpya ya uongozi wa kitaifa inapaswa kuelekeza nguvu zake katika kukabiliana na mpasuko huo.
Alisema akiwa kiongozi ndani ya CCM, aligundua kuwepo kwa mpasuko unaoanzia ngazi za kata hadi wilaya, ambao kama hautadhibitiwa sasa, unaweza kusababisha matokeo mabaya kwa chama hicho.
“Mgawanyiko ndani ya CCM unaanzia ngazi za chini, kuna mpasuko katika ngazi za kata na wilaya, viongozi waliopo sasa wajue kuwa kuna haja ya kuweka nguvu huko kudhibiti hali hiyo, vinginevyo kunaweza kuwa na matokeo mabaya,” alisema Malecela.
Akifafanua kauli yake hiyo, alisema kwa kawaida chama hicho kimekuwa na utaratibu wa kufanya mikutano ya ndani ambayo huchangia asilimia 70 ya ushindi katika chaguzi.
Kwamba ili kukabiliana na hali ya sasa katika chama, viongozi waliopo wanapaswa kuzingatia mikutano hiyo ili kuimarisha umoja badala ya mikutano ya hadhara ambayo uzoefu unaonyesha kuwa huchangia kiasi kidogo sana cha ushindi.
Alisisitiza kuwa, pamoja na kustaafu uongozi ndani ya CCM, ataendelea kuwa ‘refa’ na hatasita kukisaidia chama hicho kila kitakapomhitaji na atakapoona inafaa.
“Nasema kwa unyenyekevu kuwa, mimi sina ujasiri, ila niliamua kustaafu mwenyewe, nitakuwa kama refa, nitasaidia kwenye mapungufu, sitakubali kuona CCM inateketea, nguvu zangu sasa nazielekeza kwenye kuimarisha mashina,” alisema.
Akizungumzia sifa anazopewa na baadhi ya watu baada ya kustaafu uongozi, alisema anaamini hastahili sifa hizo kwa sababu anajua upungufu alionao na hata baadhi ya watu wanaujua.
“Siyo yote yanayosemwa juu yangu yananistahili, ninajua nina upungufu wangu na baadhi yenu mnaujua upungufu wangu, hizi sifa ninazopewa sasa hazinistahili, ila ninazichukua kama changamoto za kujirekebisha katika baadhi ya mambo ambayo ninaamini nilikuwa nikikosea,” alisema Malecela.
Huku akionyesha kukerwa na sifa hizo, alisema wanaomsifia sasa walipaswa kumpa sifa hizo akiwa madarakani badala ya kumsuburi hadi alipong’atuka ndipo wakaanza kumsifia.
Aidha, alieleza kuwa sababu nyingine ya kuzikataa sifa anazopewa ni kwa sababu anatambua kuwa yeye si msafi kiasi anachosifiwa na watu.
Kuhusu utaratibu unaotumiwa na chama hicho kupata viongozi wake, alisema mfumo uliopo sasa si mzuri na unapaswa kubadilishwa.
Alisema CCM inahitaji kubadili mfumo wa kupata viongozi badala ya uliopo sasa ambapo baadhi ya wagombea wamekuwa wakitumia kiasi kikubwa cha fedha kupata uongozi.
Alisema CCM inapaswa kuunda tume ya kuchunguza namna bora ya kupata viongozi wake, kwa sababu wagombea wanatofautina uwezo wa fedha na wasiokuwa nazo imekuwa vigumu kupata uongozi.
Wakati akikiri kuwepo kwa mpasuko ndani ya CCM, alikanusha kuwepo kwa kundi la wanamtandao ndani ya chama hicho, ambalo linaaminika kutumika kumuangusha katika harakati zake za kuwania urais mwaka 2005.
Aidha, Malecela alijigamba kwamba hakumbuki kushindwa katika utekelezaji wa mambo yake wakati wote wa uongozi wake.
Kwamba yeye ni mtu asiyependa kufikiri kinyume na kwamba hana tatizo na kustaafu kwake kwa sababu uongozi ndani ya CCM ni sawa na ujenzi wa nyumba.
Kwa kutumia mfano huo, alisema alipoifikisha CCM panatosha, hivyo anawaachia wengine waendelee, kwa sababu anaamini amefanya alichoweza katika kukijenga chama hicho.
Aliongeza kuwa, alikuwa tayari kuua nzi kwa rungu kuliko kukubali wapinzani kushinda katika chaguzi ndogo ambazo alishiriki na kufanikisha ushindi katika chaguzi 26 wakati akiwa Makamu Mwenyekiti wa CCM kwa takribani miaka 15, kabla ya kustaafu wiki iliyopita na nafasi yake kuchukuliwa na Pius Chipanda Msekwa, Spika mstaafu wa Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.