WAKATI serikali ikilalamikia upungufu wa madaktari nchini, baadhi ya wasomi wa mwaka wa kwanza wa Chuo Kikuu cha Kimataifa cha Tiba na Teknolojia (IMTU), wamesimamishwa masomo baada ya Bodi ya Mikopo ya Elimu ya Juu kushindwa kuwakopesha fedha za kulipia ada.
Kusimamishwa masomo kwa wanafunzi hao kuliwalazimu kuandamana hadi Wizara ya Elimu ya Juu, Sayansi na Teknoknlojia ili kujua hatma ya fedha za mikopo walizoahidiwa na serikali.
Jumla ya wanafumzi 137 walifika katika ofisi za wizara hiyo ili kutoa malalamiko yao.
Akizungumza kwa niaba ya wanafunzi wenzake, Biseko Mlebo alisema wameshangazwa na hatua ya Bodi ya Mikopo kuwataarifu kwa barua kwamba watapewa mikopo kwa kiasi kisichozidi sh milioni 2.6 huku kiasi kinachobaki kufika sh milioni sita wakitakiwa kujilipia.
Alisema, suala hilo limewashitua kwa vile walisaini katika bodi hiyo kwa madhumuni ya kupewa mkopo wa sh milioni sita ikiwa ni ada ya masomo kwa mwaka katika chuo hicho.
Mlebo, alisema barua hiyo imezima ndoto za watoto wa maskini wanaohitaji kusoma ili kupunguza matatizo ya afya vijijini.
Alisema, tatizo la upungufu wa madaktari limelalamikiwa na madaktari wenyewe wakati wa mkutano wao wa 41 uliomalizika hivi karibuni uliobainisha kuwa Tanzania ni nchi ya mwisho duniani kwa uhaba wa madaktari.
Pamoja na idadi hiyo ndogo, madaktari wanakimbilia nje ya nchi kutokana na maslahi kidogo ikilinganishwa na nchi nyingine.