logo spc.r_ad0
sp.b_ad0
blu.strip
spc.bt_blu.strip
HABARI MPYA KITAIFA DAR MIKOANI TAHARIRI MAKALA MICHEZO
sp.b_menu
ban
sp.b_ban
jumapili, 16 Desemba 2007
Pekua Tovuti
sp.t_sech.box sp.tafuta_w_tuma sp.t_tuma sp.r_tuma
sp.b_box sp.b_tuma
sp.b_F1
h.sep1
sp.r_men
sp.t
Gazeti la Jana
Matangazo
Bei zetu
Wasiliana nasi
Tuma habari
sp.b_tuma
sp.l_men
h.sep1
sp.l sp.t sp.r
LOGIN
sp.men.l sp.men.t sp.men.r
Username
sp.b_user
sp.t-word
Password
sp.b_word
sp.t_btn
sp.b_btn
sp.b
h.sep1


Elimu yetu ya sasa yawafaa wananchi?
Deus Bugaywa


"HAKUNA mtu anayetaka kuwapenda wengine zaidi ya tunavyojipenda wenyewe, lakini baadhi yetu tuliobahatika kupata elimu nzuri tunawajibika kuboresha ustawi wa jamii tunamoishi, ni sehemu ya kujipenda sisi wenyewe," Julius Nyerere, Machi 5, 1998.

Ni wazi kwamba kila msomi na asiyesoma ambaye ni raia wa taifa hili, ana wajibu wa msingi kabisa kuhakikisha kwamba anatumia akili, nguvu, uwezo na kila kitu chake kuifanya Tanzania kuwa mahali salama pa kuishi kwa kila kiumbe.

Na moja ya hatua za msingi za kulifanya taifa hili kuwa mahali salama na amani kwa watu wake, ni kuwapatia elimu nzuri na ya kutosha watoto wa taifa hili ili baadaye waje kuwa raia wema na wenye kushika majukumu yao kikamilifu.

Ndiyo maana elimu ni ufunguo wa maisha, kwani ukimnyima au ukimpatia elimu duni mtoto wa Tanzania utakuwa umemfungia maisha yake, kwamba kama elimu ni mwanga, basi mtoto aliyepata elimu duni au ambaye hakupata kabisa atakuwa amenyimwa mwanga wa kumulikia njia ya maisha yake.

Kwa maneno mengine utakuwa unamtupa katika shimo la kiza kinene ambalo hatakuwa na namna ya kujitoa, badala yake atakuwa mtumwa na mateka wa giza hilo daima dumu.

Na kwa taifa, kama litakuwa na raia wa sifa hizo, basi ni suala la mjadala kwamba taifa halitakuwa na matumaini ya hali yake ya baadaye.

Nathubutu kusema kwamba katika taifa hilo linaloitwa Tanzanaia kuna watu ambao wamepata elimu nzuri lakini kwa makusudi ama kwa visingizio vingine vyovyote wanavyojua wao wameamua kutotimiza wajibu wao kwa kuboresha ustawi wao, badala yake wanatumia nafsi na usomi wao kuwadunisha wengine.

Mapema wiki hii, nilikuwa safarini nikitokea Dar es Salaam kuelekea Mwanza, katika safari hiyo nilibahatika kukutana na mwalimu aliyekuwa ana safari kama ya kwangu. Mwalimu huyu ni mtu mzima ambaye atakuwa anastaafu katika kipindi cha miaka mitatu au minne ijayo, shule anayofundisha iko katika moja ya wilaya za Mkoa wa Morogoro.

Katika mazungumzo yetu kuhusu mustakabali wa nchi hii, ambao ulianzishwa na kipande cha barabara cha njia ya kati ambacho hakijakamilika, tulijikuta mjadala unakuwa mpana na kugusa nyaja zingine za maisha ya taifa hili.

Moja ya mambo yaliyotuchukulia muda wetu ni masuala yanayohusu taaluma yake ambayo amekuwa akiitumikia kwa karibu miaka thelathini sasa. Katika mjadala huu niliogopeshwa na ukweli ambao hata hivyo naamini msomaji unaujua, lakini kwamgu nilikuwa sijawahi kuusikia toka kwa mhusika moja kwa moja.

Ninaomba nimnukuu alipokuwa akizingumzia suala la elimu ya msingi.

"Ninakwambia kijana kama una watoto au utakapowapata mimi ni mwalimu nimefundisha mikoa ya Tabora, Mwanza na sasa Morogoro nilikokuja kustaafia, usimpeleke mtoto wako katika shule zenu hizi za serikali, zimepoteza sifa ya kuitwa shule siku nyingi.

"Mimi watoto wangu pamoja na dhiki zangu za kiualimu, hawasomi shule hizo na hata hizo za kata zinazoanzishwa asikudanganye mtu, hizo si shule ni viwanja tu vyenye majengo yanayoitwa shule, lakini shule kwa maana ya elimu naweza kukuapia haipo hata moja ya kata inayotoa elimu ya sekondari."

Maneno ya mwalimu huyu yaliniogopesha, niliogopa kumsikia mwalimu tena mwenye mzoefu akiapa kwa nguvu zote kwamba watoto wake hawawezi kusoma katika shule za serikali.

Aliendelea kunieleza kuwa jinsi wanafunzi wanavyojaa madarasani na jinsi isivyokuwa rahisi kumudu kuwafundisha.

Kwamba kinachofanyika mashuleni siku hizi ni mwalimu kuchagua watoto wachache wenye uwezo kidogo darasani, wanakaa mbele ya darasa, hao ndio anaohangaika nao walau kidogo, wengine anasema nikitumia maneno yake 'Mungu atawasaidia'.

Anaendelea kueleza kuwa, 'hata waratibu na wakaguzi wakija, hawawezi kufanya kitu, zaidi wanasema jamani fanyeni linalowezekana, watakaoelewa ndio hao na wasioelewa ndiyo hivyo, nchi ndiyo ishakuwa ya hivyo'.

Ananisimulia jinsi vijana wanaofaulu na kujiunga shule za kata wasivyotendewa haki kwa kukosa elimu ya sekondari inayostahili.

Ananipa mfano wanafunzi wa sekondari ya kata fulani wanaomaliza kidato cha pili wakiwa hawajasoma masomo ya Baiolojia, Kemia, Fizikia na Hesabu.

Anashangaa unafiki wa wanasiasa wakiwa majukwaani wavyosisitiza vijana wasome masomo ya sayansi ili kulisaidia taifa wakati uzoefu unaonyesha shule nyingi za kata hazina walimu wa kutosha na wanafunzi wanaburuzwa tu kumaliza mihula lakini hakuna wanachokipata katika mihula hiyo kwa maana ya elimu.

Tuliyozungumza ni mengi na yanaweza kujaza safu hii, lakini kinachoifikirisha akili yangu zaidi ya mara mbili ya kawaida ni kitendo cha mwalimu kuapa kwamba hata kwa ncha ya upanga hawezi kumpeleka mwawe kusoma katika shule anayofundisha au tuseme za serikali.

Kwa sababu zozote zile hapa kuna jambo la kulitazama kwa ujumla wetu kama taifa.

Nchi yetu suala la elimu, kuanzia ya msingi mpaka ya chuo kikuu limefanywa kuwa la kisiasa, kila uamuzi unaotolewa hauzingatii misingi na mahitaji ya kitaaluma ya kufikia uamuzi huo.

Mfano mzuri ni ufunguzi wa shule za kata, eti kwavile tu mbunge au waziri alipita akaahidi msaada fulani, basi ili kulinda heshima yake na asipoteza hadhi yake kisiasa.

Mimi sijui tumedhamiria nini hasa katika maamuzi haya tunayoyafanya kuhusu elimu, kwamba tunatengeneza walimu wa haraka haraka. Nimetembelea shule moja wanafunzi wanawaita wa 'vodafasta', wa mwaka mmoja au mwezi mmoja waende wakafundishe katika mazingira ambayo hata mwalimu aliyefuzu kikamilifu na mzoefu yanampa tabu kuyamudu.

Tunaelekea kulizika taifa letu, miaka 46 ya uhuru bado tunajenga shule na kutengeneza walimu wa kubahatisha, sijui tunamdanganya nani, kwa sababu hili ni taifa letu wenyewe.

Haijalishi sana kama sisi watoto wetu wanasoma St. nini sijui lakini maadam nao ni watoto wa taifa hili hawatakuwa na ujanja wala hawawezi kuukwepa mzingo wa ndugu zao waliopata bora elimu muda utakapofika wa kupembua mbivu na mbichi.

Ingawa watawala wanatueleza kuwa huu ni mwanzo tu baada ya muda shule za kata zitakuwa na sifa zinazostahili, lakini historia na uzoefu ni walimu wetu wazuri, tuna sababu ya kuwa na shaka.

Ninazifahamu shule ambazo zimejengwa miaka ya 60 lakini toka miundombinu yake ilivyochoka ni kwa uchache sana zimeweza kurejeshwa katika hali yake.

Lakini pia ni suala la kuikubali hali halisi kwamba, hakuna namna kwa bajeti ya nchi hii yenye kutegemea asilimia 40 toka nje, kumudu kuhudumia shule zote za kata kwa ukamilifu hata katika kipindi cha miaka 20 ijayo.

Mwisho wa siku tukubali kwamba tumejuana, nani akisema nini tunajua tu ni kwa sababu gani amesema hivyo ndiyo maana hata hizi ahadi kwamba shule za kata zitakuwa na sifa zinazostahili, zitakuwa na maabara za kisasa, maktaba, walimu wa kutosha na mahitaji mengine muhimu ya shule ni sanaa tu.

Kama tulishindwa kusoma alama za nyakati tangu mwanzo tukaanza kujipanga kwa ajili ya maandalizi ya walimu, nyumba za walimu na vyumba vya madarasa ili kuepuka kazi ya zimamoto tunayoifanya sasa, tumetoa wapi hiyo akili ya kujipanga kufanya shule hizi zikamilike?

Dalili ya mvua ni mawingu, kila dalili leo inaonyesha kwamba kila shule ikishafunguliwa na wanafunzi kuanza kusoma inakuwa imesahaulika hata kama ina walimu watatu.

Na kama dalili ya kuonyesha kwamba zoezi la kujenga shule za sekondari limekalika kwa mafanikio, sasa tunaota ndoto za kujenga zahanati na vituo vya afya kila kata.

Kwa hili sina hakika wauguzi na madaktari watakaohudumia zahanati hizi watakuwa wanasoma masomo chapuchapu kwa wiki ngapi, maana kama naamini yatakayotokea kwa wagonjwa watakaotibiwa na madaktari hawa ni Mungu na malaika zake ndio wanaojua.

Ninavyolitazama suala hili, ni kama tumeamua kujenga matabaka ya kielimu rasmi, kwamba wawepo watoto wa wateule wachache ambao ndio wenye elimu bora, watakaokuwa na jukumu la kushika hatamu za taifa hili (tayari dalili za hilo ziko wazi), na wa walalahoi ambao kazi yao itakuwa upagazi tu kwa kuwa kiwango na ubora wa elimu yao hakitaweza kushindana na cha wateule wachache.

Na kwa vile hatuna mahali pa kukimbilia kuepuka laana hii ni vema kila mwenye nia njema akatumia nafasi yake katika kijiji, kata, wilaya na popote alipo kudai maelezo ya kutosha na yenye mantiki ya mazoezi haya na nini hasa maana yake kwa jamii ya Watanznaia walio wengi.

Hawa ni watoto wetu, tuanze na wabunge wetu, watupe sababu za kutosha na mantiki ya uamuzi wa kuwa na shule kila kata kama uliamuliwa kitaalamu kiasi gani?

Na kama nia ya dhati ni elimu, kwa nini si kila tarafa shule moja au mbili ambazo kila kata itaelekeza nguvu zake huku ili kujenga shule halisi kwa maana halisi ya neno shule na kwa mujibu wa waasisi wake badala ya sasa kuweka kuta nne zilizoezekwa na kuziita shule?

Ukiona mwalimu wa shule hataki aslani kumpeleka mwanawe katika shule anayofundisha na badala yake anawapelekea wengine wamfundishe, si bure.

Sidhani kama yuko mzazi aliye tayari kumpa mwanawe nge akiomba yai, kama ambavyo hatuwezi kuwapa wanetu nge wanapoomba mayai. Wale wote wenye dhamana juu ya ustawi wa watu wa taifa hili watimize wajibu wao.

Na tujiulize, tuliikataa elimu ya kizamani, tukiiita elimu ile haramu, maana ya kikoloni, ilituishia hamu kuiga ya ugenini, Je, elimu yetu ya sasa yawafaa wananchi?

Mungu ibariki Tanzania.

Simu:0732 449 421. drbugaywa@yahoo.com


h.sep
juu sp.b
Habari Mpya  |  Kitaifa  |  Dar  |  Mikoani  |  Tahariri  |  Makala  |  Michezo  |  Matangazo  |  Webmaster
Copyright 2007 © FreeMedia Ltd.
Free media limited
mtaa wa Mkwepu na Makunganya, jengo la Bilicanas, gorofa ya kwanza, SLP 15261, Dar es salaam, Tanzania
simu +255-22-2126233  •  faksi +255-22-2126234  •  Selula  0713 296570