logo spc.r_ad0
sp.b_ad0
blu.strip
spc.bt_blu.strip
HABARI MPYA KITAIFA DAR MIKOANI TAHARIRI MAKALA MICHEZO
sp.b_menu
ban
sp.b_ban
jumapili, 16 Desemba 2007
Pekua Tovuti
sp.t_sech.box sp.tafuta_w_tuma sp.t_tuma sp.r_tuma
sp.b_box sp.b_tuma
sp.b_F1
h.sep1
sp.r_men
sp.t
Gazeti la Jana
Matangazo
Bei zetu
Wasiliana nasi
Tuma habari
sp.b_tuma
sp.l_men
h.sep1
sp.l sp.t sp.r
LOGIN
sp.men.l sp.men.t sp.men.r
Username
sp.b_user
sp.t-word
Password
sp.b_word
sp.t_btn
sp.b_btn
sp.b
h.sep1


Mlaji wa mwisho ndiye anayeumia
Privatus Karugendo


HADI sasa hakuna chombo cha kudhibiti bei ya bidhaa zinapomfikia mlaji wa mwisho.

Kama chombo hiki kipo, basi ninaamini hakifanyi kazi yake!

Serikali inatangaza bei ya bidhaa kwenye bajeti ya kila mwaka.

Bei hizi zinatangazwa kwenye vyombo vya habari, wananchi wanasikika kwamba sukari ni bei fulani, mafuta ya taa ni bei fulani, soda ni bei fulani, lakini bei hizo zinabaki kwenye maandishi tu!

Kawaida mlaji wa mwisho anawekwa kitanzini na bei tofauti na ile iliyotangazwa na serikali. Ni wazi kuna gharama za usafirishaji. Bei ya mafuta ya taa ya Dar es Salaam, haiwezi kulingana na ile ya Karagwe. Lakini kwa serikali inayojali, bei hizi haziwezi kutofautiana sana. Mafuta ya taa ni muhimu Karagwe vijijini ambako hakuna umeme.

TRA inawabana wafanyabiashara kuhakikisha wanalipa ushuru, serikali inayojali ni lazima itoze ushuru.

Wakorofi wanaokataa kulipa ushuru wanatozwa faini, na kuna wengine wanaokubaliana na TRA kwa kulipa kitu kidogo na hatimaye anayeumia kwenye mzunguko huu wa biashara ni mlaji wa mwisho.

Katika makala hii, ningependa kumjadili mlaji wa mwisho wa kijijini. Huyu ndiye anayeumia zaidi, na Watanzania wengi wanaishi vijijini.

Tunaposema kwamba Watanzania bado ni masikini, mara nyingi tunawalenga hawa wa vijijini, Lakini jambo la kushangaza ni kwamba, hawa tunaowaita maskini ndio wanaokamuliwa zaidi bila huruma. Hawa ndio hawana mifumo ya kulinda ustawi wao.

Nitoe mfano wa Kata ya Kamuli, Tarafa ya Kituntu-Mabira, Wilaya ya Karagwe. Katika tarafa hii sukari kilo moja inauzwa shilingi 1,500 na inapanda kijiji hadi kingine. Maana yake ni kwamba unaweza kukuta kijiji kingine wanauza sh 1,800!

Wafanyabiashara wanaongeza bei kufidia ushuru na kila hasara inayojitokeza katika biashara yao, soda inauzwa kati ya sh 500 na sh 700, mfuko wa saruji ni sh 23,000 na kuendelea, inategemea saruji imetoka Uganda au hapa hapa nchini.

Chumvi kilo moja ni sh 1,200, sabuni mche ni sh 1,000, mafuta ya taa lita moja ni sh 1,500 hadi sh 1,700, petroli ni sh 2,000, mabati ni sh 12,500 kwa bati moja.

Nimetoa mfano wa Kata ya Kamuli, lakini ukizunguka Wilaya ya Karagwe, utashangaa jinsi bei hizi zinavyobadilika, kijiji hadi kijiji, kata hadi kata na tarafa hadi tarafa.

Wilaya hiyo hiyo, bei ya mafuta ya taa ni tofauti, bei ya chumvi ni tofauti, bei ya sukari ni tofauti nk. Kama tofauti ni senti au shilingi, ni jambo la kawaida, lakini tofauti inapozidi elfu moja, inakuwa hatari.

Inaonyesha jinsi wafanyabiashara wanavyoachiwa uhuru wa kufanya wanavyotaka wakati mlaji wa mwisho anaendelea kuumia na kudidimia!

Pia inaonyesha jinsi viongozi wa serikali kama mkuu wa wilaya, wasivyokuwa na muda wa kuzunguka kukagua maendeleo ya wananchi.

Wanapitapita kuhimiza michango ya kujenga sekondari za kata na zahanati huku wakifumba macho kwa mambo mengine kama hili la bei za bidhaa kupanda ovyo bila mpangilio.

Hata kama hakuna chombo kinachoeleweka cha kudhibiti bei, kiongozi anayejali, hawezi kuona bei za bidhaa zinawaumiza wananchi wake akakaa kimya! Vinginevyo kiongozi huyo hafai!

Kipato cha wananchi wa Kata ya Kamuli, kinategemea mazao: kahawa, maharage, mahindi nk. Kilo moja ya kahawa inauzwa kwa shilingi 700, maharagwe shilingi 700. Mkulima wa kawaida anaweza kupata kati ya kilo 200 hadi 300 za maharage na kahawa kwa mwaka.

Ukiangalia bei ya bidhaa nilizozitaja hapo juu, mkulima huyu anahitaji kilo ngapi za kahawa na maharage ili aweze kuishi maisha bora?

Hadi sasa serikali haijaonyesha nia ya kumsaidia mkulima kuboresha kilimo chake, wakulima wengi bado wanatumia jembe la mkono, wanalima mashamba madogo ambayo hayawezi kuleta mabadiliko ya haraka, na mipango ya kutoa mikopo kwa wakulima, kama ipo, basi haiko wazi.

Bei ya kahawa imepanda karibuni baada ya shinikizo la wanunuzi binafsi. Mbunge wa Kyerwa, amefanya jitihada za kuhakikisha bei ya kahawa inakuwa nzuri, ameonyesha nia njema ya kuwajali wakulima na wapiga kura wake katika Jimbo la Kyerwa.

Pamoja na jitihada hizo, bado kuna haja ya serikali kuingilia kati kuboresha kilimo cha kahawa na kuunda chombo cha kudhibiti bei ya bidhaa zinapomfikia mlaji wa mwisho.

Vinginevyo itakuwa vigumu wakulima wa vijijini kupata maisha bora. Watauza kahawa na kupata pesa nzuri, lakini pesa hizo zitaishia kwenye kununua bidhaa muhimu ambazo bei yake inapanda kufuatana na matakwa ya wafanyabiashara.

Huyu mkulima wa Kamuli, anayekabwa koo na wafanyabiashara, bado anawekwa kitanzini na michango ya serikali, kama vile michango ya sekondari za kata, zahanati, karo, matibabu, nk.

Huyu hana maji safi, barabara mbovu, hana umeme na wakati mwingine yuko mbali na hospitali. Kwa maneno mengine, huyu anahitaji mfumo wa kumsaidia kutunza kila senti, maana kila senti inayopotea kwake ni muhimu sana.

Hali hii inanisukuma kuishauri serikali kufikiria kuunda chombo cha kudhibti bei ya bidhaa zinapomfikia mlaji wa mwisho, kwa mfano bidhaa ambazo ni za lazima kwa maisha ya kila siku na zile zinazoboresha maisha ya mwananchi.

Mafuta ya taa, chumvi, sukari, sabuni nk. ni vitu muhimu sana kwa maisha ya kila siku hivyo bei yake isipodhibitiwa, wananchi wataendelea kuishi maisha magumu.

Saruji na mabati ni muhimu sana kwa kujenga nyumba bora na za kisasa. Je, kama bei ya mfuko wa saruji ni shilingi 23,000 watu watamudu kujenga? Na je, kama mabati ni shilingi 12,500 ni wangapi wataweza kujenga nyumba za bati?

Wafanyabiashara wasiachiwe huru kupandisha bei za bidhaa jinsi wanavyotaka. Ni lazima kuwabana! kuwepo na chombo cha kudhibiti bei kwa lengo la kumlinda mlaji wa mwisho.

Serikali ya Awamu ya Nne, imekuwa ikijielekeza katika kuleta maisha bora kwa kila Mtanzania, hili ni jambo zuri na kila mtu anatamani hivyo, lakini ni ndoto kufikiria kuleta maisha bora kwa kila Mtanzania bila mifumo mizuri kama vile kudhibiti bei ya bidhaa zinapomfikia mlaji wa mwisho.

Nimetoa mfano wa Kata ya Kamuli, lakini imani yangu ni kwamba maisha ya vijiji vyetu hapa Tanzania yanafananafanana. Nafikiri kilio hiki ni kilio cha vijiji vyote!


h.sep
juu sp.b
Habari Mpya  |  Kitaifa  |  Dar  |  Mikoani  |  Tahariri  |  Makala  |  Michezo  |  Matangazo  |  Webmaster
Copyright 2007 © FreeMedia Ltd.
Free media limited
mtaa wa Mkwepu na Makunganya, jengo la Bilicanas, gorofa ya kwanza, SLP 15261, Dar es salaam, Tanzania
simu +255-22-2126233  •  faksi +255-22-2126234  •  Selula  0713 296570