JUNI 3 hadi 12, mwaka huu, Tanzania ilipata ugeni wa timu za mpira wa kikapu za Young Life zinazojumuisha wachezaji wanaosoma vyuo vikuu mbalimbali nchini Marekani.
Young Life ni taasisi isiyo ya kiserikali, inayojishughulisha na kuwalinda na kuwapa matumaini kimaisha vijana, ambayo ina mtandao katika nchi zaidi ya 50, Tanzania ikiwa mojawapo.
Kwa ushirikiano wa Young Life Tanzania na Young Life Marekani, zilifanikisha ziara ya timu hizo, ambayo hakika imetoa changamoto kubwa katika mpira wa kikapu hapa nchini.
Mbali ya kucheza mechi kadhaa na timu za hapa nchini, wachezaji wa timu hizo pia walipata fursa ya kutoa ufundi na mbinu za mchezo huo kwa wachezaji hapa nchini, kupitia kliniki mbalimbali zilizokuwa zikifanyika mara na baada ya mechi hizo.
Kwa wadau wa michezo, hususan mpira wa kikapu, waliopata fursa kuwa pamoja na timu hizo wakati wa ziara yao hapa nchini, watakubali kuwa, ziara hiyo ilikuwa ya mafanikio na imeacha changamoto kubwa, na endapo ikifanyiwa kazi, mabadiliko makubwa ya kimaendeleo katika mpira wa kikapu Tanzania, yataanza kutokea.
Namshukuru Mungu, nilikuwa mmoja wa watu waliohudhuria programu mbalimbali, ikiwamo mafunzo na mechi kwa karibu kipindi chote wageni hao walipokuwa hapa nchini.
Mambo yaliyokuwa yakifanywa na wageni hao si kwamba yalikuwa mazuri tu, bali yalimvutia kila aliyebahatika kushiriki ama kutizama jinsi walivyokuwa wakiendesha shughuli zao kwa kujiamini na uangalifu mkubwa.
Jambo muhimu lililowaleta hapa nchini ni kufahamiana na wenzao, yaani Young Life Tanzania ili kubadilishana mambo mbalimbali kuhusu mpira wa kikapu na ya kijamii kwa ujumla.
Kutokana na mafunzo mbalimbali kuhusu mpira wa kikapu, yalisaidia kugawana uzoefu sambamba na kujenga urafiki.
Katika mechi zote walizocheza, timu za Tanzania zilikuwa zikitolewa nishai na wageni hao jambo lililonifanya nitafute nini tatizo, au upungufu na tofauti baina yao ni nini.
Katika mahojiano na kocha mkuu wa Young Life Marekani Wanaume, Chaz Fritz, alisema kuwa Tanzania kuna vipaji na wanaweza kufanya vema.
Kadiri siku zilivyokuwa zinakwenda matokeo yalionyesha Tanzania ‘Negative’, Marekani ‘Positive’, ilibidi nigune na kumuuliza tena mchezaji mrefu ambaye alikuwa aking’ara na Wamarekani, Kelvin Cantinol, kulikoni mbona tunashindwa kuwamudu.
Mchezaji huyo alijibu kuwa, Tanzania kuna wachezaji lukuki wenye vipaji, lakini haelewi tatizo lao linatokana na nini hasa, maana uwezo wanaoonyesha kimsingi ndio kama wanaouonyesha wao.
Nilikubaliana kwa namna moja ama nyingine na majibu hayo, kwani nilipokuwa nikitizama mechi za wasichana na hata wavulana, sikuiona tofauti kubwa kati ya nyota mwingine wa Wamarekani hao, Tyler Fritz (mtoto wa kocha timu ya wanaume-USA) na Emmanuel ambaye ni nyota wa Young Life Tanzania.
Jambo hilo lilinifanya nimtafute Emmanuel, ambaye alikuwa akifananishwa na Tyler. Nilipomuuliza tofauti ya yeye na Tyler alijibu kuwa:
“Huyu ni mtoto wa kocha na isitoshe huu mchezo asili yake umeanzia huko huko kwao.”
Kwa majibu hayo, niliona sababu hiyo hainiridhishi sana, ikizingatiwa hata Fritz mwenyewe anakiri uwepo wa utitiri wa vipaji hapa nchini aliouona kwa kipindi hicho kifupi alichokaa hapa.
Kwa ufupi ni kwamba, niligundua tatizo walilokuwa nalo wachezaji wa Tanzania ni kutokujiamini tu basi! Si kocha mbaya wala muda mfupi wa mazoezi.
Nasema hivyo kwa sababu hata kocha wa timu ya Young Life Wanaume ya Marekani, Chas Fritz alikuwa akilisema hilo mara kwa mara pindi mechi zinapomalizika.
Nilijaribu tena kumdadisi tena kocha huyu, pale niliposhuhudia kombaini ya Mkoa wa Dar es Salaam ‘The Dream Team’ ilipofungwa na Young Life Marakekani, kwenye Uwanja wa Ndani wa Taifa, jijini Dar es Salaam katika mechi ya mwisho ya Wamarekani hao kwa Tanzania Bara kabla hawajaelekea Zanzibar.
Fritz alijibu kuwa: “Ninyi hamna tatizo, zaidi ya kutokujiamini. Mpira unapokuwa eneo la hatari, wachezaji wanatakiwa kuwa makini na kujiamini, maana hapo ndipo panapotupa sisi faulo ambazo zinatusaidia sana na ndiyo maana tunaondoka na ushindi katika mechi zote.”
Kauli hiyo ya Fritz niliiridhia kutokana na ukweli kuwa, ndiyo hali halisi iliyokuwa ikijitokeza kiufundi kwani timu zetu zilikuwa zikifanya faulo mara kwa mara katika eneo la hatari, jambo ambalo wenzetu walikuwa makini kuliepuka kwa kila hali japokuwa kwa mara chache walikuwa wakifanya faulo katika eneo lao la hatari.
Kutokana na makosa hayo ya kiufundi na kutojiamini kwa Watanzania, kuliwagharimu na kupoteza mechi zote na kuifanya timu hiyo kuondoka na rekodi ya aina yake.
Tukianza na mechi ya kwanza iliyokuwa kati ya Young Life Marekani na wenyeji wao Young Life Tanzania, katika Uwanja wa Ubungo Flats, kwa upande wa wanaume Tanzania ililala kwa pointi 49-61 wakati wanawake walichapwa kwa pointi 22-11.
Mechi ya pili iliwakutanisha, Wamarekani hao na Shule ya Sekondari Filbert Bayi, Kibaha kwa upande wa wanawake huku kwa wanaume wakikipiga na Oilers ya Tanzania.
Katika siku hiyo, kama ilivyokuwa ada, mafunzo yalitolewa na wageni hao ili kujenga ukaribu kabla ya mechi jambo ambalo lilisaidia kufahamiana miongoni mwa wachezaji na kusaidia kuondoa woga kabla ya mchezo.
Katika mechi hizo, jambo la kushangaza ni kwamba, vijana wa Filbert Bayi walicheza kwa kujiamini, hasa walipokuwa wakishambulia, lakini mara mpira unaporudi golini kwao, walikuwa wakipaniki kufanya faulo, zilizochangia kushindwa.
Hali hiyo pia ilijitokeza kwa Oilers, ambao licha ya kuongoza kwa muda mrefu katika mechi yao, lakini kutokana na makosa kama hayo, walijikuta wakilala kwa pointi 56-41.
Na kikubwa klilichojitokeza katika mechi hizo licha ya kucheza kwa kujituma, lakini ukweli uliojibainisha ni kutokujiamini na si jambo lingine.
Jambo hilo pia liliridhiwa na kocha msaidizi wa Young Life Tanzania, Charles Mosoji.
“Nimegundua tatizo tulilokuwa nalo sisi wakati wa mechi yetu pale Ubungo, ndilo ninaloliona hapa uwanjani hii leo na hili suala hawa wageni wamekuwa wakituasa sana, tangu walipowasili nacho ni kujiamini na umakini,” alisema.
Kutokana na kuwa, makosa hayo ya kiufundi ndiyo yaliyochangia kupata matokeo mabaya kwa timu zetu, hii iwe changamoto ambayo makocha wa Tanzania wanapaswa kuifanyia marekebisho na kuwajenga wachezaji wao katika kuyaepuka.
Baadhi ya matokeo ya mechi nyingine zilizochezwa na Young Life Marekani hapa nchini ni kati ya kombaini ya Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM) na wageni hao ambako walishinda 77-41 huku Prisons wanawake wakichapwa 66-51.
The Dream Team wanaume nayo ilitia aibu baada ya kupata kipigo cha pointi 73-53 huku wanawake wakifungwa kwa taabu 41-40, wakati huko Zanzibar, kombaini ya wanawake Pemba ilichapwa pointi 64-42 wakati wanaume nao wakiangukia pua kwa kulala 76-57.
Kwa baadhi ya matokeo ya mechi hizo na kama ulipata nafasi ya kuhudhuria mechi hizo, kimsingi utakubaliana na makocha hao kuwa, wachezaji wetu wanaponzwa na kutokuwa na umakini na kujiamini, mambo yanayowasababisha kufanya faulo katika maeneo ya hatari.
Basi makocha mbalimbali nchini, hii ni changamoto, iliyoachwa na nyota hao kutoka Marekani, ambayo inatakiwa kufanyiwa kazi ili kuleta mabadiliko ya kimaendeleo katika mpira wa kikapu hapa kwetu.