jumatano, 20 Juni 2007

Ahoji ‘mabilioni ya JK’ kwa Z’bar
MBUNGE JIMBO LA GANDO

na Kulwa Karedia na Rachel Chizoza, Dodoma


MBUNGE wa Gando, Khalifa Suleiman Khalifa (CUF), jana aliiohoji serikali na kutaka kupata maelezo kuhusu mpango wa kuigawia Zanzibar, fedha za kuwawezesha wajasirimali.

Akiuliza swali bungeni jana, Khalifa alitaka kujua ahadi iliyokuwa imetolewa na serikali kuwa, Zanzibar nayo itahusishwa na mpango wa ‘Mabilioni ya JK’, imefikia wapi.

Katika maelezo yake, serikali ilisema kuwa ipo hatua za mwisho za kupeleka sh milioni 200 kwa kila Mkoa wa Zanzibar.

Naibu Waziri wa Fedha, Abdisalaam Issa Khatib alisema serikali hivi sasa iko katika zoezi la kukamilisha utaratibu kwa ajili ya kuanza awamu ya pili ya mpango huo, ambayo itajumuisha pia Zanzibar.

Alisema maandalizi ya kuiingiza Zanzibar katika mpango huo, ni pamoja na kukubaliana kuhusu benki itakayotoa mikopo hiyo, utaratibu wa usimamizi na utaratibu wa mpango huo kama ilivyo kwa Tanzania Bara.

Khatib alisema kuwa katika bajeti yake ya mwaka 2007/08 na katika mwaka 2006/07, serikali ilianzisha awamu ya kwanza ya mpango maalumu wa kuwawezesha wananchi kupata mikopo ya masharti nafuu kupitia benki za CRDB na NMB kwa kudhaminiwa na serikali.

Alisema kuwa mpango huo ulianza Aprili 2007 baada ya kukamilika kwa taratibu husika, awamu hiyo bado inaendelea.