SEPTEMBA 25 hadi Agosti mosi mwaka huu, katika Jiji la Osaka Japan, kutarindima Mashindano ya Dunia ya Riadha.
Mashindano haya ni makubwa kuliko yote katika kalenda ya Shirikisho la Riadha la Kimataifa (IAAF), ambayo hufanyika kila baada ya miaka miwili.
Mara ya mwisho mashindano haya yalifanyika jijini Helsink, Finland mwaka 2005 ambako Tanzania iling’ara kwa mwanariadha Christopher Isegwe kutwaa medali ya fedha, baada ya kushika nafasi ya pili.
Ushindi huo uliitoa kimasomaso Tanzania na kuitangaza kimataifa katika medani ya michezo, ambako mwanariadha huyo mbali ya kupewa zawadi mbalimbali, mwajiri wake, Jeshi la Magereza Tanzania, lilimpandisha cheo kutoka warder hadi sajenti kutokana na kitendo chake hicho cha kishujaa.
Mwaka huu, Tanzania imebahatika tena kuwa na wachezaji waliofuzu viwango vya kushiriki mashindano hayo, ambako timu ya taifa inaundwa na wachezaji tisa.
Kocha na meneja wa timu hiyo, Morris Okinda, anasema Tanzania inakwenda Japan ikiwa na matumaini makubwa ya kufanya vema.
Okinda anasema Tanzania safari hii, inakwenda ikiwa na matumaini makubwa kutokana na kwamba, mwaka huu inawakilishwa na timu kamili ya marathon.
Anasema manufaa ya kwenda timu kamili ni kutokana na kuwa kuna zawadi za aina mbili, ya ushindi wa jumla na wa mtu mmoja mmoja.
“Hivyo timu yetu itakuwa ikicheza kwa malengo mawili, aidha kwa mwanaridha mmoja mmoja kutaka kufanya vema kwa kushika nafasi za juu, au kwa timu nzima kushika nafasi za juu na hivyo kushinda ushindi wa jumla,” anasema.
Kocha huyo anaongeza kuwa, wanariadha watakaoshika nafasi 20 za mwanzo watakuwa wamekata tiketi ya Olimpiki mwakani nchini China.
Okinda anasema tegemeo kubwa safari hii ni katika mbio za marathon ambako wamefanikiwa kupata timu nzima ambayo ni wachezaji sita.
“Mwaka 2005 timu ilienda ikiwa haijakamilika, hivyo mchezaji kama Isegwe na wengineo, walikuwa wakikimbia kwa lengo la kupata ushindi binafsi ‘Individual’, ambako safari hii itakuwa tofauti, kwani watakuwa timu kamili,” anasema.
Kocha huyo ambaye ni mwanariadha mahiri wa mbio za vihunzi wa zamani, anasema kati ya wachezaji tisa wa kikosi chake, sita ni wa marathon na watatu wanakimbia mbio za uwanjani ‘track’.
Wachezaji wanaounda timu ya Tanzania ni pamoja na mshindi wa medali ya fedha katika mashindano yaliyopita, Christopher Isegwe, Samson Ramadhani, Getuli Bayo, Michael Tluway, Andrea Sambu, Andrea Silivin ambao wanaunda timu ya marathon, Samwel Mwera anayekimbia mita 800, Dickson Marwa mita 10,000 na mwanadada pekee, Zakia Mrisho anayetimua mita 5,000.
Okinda anasema anakiamini kikosi chake, kutoka na kila mchezaji kuwa na sifa na uwezo tofauti, ambako mbali ya Isegwe kuwa mshindi wa medali ya fedha katika mashindano yaliyopita, pia wanariadha wengine ni moto wa kuotea mbali, hasa kutokana na jinsi wanavyojiandaa jijini Arusha.
Kocha huyo anamtaja Sambu kuwa ni kati ya wanariadha wa marathon, ambao wamekuwa wakifanya vema hapa nchini.
“Sambu ni mwanariadha mzoefu na muda mwingi hajawahi kuliwakilisha taifa, hivyo tuna matumaini katika mashindano haya, atafanya vema na kuipeperusha bendera ya Tanzania,” anasema.
Okinda anasema Sambu amefuzu kushiriki mashindano hayo ya dunia baada ya kufikia viwango, ambako alishika nafasi ya kwanza katika mbio za marathon za Belgrade, baada ya kutumia saa 2:14.54.
Kwa upande wa Silvin, anasema ni mwanariadha anayeibukia kwa kasi na amekuwa akifanya vema katika mashindano ya hapa nchini, ambako mapema mwaka huu alishika nafasi ya kwanza katika mbio za Kilimanjaro Marathon.
Mwanariadha huyo amefuzu baada ya kukimbia kwa saa 2:14.58 na kuachana kwa sekunde nne na Sambu katika mbio za Belgrade Marathon.
Okinda anasema, nyota mwingine katika kikosi chake ni Samson ambaye ni mshindi wa medali ya dhahabu katika mashindano ya Jumuiya ya Madola, mwaka jana huko Melbourne, Australia.
Anasema Samson amefuzu baada ya kushika nafasi ya kwanza katika mbio za Lake Biwa huko Japan, baada ya kutumia saa 2:10.34.
Kwa upande wa Bayo, ambaye ni mara yake ya kwanza kushiriki mashindano hayo, amefuzu baada ya kutumia saa 2:14.54 Amsterdam Marathon, Uholanzi.
Okinda anasema Tluway amefuzu baada ya kutumia saa 2:16 katika mbio za Sao Paulo nchini Brazil, ambazo ni kati ya mbio ngumu, hasa kutokana na joto kali lililoko katika mji huo.
Kocha huyo anasema mbali ya bunduki hizo ambazo anazitegemea kwa upande wa marathon, pia anao nyota ambao watatoana jasho kwenye mbio za uwanjani.
Anasema Mwera, ana matarajio ya kufanya vema hasa kutokana na muda aliofuzu wa dakika 1:46.56 huko Rome, Italia, sambamba na Marwa mwenye rekodi ya dakika 27.36 na Zakia ambaye majuzi amefuzu baada ya kutumia dakika 15: nchini Sweden.
Kocha huyo anasema timu hiyo inajinoa jijini Arusha ambako, Agosti 14 itahamia Dar es Salaam na kuweka kambi Chuo cha Takwimu, Mwenge jijini Dar es Salaam, kabla ya kukwea pipa Agosti 21 kwenda Osaka Japan tayari kwa kinyang’anyiro hicho.
Je, wanariadha hao watawapa raha Watanzania katika mashindanbo hayo, kama ilivyokuwa kwa Isegwe mwaka juzi?