MWISHONI mwa wiki, ilikuwa ni hitimisho la michuano ya Kombe la Tusker iliyoanza kutimua vumbi jijini Mwanza kuanzia Julai 28.
Michuano hiyo iliyofikia tamati Jumamosi iliyopita, ilishirikisha jumla ya timu sita. Miongoni mwa hizo, nne ni kutoka Tanzania na mbili kutoka Kenya na Uganda.
Uganda iliwakilishwa na Sports Club Villa huku Kenya ikiwakilishwa na Tusker FC.
Kimsingi, uwepo wa michuano hii, ni kukuza kiwango cha soka kwa upande mmoja, ingawa kwa upande mwingine ni malengo ya kibiashara.
Pamoja na hayo, kitendo cha Kampuni ya Bia ya Afrika Mashariki (EABL), kuamua kutumia mamilioni ya fedha katika udhamini wa michuano hii, kinapaswa kupongezwa.
Tunayasema haya tukizingatia kuwa, kupitia michuano hii, timu shiriki mbali ya kupata mazoezi, hivyo kujiimarisha kwa ligi za nchi husika, pia kwa timu zilizofanya vema, zimetunisha mifuko yao.
Kwa mfano kitendo cha Yanga kutwaa ubingwa, imefanikiwa kupata kiasi cha sh mil. 25, mshindi wa pili sh mil. 10 na sh mil. 5 kwa mshindi wa tatu.
Licha ya kuwako kwa dosari au mapungufu kadha wa kadha katika michuano hiyo, bado tunaamini wachezaji wa timu husika, wamejifua vya kutosha.
Kwa timu za Yanga, Mtibwa Sugar, Prisons na Kagera Sugar, tunaamini zimenufaika vya kutosha na michuano hii hasa tukizingatia kuwa, ni kipindi kifupi kabla ya kuanza kwa Ligi Kuu Septemba 15.
Ni wazi, kwa vile michuano ya Tusker ilishirikisha timu mbili za kigeni, hatutakosea kuiita ya kimataifa na ndiyo maana ilikuwa na ushindani mkubwa.
Kama hivyo ndivyo, ndiyo maana tunaipongeza timu ya Yanga kwa kutwaa taji hilo, hivyo kulibakisha taji hilo katika ardhi ya Tanzania tangu kuanzishwa kwake mwaka 2001.
Licha ya kushirikisha timu kutoka nje ya Tanzania, tangu kuanzishwa kwake, taji hilo limetwaliwa na timu za Tanzania ambazo ni Simba, Kagera Sugar na Yanga.
Hivyo, kwa vile Yanga ni ya Tanzania, kwa hakika inastahili kupongezwa kwani ni mafanikio yaliyotokana na juhudi kubwa ya pamoja kuanzia wachezaji makocha na viongozi wa klabu hiyo.
Tunatoa pongezi kwa Yanga tukirejea kwenye mazingira ya michuano husika ya safari ambayo kwa hakika, ilikumbwa na majaribu makubwa.
Wito wetu kwa wachezaji na viongozi wa timu hiyo, ni kuuchukulia ushindi wa Tusker kama changamoto katika kujipanga vema kwa Ligi Kuu itakayoanza Septemba 15.
Hii ni baada ya Simba ambayo uwepo wake katika michuano hiyo pamoja na mtani wake wa jadi, Yanga, ndiyo huwa msisimko wenyewe.
Katika hali ya kawaida, kitendo cha Simba kujiweka kando safari hii huku ikijenga hoja ya kwanini imefikia uamuzi huo, ingewezekana hata timu nyingine kujitoa.
Hata hivyo, ingawa hatuungi mkono kitendo cha Simba kujitoa kwenye michuano hii kwa vile si cha kiuanamichezo, pia tunasema iko haja kwa waaandaaji wa michuano ya Tusker kurekebisha dosari.
Tunayasema haya, kwa kuzingatia kuwa, wakati fulani, yawezekana mtu akajifunza hata kupitia makosa, hivyo hatudhani kama michuano hii, ilifana kwa asilimia 100.
Ipo haja sasa kwa wadhamini hao kufanyia kazi dosari hizo pamoja na kujenga utaratibu wa kuweka mambo wazi ili kuepukana na kile kilichotokea safari hii.
Hatuungi mkono madai ya Simba, kwa vile hatuna ushahidi nayo, lakini wahusika (wadhamini), pia wanapaswa kuyachukua madai ya Simba kama changamoto kwao.
Tukirejea kwa upande wa Yanga, ushindi wa Tusker uwe changamoto ya kujipanga zaidi kwa ajili ya maandalizi ya Ligi Kuu iliyopangwa kuanza Septemba 15.
Kwa vile huu ni ubingwa wa kwanza kwa uongozi wa klabu hiyo ulio chini ya Mwenyekiti, Imani Madega, ndiyo maana, tunasema hongera Yanga kwa ushindi, jipangeni upya.