logo spc.r_ad0
sp.b_ad0
blu.strip
spc.bt_blu.strip
HABARI MPYA KITAIFA DAR MIKOANI TAHARIRI MAKALA MICHEZO
sp.b_menu
ban
sp.b_ban
jumapili, 27 Januari 2008
Pekua Tovuti
sp.t_sech.box sp.tafuta_w_tuma sp.t_tuma sp.r_tuma
sp.b_box sp.b_tuma
sp.b_F1
h.sep1
sp.r_men
sp.t
Gazeti la Jana
Matangazo
Bei zetu
Wasiliana nasi
Tuma habari
sp.b_tuma
sp.l_men
h.sep1
sp.l sp.t sp.r
LOGIN
sp.men.l sp.men.t sp.men.r
Username
sp.b_user
sp.t-word
Password
sp.b_word
sp.t_btn
sp.b_btn
sp.b
h.sep1


Dhambi ya choyo
Mwinjilisti Kamara Kusupa


KUNA tofauti kati ya uchoyo na choyo, pia kuna tofauti kati ya mtu mchoyo na mwenye choyo. Kwa tafsiri rahisi mtu mchoyo ni yule mwenye tabia ya unyimi, ama mwenye ubinafsi wa kutotaka kumgawia mwingine kutoka kwenye vitu alivyonavyo.

Lakini mwenye choyo ni mbinafsi zaidi, ni yule ambaye kutokana na mbegu ya ubinafsi ndani yake, hataki wala hayuko tayari kumgawia mtu mwingine kile alichonacho, na hataki wala hayuko tayari mtu mwingine akapata kutoka vyanzo vingine.

Hii tafsiri ni yangu, naamini na wengine nao wanaweza kutoa tafsiri zao na huenda zikawa tofauti na tafsiri iliyoandikwa kwenye kamusi, kwani kamusi si mwanzo na mwisho wa yote.

Lakini chukulia mfano ufuatao: Mtu (mume au mke) kwa sababu anazozijua yeye anamwacha mwenziwe, lakini hataki mwenzake apate rafiki ama mchumba mwingine. Hicho ni choyo.

Ama mtu amemfukuza kazi aliyekuwa mfanyakazi wake, lakini pamoja na kumfukuza bado hataki akapata kazi sehemu nyingine, hicho ni choyo, ni tofauti na uchoyo wa mtu kumnyima mtu mwingine mema aliyonayo, hatosheki.

Yesu aliwatahadharisha wanafunzi wake akisema, ‘jihadharini na choyo kwa sababu uzima wa mtu hauko katika wingi wa vitu vyake’. Baadaye Yesu akahitimisha mada yake kwa kutoa simulizi ya kisa cha kweli kati ya tajiri mmoja katika jamii ya Kiyahudi na masikini mmaja aliyekuwa akiitwa Lazaro.

Yesu alisimulia yale aliyoyaona na kuyasikia huko kabla ya kuja kwake hapa duniani, ndiyo maana anataja majina ya watu halisi kama vile Abrahamu (baba wa Wayahudi), Musa na manabii.

Chanzo cha mada hii ya choyo kilitokana na chokochoko ya mtu mmoja kati ya hao waliokuwa wakimsikiliza Yesu mkutanoni, alianza mwanamke mmoja ambaye kwa jazba alipaza sauti yake na kusema, ‘heri tumbo lililokuzaa na matiti uliyoyanyonya’.

Naye Yesu akamjibu, ‘heri yao wasikiao na kuyashika maneno ya Mungu’.

Hapo ndipo mwanamke mmoja akamuomba Yesu akisema, ‘mwalimu mwambie ndugu yangu anipe urithi wangu’, Yesu akamjibu. ‘Ni nani aliyeniweka mimi niwe mwamuzi juu ya mambo yenu (ya maslahi, faida na malimbikizo)?’

Hapa msisitizo ni wangu, yaelekea ndugu wawili walikuwa wamedhulumiana mali za kurithi, yule aliyedhulumiwa alihofu kutumia mkondo wa sheria na nguvu za dola, kwamba kutokana na kiwango cha rushwa iliyokuwapo enzi hizo, nduguye aliyedhulumu angeweza kutumia sehemu ya mali hiyo inayogombewa akahonga hata kupata haki.

Kwa hiyo mhanga akatamani kutumia nguvu za dini akiamini kwamba endapo nduguye angeendewa na mtu mwenye ushawishi wenye nguvu kama ule alioushuhudia kwa Yesu na kisha kumshawishi aachane na mpango ule, huenda angeafiki na kuepuka kushitakiana mahakamani.

Lakini kinyume chake, Yesu akamkemea na kujiweka mbali na ufalme unaojihusisha na maslahi ya dunia, ndiyo maana alisema ni nani aliyeniweka mimi niwe mgawaji wa mali zenu?

Kisha Yesu akawageukia wanafunzi wake na kuwaonya akisema, jihadharini na choyo kwani uzima wa mtu hauko katika wingi wa vitu vyake. Akaongeza kuwa mtu mmoja tajiri, shamba lake lilizaa sana na kutokana na uzalishaji huo uliozidi kawaida, liliibuka tatizo lililompa kero hadi kuwaza na kulalama afanyeje maana hakuwa na mahali pa kuweka mali yake.

Akafikia hitimisho la kuvunja ghala zake zote (za zamani) na kujenga ghala mpya ambalo lingeweza kuhifadhi akiba yote ya chakula chake, hapo akaridhika na kujipongeza kwamba nafsi yake ina vitu vingi ilivyojiwekea akiba kwa miaka mingi hivyo ipumzike, ile, inywe na kufurahia maisha.

Lakini Mungu akamwambia ‘mpumbavu mkubwa wewe, usiku huu nawatuma malaika kuja kuchukua roho yako, sasa hivyo vitu ulivyojilimbikizia vitakuwa vya nani?’ Mwisho wa kunukuu.

Hapa tunaona tofauti ya mitizamo, Mungu siku zote mtizamo wake ni tofauti na mtizamo wa binadamu, ndiyo maana hata mtu anayeona mambo kama Mungu anavyoyaona, mara zote huhitilafiana na watu wengine wenye mtizamo wa kibinadamu.

Kwa ajili hiyo, hata katika kushughulika na mambo yanayohusu nchi zetu na dunia yote kwa ujumla, inabidi kupata mtizamo wa ki-Mungu kwa vile Mungu anaiona Tanzania tofauti na Watanzania wenyewe wanavyoiona.

Hivyo hata anayeonekana mpumbavu katika dunia hii, mbele za Mungu si mpumbavu, na vivyo hivyo anayeonekana mjanja na mwenye kufanikiwa katika dunia yetu, mbele za Mungu aweza kuwa ndiye mpumbavu wa kutupwa.

Katika kisa hiki cha tajiri na mali zake, mtu ana mipango yake ambayo kibinadamu ni mipango mizuri ya kuendesha maisha sawa sawa na tajiri, uamuzi juu ya changamoto iliyokuwa inamkabili kuhusu jambo la kufanya baada ya uzalishaji kuongezeka na hitimisho lake kwamba atajitengenezea mazingira mapya yatakayoendana na kiwango cha uzalishaji.

Akiisha jijengea mazingira ya kuwa anayo ‘guarantee’ ya kuishi kwa siku nyingi na kufurahia maisha, hitimisho lake linaonekana kama upumbavu wa kupindukia mbele za Mungu, na ili kudhihirishia kwamba mawazo yake ni upumbavu uliotofautiana na ukweli na uhalisi wa maisha, Mungu naye baada ya kuyasoma mawazo yake, anamwambia ‘usiku huu watakuja wajumbe na ujumbe wa kuitaka roho yako’.

Kuna kila uelekeo kwamba, tajiri yule anayesimuliwa kwenye kisa hiki cha uzalishaji unaozidi kawaida, ndiye yule yule aliyeishi jirani na maskini aliyeitwa Lazaro.

Tajiri huyu siku zote alikula kwa anasa na kuvaa mavazi ya kifahari sawa kabisa na kawaida ya walimwengu wengi ambao hupenda kujipambanua na kujitofautisha na wanadamu wengine kwa kumiliki vitu vya thamani, wakiamini kwamba hali hiyo inawaongezea heshima na utukufu katika maisha ya kidunia.

Haikuishia hapo, tajiri huyu alisumbuliwa na dhambi ya choyo, kutokana na ufunuo alioutoa Yesu, yaonyesha ni dhambi ya choyo.

Utajiri kama ulivyo, si dhambi wala kitu kibaya cha kumpelekea mtu mahala pa mateso kwani kulingana na kisa hiki, hata Abrahamu alikuwa tajiri wa fedha, mifugo, dhahabu na wafanyakazi wengi.

Ni Mungu aliyemzidishia hayo yote, lakini kwa ufunuo huu wa Yesu, Abrahamu yuko peponi, na tajiri yule yuko kuzimu mahala pa mateso. Je, ilikuwaje? Na nini kilichomfikisha mahala pale? Jibu linapatikana kwa Lazaro na kwenye mahojiano kati yake tajiri na Abrahamu.

Imeandikwa ya kwamba baada ya tajiri yule kufa, akiwa kuzimu aliinua macho yake na kumuona Lazaro akiwa kwenye himaya ya Abrahamu akifurahi, akalia na kusema. Eeh Baba Abrahamu, (hivyo ndivyo Wayahudi walivyotamka) naomba unihurumie kwa kuwa na mimi ni wa uzao wako.

Abrahamu akamuuliza, ‘wataka nikufanyie nini?’ Akajibu, ‘umtume huyo Lazaro achovye kidole chake kwenye maji, na aje, auguse tu ulimi wangu nami nijisikie burudani japo kwa nukta moja.’

Hapa tunapata fundisho kwamba baada ya mtu kufa hakuna kinachobadilika, kumbukumbu zake hazifi wala wajihi wake na sura yake haipotei.

Ndiyo maana tajiri aliweza kumkumbuka Lazaro kwamba alikuwa jirani yake duniani na pia kumtofautisha na Abrahamu. Pia alikumbuka ndugu zake watano na namna ya maisha aliyowaacha nayo.

Abrahamu alijibu kwamba, ‘kumbuka ulivyokuwa duniani enzi za furaha yako na ulipokuwa ukijali mali zako. Je, ulimjali huyo Lazaro? Je, ulimthamini?’ Ni Lazaro aliyefunua mambo ya tajiri yule kwamba duniani alikuwa radhi kuwapa mbwa makombo ya chakula yaangukayo kutoka mezani kwake, hakuruhusu kabisa Lazaro jirani yake japo ajishibishe kwa makombo tu ambayo yeye tajiri hakuyahitaji.

Hakumpa Lazaro maskini aliyekuwa anaumwa vidonda mwili mzima, akafa kwa njaa mbele ya jirani yake, aliyekula, akashiba na kusaza.

Tajiri yule alipokumbushwa juu ya matendo yake ya jinsi alivyokuwa akitumia, hakuendelea tena kumuomba Abrahamu amtume Lazaro kumburudisha, badala yake akabadilisha, akaomba Abrahamu amtume Lazaro arudi duniani kutoka kwa wafu, ili akawashuhudie ndugu wa tajiri yule kwani alikumbuka kwamba ameacha ndugu zake watano wenye kuishi maisha kama yake.

Kwamba nao wasije wakaishia motoni, lakini ombi hili halikufaulu, maana Abrahamu alimjibu kwamba duniani kuna sheria ya Musa (tarati ya Musa) nduguze na wafuate hiyo kwa kuwa ndiyo mwongozo wa maisha kwa Wayahudi wote yaani wana wa Abrahamu.

Yule tajiri akajenga hoja kwamba kwenye torati ya Musa, haikuandikwa dhambi ya uchoyo badala yake zinaelezwa dhambi zingine tu za uuaji, uzinzi, uongo, wizi, kuabudu sanamu n.k.

Ndipo Abrahamu alipomjibu tena akisema, kama unadai dhambi iliyokuleta hapo haikuandikwa popote kwenye amri kumi za Mungu basi duniani kuna manabii, ndiyo kazi yao kutabiri, kuonya na kuwahubiri watu yale yasiyoandikwa, lakini Mungu anataka yafanyike huko duniani.

Tajiri akaitetea hoja yake ya kutaka Lazaro atumwe duniani kwa kudai nduguze ni watu wa dharau, hawawaheshimu wala kuwajali manabii kutokana na kiburi cha utajiri wao na pia mwonekano wa manabii wa Mungu ni wa kawaida sana.

Ni watu wasiojipambanua kwa lolote na raia wengine, kwahiyo inakuwa vigumu kwa watu matajiri kama wale kuwaamini manabii isipokuwa kama akitumwa na mtu kutoka kwa wafu, kiasi kwamba kaburi lifunguke na maiti ya mtu aliyekufa hata matajiri.

Lakini Abrahamu akahitimisha kuwa kama hawawasikilizi manabii, hata mtu akitoka kwa wafu hatafaulu kuwashawishi waachane na mtindo wao mwovu wa maisha.

Hapo ukawa mwisho wa mjadala. Sijui leo hii ni wanadamu wangapi ambao wangependa kumsikiliza mhubiri aliyefufuka kutoka kwa wafu, maana ni ukweli usiopingika kwamba watu wengine kutokana na kiburi cha utajiri wa madaraka na umaarufu, wamefikia kiwango cha kutojali mahubiri ya aina yoyote wala hawataki kusikia ujumbe wa aina yoyote isipokuwa ule unaohalalisha yale waliyoyazoea. Katika mazoea kuna hasara ya milele!!

Mwandishi wa makala hii anapatikana kwa simu 0786 311422


h.sep
juu sp.b
Habari Mpya  |  Kitaifa  |  Dar  |  Mikoani  |  Tahariri  |  Makala  |  Michezo  |  Matangazo  |  Webmaster
Copyright 2008 © FreeMedia Ltd.
Free media limited
mtaa wa Mkwepu na Makunganya, jengo la Bilicanas, gorofa ya kwanza, SLP 15261, Dar es salaam, Tanzania
simu +255-22-2126233  •  faksi +255-22-2126234  •  Selula  0713 296570