logo spc.r_ad0
sp.b_ad0
blu.strip
spc.bt_blu.strip
HABARI MPYA KITAIFA DAR MIKOANI TAHARIRI MAKALA MICHEZO
sp.b_menu
ban
sp.b_ban
jumapili, 27 Januari 2008
Pekua Tovuti
sp.t_sech.box sp.tafuta_w_tuma sp.t_tuma sp.r_tuma
sp.b_box sp.b_tuma
sp.b_F1
h.sep1
sp.r_men
sp.t
Gazeti la Jana
Matangazo
Bei zetu
Wasiliana nasi
Tuma habari
sp.b_tuma
sp.l_men
h.sep1
sp.l sp.t sp.r
LOGIN
sp.men.l sp.men.t sp.men.r
Username
sp.b_user
sp.t-word
Password
sp.b_word
sp.t_btn
sp.b_btn
sp.b
h.sep1


Bunge linapolalia ufisadi, wananchi kirago
Christopher Nyenyembe


SIDHANI na sifikirii kama anayefurahia yanapojitokeza mambo mazito kama haya ya sasa, wananchi wanapoona jinsi nchi inavyoangukia mikononi kwa mafisadi wasiokuwa na huruma, wanaoendelea kuneemeka kwa fedha za umma huku makabwela wakiachwa hoi.

Wananchi hawa wana kiu kizito, wanataka kuwasikia wabunge wao katika kikao kijacho wakiwaambia wazi na wakikiri hadharani kuwa hawajaulalia ufisadi, tangu walipochaguliwa kwa mbwembwe katika Uchaguzi Mkuu mwaka 2005.

Wananchi hawa maskini wasiokuwa na uwezo wa kununua hata mfuko mmoja wa mbolea ya ruzuku ya serikali, wasioweza kulipia gharama za matibabu, wasioweza kulipia gharama za kuunganishiwa umeme na wasioweza kuwalipia watoto wao ada za shule na vyuoni, wanataka kuwasikia wabunge wao watasema nini kuhusu ufisadi ambao sasa umethirika kuwepo serikali.

Wanataka waambiwe huu ufisadi unaoendelea kutajwa kila kona na wengine kutolewa kafara, kuna wepi wengine, wangapi kwenye chujio la kuondoa makapi serikalini na kuwaacha viongozi safi na waadilifu?

Wananchi wanataka kujua kwa undani tume ya kuchunguza mkataba wa Richmond imefikia wapi na kina nani wanahusika kuiingiza serikali kwenye mkenge huo wa ajabu, huku watu wakilipwa mabilioni ya fedha bila umeme kuzalishwa, wananchi wanataka kujua.

Wananchi wanataka kujua kama wabunge wao hawajalalia godoro la ufisadi na kuwaacha wao wakiwa wamelalia kirago kilichotengenezwa kwa majani ya mgomba au matete, wawaeleze tume ya kuchunguza ununuzi wa rada imeishia wapi?

Wananchi wanataka kufahamu mlolongo wa tume na kamati kadhaa zinazoundwa na kutumia mamilioni ya fedha katika uchunguzi uliowazi, wabunge wao watawaeleza nini juu ya kamati zilizoundwa na Rais Kikwete kuchunguza na kuwatia hatiani wale wote waliohusika na ubadhirifu kule Benki Kuu Tanzania (BoT).

Sina shaka, kiu ya wananchi haiwezi kukoma kwa maji au asali kama hawajaelezwa kinagaubaga, ndege ya Rais ya kifahari iliyonunuliwa kwa mabilioni ya fedha ambayo haiwezi kutua kwenye viwanja vya makabwela, wabunge wanapaswa kuwajibu kwani wao ndio wawakilishi wao.

Hawataishia hapo, wananchi wanataka kujua tume iliyoundwa kuchunguza uuzaji wa nyumba za serikali imefikia wapi na wale walioshindwa hata kuzilipia nyumba hizo nao wako wapi na ngapi zimerejeshwa baada ya kuuzwa kwa bei ya kutupwa.

Hawangoji kupiga hodi ili kuruhusu mwanya wa mafisadi hao waikimbie nchi, wananchi wanataka kujua tume ya kuchunguza mikataba mibovu ya madini kwa lugha nyepesi Kamati ya Rais aliyoiunda ya kuchambua mfumo wa usimamizi katika sekta ya madini itawaambia nini wananchi.

Ni dhahiri kwa mlolongo huu mrefu wa tume kwa tume au tuziite matume, zina nafasi kubwa za kuwapa uelewa mkubwa wabunge wetu ambao kwa umakini mkubwa wanapaswa kujua nchi hii inakoelekea, kama imesimama, inakwenda au imelala ?

Pamoja na semina elekezi kadhaa zilizotolewa na serikali kwa nyakati tofauti karibu kwa watendaji wote wa serikali wakiwemo wabunge, nini dhana ya utawala bora na uwajibikaji wenu wanaouhitaji wananchi kama mnafika bungeni na kuchekeana kwa mambo ya kiitikadi?

Wananchi wanajua wao ndio waliowaingiza ninyi madarakani na wanajua jinsi walivyoweza kuichagua CCM kwa asilimia zaidi ya 80 ya kura, hilo wanalijua sana na hawahitaji ushahidi.

Wananchi wanajua serikali iliyopo madarakani ni serikali ya CCM, wanajua kuwa ndani ya Bunge idadi kubwa ya wabunge wanatoka CCM, wa upinzani ni wachache.

Wanajua idadi hiyo ndogo ya wabunge wa upinzani ndiyo iliyowasha moto kwa kuiambia serikali kuwa nchi inatafunwa, kuna mafisadi wanaua uchumi wa nchi, hao wengi walishangaa na kuwakandamiza wenzao kuwa ni waongo.

Sasa nawashauri wabunge wa CCM kama hawataki kulalia godoro la ufisadi, wageuke mbogo, waieleze serikali kuwa muda umefika, Watanzania wamechoka, wanataka kuona mali ya umma inawanufaisha wao.

Waambieni serikali kuwa ahadi zote za chama zitawezaje kutimizwa kama nchi imekabwa koo na mafisadi, kwamba hayo mabilioni ya fedha yanayochotwa na mafisadi yangeweza kutengeneza barabara ya Tunduma hadi Sumbawanga, Nkasi hadi Mpanda?

Umefika wakati kwa wabunge wanaosali pamoja kabla ya kuanza shughuli za Bunge kurudi kwa wananchi kuwaomba radhi babada ya kushindwa kuwafichua mafisadi waliokuwa wakiwajua muda mrefu.

Sala ya kuliombea Bunge inayoongozwa na Spika haikutungwa kwa unafiki, ilitungwa kuliwezesha Bunge kuendesha shughuli zake kwa ukweli, uwazi na bila vificho na hila, kwa imani kuwa Mungu yupo mbele ya wabunge kwa ajili ya kulitakia mema taifa.

Kinyume chake sala ya kuliombea Bunge imegeuzwa kuwa sala ya kuwalinda mafisadi ambao baadhi yao wamo bungeni, lakini wabunge hawawezi kuweka hoja mbele ya Spika inayohusu ufisadi kwa sababu baadhi ya wenzao wanaguswa na kampuni zilizochota mabilioni BoT.

Kama hamjawalalia mafisadi na kama mpo tayari kuwaondoa wananchi katika umaskini wa kulalia virago huko vijijini, nasema hivi, huu ndiyo wakati muafaka wa kuwa na Bunge la mfano litakaloweza kuendeleza mapambano ya kufichua mafisadi bila aibu.

Kazi iliyopo mbele yenu katika uchaguzi mkuu ujao wa mwaka 2010 ni kubwa kuliko mnavyotarajia, Inshallah kama Mwenyezi Mungu atazihifadhi vyema nyoyo zetu hadi muda huo, kwa watakaoweza kubadilika, mwaka huo utakuwa wa mafanikio makubwa kwao kisiasa.

Nataraji kikao kijacho cha Bunge kitaendeleza mapambano hayo kwa kuwaunga mkono wabunge wachache wa upinzani, ambao mara kadhaa wamekuja na hoja zilizokuwa zikibezwa bungeni, lakini walipozipeleka kwa wananchi, matokeo yake ndio haya.

Wananchi wanataka kuliona Bunge lenye nguvu na hoja nzito juu ya mustakabali wa nchi, hawataki kuona baadhi ya watendaji serikalini wakipita na kuwaandalia vikao vya siri ili kuwaweka sawa, juweni kuwa jua halisimami hata kidogo.


cnyenyembe@yahoo.com
0754 301864


h.sep
juu sp.b
Habari Mpya  |  Kitaifa  |  Dar  |  Mikoani  |  Tahariri  |  Makala  |  Michezo  |  Matangazo  |  Webmaster
Copyright 2008 © FreeMedia Ltd.
Free media limited
mtaa wa Mkwepu na Makunganya, jengo la Bilicanas, gorofa ya kwanza, SLP 15261, Dar es salaam, Tanzania
simu +255-22-2126233  •  faksi +255-22-2126234  •  Selula  0713 296570