MWANAMUZIKI maarufu kutoka Zimbabwe, Oliver Mtukudzi ‘Tuku’, anatarajiwa kufanya onyesho ‘live’ katika Jiji la Dar es Salaam na Arusha.
Kwa mujibu wa waratibu wa ziara hiyo, Kampuni ya Red Promotion Limited-Bohemia, Oliver ‘Tuku’ Mtukudzi atafanya onyesho la kwanza katika ukumbi wa The Marquee ndani ya Hoteli ya Movenpick, Ijumaa ya Februari mosi, na la pili litakuwa katika viwanja vya Leaders Club, Jumamosi Februari 2, kuanzia saa 6:00 mchana hadi saa 12:00 jioni.
Mwanamuziki huyo ambaye anaheshimika mno na kukubalika, ila shaka kama mwanamuziki mwenye sauti ya asili ya muziki wa Afrika, atasindikizwa na burudani nyingine kutoka kwa wanamuziki mashuhuri na mahiri wa Kitanzania na kutoka nje ya Tanzania kama vile Silje Louise kutoka Norway, Jhiko Manyika, a.k.a Jhiko Man, Akudo Impact, Lady Jaydee na Banana Zorro.
Kwa kutumia gitaa lake lenye sauti ya kuvutia, Oliver ‘Tuku’ Mtukudzi amefanikiwa kuendeleza na kuibua aina ya pekee ya muziki unaohusisha mchanganyiko wa hisia kali za muziki wenye asili ya kiroho, muziki wenye sauti na midundo yenye asili ya Kishona, Mbaganga wenye asili ya Afrika Kusini, pamoja na mtindo maarufu wa Zimbambwe wa ‘Jit’.
Kampuni ya Bia Tanzania kupitia bia yake ya ‘Ndovu Special Malt’ ni kati ya wadhamini wakuu wa ziara ya gwiji huyo.
Mtukudzi hivi sasa ametoa albamu yake mpya inayokwenda kwa jina la Tsimba Itsoka, ‘Hakuna miguu, hakuna nyayo’ sentesi rahisi inayobeba msingi wa kila wimbo katika albamu yake, kuwa ‘Kila mtu ana unyayo tofauti.’