logo spc.r_ad0
sp.b_ad0
blu.strip
spc.bt_blu.strip
HABARI MPYA KITAIFA DAR MIKOANI TAHARIRI MAKALA MICHEZO
sp.b_menu
ban
sp.b_ban
jumanne, 29 Januari 2008
Pekua Tovuti
sp.t_sech.box sp.tafuta_w_tuma sp.t_tuma sp.r_tuma
sp.b_box sp.b_tuma
sp.b_F1
h.sep1
sp.r_men
sp.t
Gazeti la Jana
Matangazo
Bei zetu
Wasiliana nasi
Tuma habari
sp.b_tuma
sp.l_men
h.sep1
sp.l sp.t sp.r
LOGIN
sp.men.l sp.men.t sp.men.r
Username
sp.b_user
sp.t-word
Password
sp.b_word
sp.t_btn
sp.b_btn
sp.b
h.sep1


Bila barabara uchumi hautakua
Daniel Misheto


BARABARA nyingi bado ni mbaya mno kiasi cha nyingine kutopitika katika misimu ya mvua. Kutokana na hali hiyo, baadhi ya bidhaa za wakulima hubaki vijijini na hivyo kuwafanya wananchi wazidi kubaki maskini.

Kwa wananchi waliobahatika kutembea katika maeneo mengi ya nchi, watakubaliana nami kuwa bado hakujawa na mchango wa barabara katika kuleta maendeleo yatakayotufikisha kwenye maisha bora kwa kila Mtanzania.

Tunapozungumzia uchumi wa nchi hatuwezi kukwepa kuzungumzia barabara, kwani ndiyo kiungo cha kuunganisha maeneo tofauti ya nchi na hata nchi jirani kama Zambia ambazo zinaweza kufikiwa kwa barabara.

Barabara ndiyo inayoruhusu magari kubeba watu na bidhaa zao wakienda au wakirudi sokoni na kusafiri bila shida. Hivyo, barabara zinapaswa kupewa kipaumbele cha pekee tunapozungumzia maendeleo.

Kabla ya uhuru na miaka kadhaa baada ya uhuru, serikali ilikuwa na idara ya kusimamia ukarabati na uangalizi wa barabara ili kuhakikisha zinapitika wakati wote.

Idara hii ilijenga kambi kadhaa zilizoachana kwa umbali usiozidi kilomita kumi kandokando ya barabara na katika kila kambi kulikuwa na kiongozi mmoja aliyefahamika kama ‘msimamizi’ au ‘mnyapara’.

Huyu alipewa wafanyakazi au vibarua chini yake wanaofanya kazi ya kuchimba na kusafisha mifereji ya maji ya mvua na kadhalika. Kama hiyo haikutosha, kulikuwapo pia matrekta ya kukwangua na kusawazisha barabara mara kwa mara.

Kwa mtazamo wa wengi niliozungumza nao waliokuwepo kipindi hicho, walisema idara hiyo ilisaidia sana maana wakati huo barabara nyingi hazikuwa na lami, hivyo vumbi au mvua vyote vilileta kero kwa watumia barabara. Barabara hizi zilisababisha maeneo mengi ya nchi yasipitike misimu ya mvua.

Faida

Zipo faida za kawaida na pia nyingine nyeti kwa taifa lolote lile liwe limeendelea au linaloendelea. Kazi na faida kuu ya kuwapo barabara ni kurahisisha binadamu kupita wao na mali zao kama njia za kuwafikisha waendako.

Hata leo hii kwa kuwa hatujawa na uwezo wa kuwa na viwanda vya kutengeneza bidhaa, bado mara nyingi tunalazimika kuuza mazao yetu yakiwa ghafi kwa bei ya chini mno. Na katika kufanikisha hili magari ndiyo yamesaidia wananchi kubeba mazao yao na kuyafikisha katika masoko ya ndani.

Ni kupitia barabara hizo kwamba maeneo mengi ya nchi yamesababisha bidhaa kutoka nchi za nje au kutoka nje ya mkoa kama vile saruji, mabati, misumari, nguo, na hata bidhaa za vyakula mbalimbali.

Barabara zimesaidia kujenga mahusiano mazuri na kufahamiana kwa watu wa nchi mbalimbali ambapo wameweza kusaidiana na kufanya biashara baina yao. Hivyo wafanyabiashara wameweza kuunganishwa na wakulima au viwanda.

Unapofika kwenye baadhi ya vijiji kama Ilangali na Huzi katika Wilaya ya Dodoma Vijijini, utajionea jinsi walivyobarikiwa kuvuna mazao mengi hususan mahindi na asali, lakini wanashindwa jinsi ya kuyasafirisha ili yafike sokoni, kutokana na ubovu wa barabara unaosababisha magari kushindwa kufikia katika vijiji hivyo.

Ukifika na kupanda milima ya Upare kama kule Mwala na Lugulu utaona jinsi wananchi wanavyopata shida kubeba mazao yao kichwani hadi Hedaru na Kihurio kuliko na barabara - umbali wa kilomita takriban 30 au 40.

Pia ukitazama ile barabara ya Mkomazi Bendera hadi Same (Kilimanjaro) au ile ya Mzakwe Mundemu hadi Makanda (Dodoma) au ile ya Kilosa, Ilonga hadi Mvomero (Morogoro), nazo haziko katika hali nzuri kutokana na ubovu hasa katika kipindi hiki cha masika.

Nini kifanyike?

Serikali baada ya kipindi cha miaka kama kumi baada ya uhuru, iliamua kuzifunga kambi za Public Works Department (PWD) na kuanzisha Idara ya Ujenzi kusimamia barabara na baadaye kazi ya ujenzi wa barabara zikawa chini ya Wizara ya Miundombinu.

Baada ya kuvunjwa kwa kambi za PWD, maeneo yalikuwa jirani na kambi yaliathirika zaidi, kwani barabara zilizokuwa na matengenezo na uangalizi wa mara kwa mara, hayakupata huduma ile, hivyo barabara zikawa hazipitiki.

Pengine nami niungane na wananchi wanaotaka kurejeshwa kwa idara na kambi za PWD hasa kwa barabara zile ambazo hazina lami ili matengenezo yafanywe mara kwa mara.

Hata hivyo, naamini kujenga barabara nzuri ni jambo jema, lakini si jema sana kama tunasahau na kupuuzia kujenga barabara za vijijini na kwenye miji midogo sehemu walipo watu wengi. Eneo lenye barabara nzuri ni sawa na kumvisha mtoto nguo nzuri ambaye kila mgeni ajaye anatamani kumbeba.

Nasisitiza kwamba kuwa na barabara nzuri nchini ni hatua moja kubwa ya kimaendeleo katika nchi ambayo pia itasaidia kuchochea maendeleo.

Barabara mbovu pia zimechangia sana baadhi ya viongozi kushindwa kwenda kuwatembelea wananchi vijijini na ndiyo sababu ya Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA) kutumia helikopta kumnadi mgombea wao wa nafasi ya urais.

Serikali irejeshe idara ya PWD ikiwa na muundo ule wa zamani kiutendaji na kujenga kambi kwenye barabara kuu zisizo na lami ili zisaidie barabara kupitika wakati wote.


h.sep
juu sp.b
Habari Mpya  |  Kitaifa  |  Dar  |  Mikoani  |  Tahariri  |  Makala  |  Michezo  |  Matangazo  |  Webmaster
Copyright 2008 © FreeMedia Ltd.
Free media limited
mtaa wa Mkwepu na Makunganya, jengo la Bilicanas, gorofa ya kwanza, SLP 15261, Dar es salaam, Tanzania
simu +255-22-2126233  •  faksi +255-22-2126234  •  Selula  0713 296570