MKAZI wa mkoani Tabora, Peter Komba, aliyeng’atwa na mbwa, ameilalamikia Hospitali ya Taifa Muhimbili (MNH) kwa kushindwa kumpatia matibabu, kwa maelezo ya kutokuwa na kibali kutoka kwa ofisa mifugo.
Kijana huyo ambaye aliwasili jijini Dar es Salaam jana, akitokea mkoani Morogoro, alisema kutokana na kutopata matibabu, hali yake inaendelea kuwa mbaya.
Akizungumza na Tanzania Daima jana katika Hospitali ya Muhimbili, alisema aling’atwa na mbwa Februari 6 mwaka huu alipokuwa mkoani Morogoro.
Alisema baada ya kung’atwa alikimbizwa Hospitali ya Kiwanda cha Sukari cha Kilombero na kupewa huduma ya kwanza ambapo alichomwa sindano mbili za tetenasi.
“Baada ya huduma hiyo waliniambia nije Muhimbili ili kuweza kupata matibabu zaidi kwa kuwa hospitali hii ndiyo pekee inayotoa huduma hii, lakini cha kushangaza wamekataa kunipatia matibabu mpaka niwe na kibali kutoka kwa ofisa mifugo,” alisema.
Alisema kutokana na kipato kidogo alichonacho ilimbidi akae hadi jana ndipo alipofika jijini na kwenda Muhimbili.
“Nasikitika nimefika hapa hawataki kunihudumia, wanadai niende Zanaki kwa ofisa wa mifugo ili niweze kupewa kibali. Mimi hapa mjini ni mgeni, sipajui mahali popote,” alisema.
Alisema pamoja na kuwaeleza wauguzi wa hospitali hiyo kuwa ni mgeni jijini Dar es Salaam, walisisitiza kuwa hawawezi kusaidia kwa kuwa huo ndio utaratibu.