MWANAMUZIKI mahiri wa muziki wa kizazi kipya, Banana Zorro, akiwa na bendi yake ya B Band, amewaahidi wapendanao, kuwapa burudani ya aina yake katika onyesho litalorindima Siku ya Wapendanao ‘Valentine’s Day’, Februari 14 kwenye Ukumbi wa Royal Village mkoani Dodoma.
Akizungumza jana kwa simu, Zorro alisema kuwa yeye pamoja na bendi yake wamejichimbia kambini kwa ajili ya kujifua ili kutoa burudani ya aina yake siku hiyo.
Zorro alisema kuwa, anawaahidi wapendanao na wakazi wa mkoa huo na wa jirani burudani ya aina yake, kwani siku hiyo atatumia muda muafaka kuwaonjesha nyimbo mpya ambazo siku hiyo itakuwa ni mara ya kwanza kusikika.
“Nawaomba mashabiki na wapenzi wa muziki wa kizazi kipya, wafike kwa wingi kujipatia burudani ya nguvu kutoka kwetu maana siku hii ni muhimu na ndiyo maana na sisi tunawapenda,” alisema Zorro.
Zorro aliwataka wapenzi wa muziki wa kizazi kipya kujitokeza kwa wingi kupata burudani, vikiwamo vibao vinavyotamba sasa kama ‘Sultan', ‘Dar es Salaam’ aliomshirikisha Chai Jaba, pamoja na ‘Sikuhitaji Wewe’ aliomshirikisha Mwasiti na nyinginezo nyingi.