jumamosi, 16 Februari 2008

Sakana Tuache dhana ya kupeleka watoto kusoma Kenya, Uganda

na Mwandishi Wetu


HADI sasa, bado kuna wazazi ambao pamoja na kuwa na uwezo kifedha, bado wanatawaliwa na dhana potofu kuwa elimu bora inapatikana nchini Kenya na Uganda.

Dhana hiyo ndiyo inayowasukuma Watanzania hao kuendelea kupeleka watoto wao katika nchi hizo ili kupata elimu bora.

Hata hivyo, mwalimu Abel John wa Shule ya Msingi ya Kimataifa ya Sakana, anapingana na dhana hiyo na kuwataka Watanzania wa aina hiyo kuachana nayo.

“Kwanza niwaambie tu wazazi wenye mtazamo wa aina hiyo kuwa, mitaala ya masomo kwa nchi za Uganda na Kenya ni tofauti na ya hapa Tanzania. Tofauti yake ni kwamba mitaala yetu inajulikana na kutumika kimataifa kuliko ya Kenya na Uganda.

“Zamani wazazi walikuwa wakipeleka watoto Uganda na Kenya kwa sababu wao wanatumia zaidi lugha ya Kiingereza, lakini sasa kuna shule kama Sakana ambayo ina walimu wazuri na wenye sifa wanaofundisha vizuri lugha ya Kiingereza na baadhi yao wanatoka Kenya na Uganda,” anasema mwalimu John.

Anataja athari ya kuwapeleka watoto wadogo katika nchi za Kenya na Uganda ni suala la uangalizi wa watoto katika nchi hizo ambazo tumetofautiana nazo sana kimaadili.

Anasema Sakana ni shule ya msingi ya kisasa, ina vifaa kama kompyuta na walimu wenye sifa kama wa shule za Kenya na Uganda, lakini mbali ya kuwa shule, ni kama chuo cha kuwafundisha watoto tabia na malezi mazuri kwani kwa Sakana mwanafunzi ni rafiki wa mwalimu.

“Sakana ni zaidi ya shule, leteni watoto wenu tuwalelee, tunawafundisha watoto tabia na maadili mazuri, tunawafundisha dini zote kwani shule yetu haina itikadi za kidini na mtoto akiguswa na imani ya dini, atakuwa mwoga na mwangalifu katika matendo yake hata katika maisha yake ya utu uzima baadaye.

“Tunataka mtoto akifundishwa aelewe akiwa darasani kutokana na madhali nzuri ya darasa, lakini pia tunahakikisha anakuwa na tabia njema, lugha nzuri si ya matusi na akiwa na lugha ya matusi lazima tumkanye na kumpa ushauri mzuri, wataalam wa ushauri kwa watoto tunao, mwenye tabia ya udokozi tunamjua na kumrekebisha. Hii ndio tofauti kubwa ya Sakana na shule zingine,” anasema mwalimu John.

Anaongeza kuwa, pia wanawafundisha watoto jinsi ya kufua nguo zao za ndani, kutandika vitanda hasa kwa wale wanaoishi shuleni na kwa kipindi cha miezi sita ambayo mtoto huwa mbali na wazazi, anapata fursa na kujifunza maisha ya kuwa mbali na wazazi wake.

Kwa mujibu wa mwalimu John, shule hiyo ilifunguliwa Januari 14 mwaka huu, eneo la Kiluvya Gogoni, kilomita 100 kutoka barabara kuu ya Morogoro.

Anasema lengo la kuanzisha shule hiyo Kiluvya, ni uhaba wa shule za kisasa katika eneo hilo ambalo idadi ya watu wanaoishi katika eneo hilo, inaongezeka kwa kasi.

“Eneo hili halina shule za English Medium, wazazi wanawapeleka watoto wao kwenye shule za maeneo ya Mbezi Beach, Mbagala na mengine ambayo ni mbali, na kumfanya mtoto afike akiwa amechoka hata kabla ya kuanza masomo yenyewe na anaporudi, anashindwa hata kufanya kazi alizoachiwa shuleni kutokana na uchovu,” anasema John.

Anasema shule hiyo pia inachukua wanafunzi ambao tayari walishakuwa kwenye shule za msingi za kawaida kwani wana mafunzo maalum kwa ajili ya wanafunzi wa aina hiyo ili waende sambamba na wenzao walioanza masomo yao katika shule hiyo hiyo.

“Jamii ielewe kuwa hakuna mtoto asiye na akili ila watoto huwa wana matatizo ambayo kama mwalimu hajayajua na kubaini mbinu ya kumsaidia, anaweza asishike masomo darasani na hapo ndipo unaposikia mtoto fulani hana akili,” anasema John na kuwasisitiza wazazi kuwapeleka watoto katika shule hiyo.

John anasema mbali ya walimu wenye sifa, shule hiyo ina vifaa vingi vya michezo, somo la kompyuta linalofundishwa kwa watoto wote, somo la Kifaransa, uwanja mkubwa wa michezo ya aina mbalimbali na mandhari ya kuvutia.

Katika kumjenga mtoto katika elimu ya kujitegemea, John anasema wanawafundisha watoto kilimo kwani wana eneo kubwa la shamba ambalo pia wanatoa mafunzo kwa vitendo kwa ajili ya wanafunzi wao.

Akizungumzia mipango ya baadaye, John anasema wanatarajia kuipanua shule hiyo hadi kufikia sekondari, na kuongeza madarasa katika mikondo mitatu katika kila darasa.

“Sakana tuna muda wa kulea watoto, waleteni watoto wenu hapa na mtashangaa watakavyokuwa tofauti na watoto wengine,” anatamba Mwalimu John.