WABUNGE wameitaka serikali kuwajengea ofisi zenye hadhi katika majimbo yao pamoja na kuwaweka wataalamu wa fani mbalimbali ambao watawasaidia kuratibu shughuli zao.
Wabunge walitoa kauli hiyo juzi walipokuwa wakihitimisha semina inayohusu mwongozo wa kutayarisha mipango na bajeti ya serikali kwa kipindi cha mwaka 2008/09-2010/2011 iliyoandaliwa na Wizara ya Mipango na Fedha.
Mbunge wa Dole, Juma Selemani N’hunga (CCM), alisema ni aibu kwa wabunge kuendelea kutegemea ofisi za wakuu wa wilaya ambazo hupewa ofisi moja, huku ikiwa haina vifaa vya kufanyia kazi vinavyotakiwa na wabunge.
Alisema wabunge ni watu muhimu na wanapaswa kuwa na ofisi zenye vifaa vya kisasa ambavyo vitawarahisishia utendaji kazi wao tofauti na ilivyo hivi sasa ambapo wanatumia vifaa duni visivyokidhi mabadiliko ya teknolojia ya kisasa.
“Kule Marekani kila jimbo lina ofisi yake na kila mbunge ana wasaidizi na wataalamu wasiopungua 15, sasa angalau na sisi tuwe na wataalamu na wasaidizi hao hata kama hawatafikia kama wale wa Marekani,” alisema N’hunga.
Naye Mbunge wa Iramba Mashariki, Mgana Msindai (CCM), alisema ni vema mazingira ya ufanyaji kazi wabunge yakaangaliwa, kwani gharama za maisha zimepanda huku bajeti kwa ajili ya Bunge ikiwa kidogo.
Alisema endapo wabunge wataboreshewa mazingira ya kufanya kazi itawasaidia kuwafikia kwa urahisi wananchi wao sambamba na kurahisisha mawasiliano na baadhi ya viongozi wa serikali.
“Nina uhakika kama mambo yakiboreshwa tunaweza kufanya kazi vizuri na kuwafikia wapiga kura wetu kwa urahisi zaidi,” alisema Msindai.
Aidha, Mbunge wa Lulindi, Suleiman Kumchaya (CCM), alisema mambo ya uboreshaji wa uchumi wa nchi ni lazima uwashirikishe wananchi na ikiwezekana kuwe na benki ambazo zitakuwa zikitoa mikopo kwa Watanzania pekee.
Alisema kwa muda mrefu serikali imekuwa ikiimba wimbo wa kuwa kilimo ni uti wa mgongo, huku ikiwa haiweki mkazo unaotakiwa, hivyo kuchangia kuchelewa kwa maendeleo katika sekta husika.
“Utaratibu wa kusema kila siku kuwa kilimo ni uti wa mgongo halafu hatuweki mipango thabiti ya kukinyanyua tunapaswa tuachane nao,” alisema Kumchanya.
Aidha, wabunge hao waliitaka serikali kuweka utaratibu maalamu ambao utakuwa ukiratibu mipango ya maendeleo na kutoa tathimini ya mafanikio au kushindwa kwake kila baada ya muda fulani.