WAFANYABIASHARA watatu wamekusudia kukifikisha mahakamani Chama Cha Mapinduzi (CCM) Wilaya ya Moshi mjini kwa kushindwa kuwapatia eneo la ujenzi licha ya kuchukua malipo kwa zaidi ya miaka saba.
Wafanyabiashara hao ni Shabani Msuya, Hamza na Haruni Mringo, waliofikia uamuzi huo baada ya kukipatia chama hicho zaidi ya sh milioni 4.8 tangu mwaka 2001 kwa ajili ya ujenzi kwenye mzunguko wa ofisi za wazee wa CCM, lakini hadi sasa wanazungushwa.
Akizungumza kwa niaba ya wenzake, Hamza alisema wote ni wakurugenzi wa Kampuni ya usafirishaji ya Shabaha na kwamba wapo tayari kuachana na mpango wa kukifikisha chama hicho kwenye vyombo vya sheria endapo kitawapatia eneo hilo na kuruhusiwa kujenga.
Licha ya wao kuwa wanaCCM, wanasema imewabidi kuchukua hatua hiyo ili kurudishiwa fedha zao na fidia, hasa baada ya kuona Diwani wa Mawenzi, Lady Kinabo, akitumia eneo hilo kwa ajili ya biashara zake wakati hakuwa miongoni mwa waliounguliwa.
Hamza alisema, jambo linalowasikitisha zaidi ni diwani huyo kuzungushia uzio unaoziba eneo walilojenga kwa ajili ya kuhifadhia mizigo hali inayowalazimu kuomba ruhusa kwake kabla, wanapokwenda kuhifadhi au kutoa mizigo yao na kusema hiyo ni kero kwao.
Alisema kwa kipindi cha miaka saba wanawasiliana na ofisi ya CCM wilaya na ile ya Katibu Mkuu Taifa, lakini hawapati majibu hali iliyowalazimu kumwandikia barua mdhamini wa chama hicho, Peter Kisumo, aliyeahidi kuwasaidia.
Nyaraka mbalimbali ambazo Hamza alizionyesha kwa Tanzania Daima, zinaeleza kuwa kati ya fedha hizo sh milioni 3.9 zililipwa kupitia akauti namba 6590850191 ya CCM Moshi Mjini iliyopo benki ya NBC zikiwa ni malipo ya awali kwa ajili ya kuanza ujenzi na walipatiwa stakabadhi za chama hicho.
Alisema, fedha nyingine kiasi cha sh 950,000 walizilipa kupitia mfanyakazi wa ofisi ya CCM Wilaya ya Moshi aliyekuwa akichukua kidogo ambapo walimsainisha vocha maalum, aliyedai kutumwa na ofisi ili zitumike kugharamia safari za kufuatilia michoro makao makuu ya chama hicho.
Mwenyekiti wa CCM mkoani Kilimanjaro alipoulizwa kuhusu suala hilo, alisema kuwa ni vema wafanyabiashara hao waende ofisini kwa mazungumzo na kuonyesha risiti walizofanya malipo hayo kwa kuwa Mchome anayedaiwa kulipwa fedha hizo alishafariki.
Kwa upande wake, Mwenyekiti wa CCM Wilaya ya Moshi, Godfrey Mwangamilo, alisema atakutana na viongozi wenzake ili kulipatia ufumbuzi suala hilo, huku akibainisha anachojua kuwa karibuni eneo hilo litagawanywa kwa wafanyabiashara na kipaumbele kitatolewa kwa waliokuwapo kabla eneo hilo halijaungua mwaka 2000.
Eneo hilo kuzunguka ofisi za wazee wa CCM mjini Moshi lilikodishwa kwa wafanyabiashara waliojenga vibanda vya mbao kwa ajili ya shughuli zao kabla ya kuteketea kwa moto mwaka 2000.