UNYANYASWAJI wa wananchi na watendaji wa idara mbalimbali, hasa za serikali nchini, umekuwa kero miongoni mwa jamii kutokana na wengi wao kuilalamikia hali hiyo.
Polisi ni moja ya idara nyeti zinazolalamikiwa na wananchi kwa kiasi kikubwa kutokana na askari wake kudaiwa kutotenda haki kwa wana jamii ambao hulalamikia masuala mbalimbali.
Ikiwa mwananchi atapeleka malalamiko yake kwao juu ya kitu ama mtu fulani kama hawatapindisha ukweli, basi watamzungusha mpaka atakata tamaa.
Si siri, tumeshuhudia wananchi mbalimbali wakibambikiwa kesi wazi wazi kabisa wakati makosa hayo hawajayafanya. Yupo mpiga picha mmoja aliwahi kuwapiga picha askari polisi wakati wanakamata kibaka ili aweze kuitumia picha hiyo katika kazi zake lakini cha ajabu alikamatwa na kushambuliwa na askari hao na kama haitoshi walimfungulia kesi ya kukutwa na bangi.
Katika hili haki iko wapi? Kweli mtu ambaye ameshambuliwa na baada ya kufanyiwa kitendo hicho yeye ndiye alitakiwa kuwashitaki askari hao kutokana na kumpiga, lakini kinyume chake walimbambikizia kesi ya kumkuta na bangi ilhali haikuwa kweli.
Hivi karibuni niliwahi kuandika makala katika gazeti hili ikielezea mikakati ya kuliboresha Jeshi la Polisi. Uboreshwaji wa jeshi hilo ulitolewa na Mkuu wa jeshi hilo, Inspekta Jenerali, Said Mwema.
Baada ya makala hiyo kutoka katika gazeti mwananchi mmoja aitwaye Mario Kivamba, mkazi wa Mzinga Kongowe, alinitumia ujumbe mfupi wa maneno akilipongeza jeshi hilo kwa mikakati hiyo lakini alilalamika kuwa pamoja na hayo baadhi ya askari wa jeshi hilo si waadilifu. Alidai kudhulumiwa sehemu ya kiwanja.
Kuonyesha kuwa amekerwa na jambo hilo tuliwasiliana zaidi na kuelezea kwa kina kuhusu suala hilo.
Anasema katika eneo la Mzinga - Kongowe ana eneo la robo ekari ambalo limevamiwa na askari polisi anayemtaja kwa jina la John Maduhu, ambaye wamepakana naye katika eneo hilo kisha kuliuza kwa mtu mwingine.
Askari polisi huyo anafanya kazi katika moja ya vituo vya jijini Dar es Salaam.
“Askari huyu amevamia eneo langu, ameziba njia ya kupita, eneo hilo alilolichukua amekata sehemu na kumuuzia mkazi wa eneo hilo Said Kumatamata, nilipoona hivyo nilikwenda kwa Mwenyekiti wa Serikali ya Mtaa wa Mzinga, Mpanjinji, na kumwomba amwite Kumatamata ili tujadili suala hilo,” anasema Kivamba.
Anasema baada ya Kumatamata kufika katika ofisi za serikali ya mtaa aliulizwa kama ameuziwa eneo, naye alikiri kisha mwenyekiti huyo alimtaka mjumbe wa Serikali ya Mtaa, Richard Manase, kuongozana nasi hadi katika eneo la shamba alikouziwa Kumatamata.
Kwa mujibu wa Kivamba, walipofika katika eneo hilo Kumatamata alionyesha eneo alilouziwa lakini kabla hajamaliza alifika askari polisi huyo akiwa amevalia sare nusu za polisi ambazo ni suruali, viatu na mkanda kisha kumvamia kwa nia ya kumpiga.
Anasema baadaye askari huyo ambaye alikuwa kifua wazi akiwa na mkewe pamoja na mdogo wake, walimvamia mbele ya mjumbe huyo wa serikali ya mtaa kisha kumtukana na kumjeruhi mkono pamoja na mdomo huku wakimtukana.
“Wakati zoezi hilo likiendelea, mjumbe wa serikali ya mtaa aligombelezea ugomvi huo bila mafanikio, baadaye nilijitahidi kujinasua huku na huko, kisha nilifanikiwa kujinasua na kukimbia hadi ofisi za serikali ya mtaa nikiwa na mjumbe na kueleza yaliyotokea,” anasema Kivamba.
Anaongeza kuwa baada ya mwenyekiti wake kumuona alimtaka aende polisi kuchukua fomu namba tatu ya polisi (PF 3) na alipofika katika kituo kidogo cha Kongowe kabla hajahudumiwa ghafla askari Maduhu alifika kituoni hapo akiwa na mkewe na mdogo wake na kumkataza askari polisi wa kituoni hapo kutomwandikia PF 3.
“Yule askari wa pale kituoni aliuliza sababu ya mwenzake kutotaka niandikiwe PF 3, hata hivyo alisema kuwa kitaratibu na sheria za kazi, hawezi kuninyima kibali cha kutibiwa, hata hivyo baadaye alinipa PF 3. Ilikuwa na namba 8/963 na ilitolewa Agosti 18, mwaka jana.
“Kabla sijapewa PF 3, askari yule alipofika hapo kituoni na ndugu yake na mkewe alimweleza askari wa pale kituoni kuwa mimi sistahili kupewa PF 3 kwa kuwa nilimpiga ndugu yake, hivyo kutokana na mimi kupewa PF 3 alimtaka yule askari kumpa na ndugu yake, naye alikubali,” alisema.
Kwa mujibu wa Kivamba, alikwenda kutibiwa katika Hospitali ya Temeke na Agosti 21 alifungua kesi ya shambulio katika Kituo Kidogo cha Polisi Kongowe kisha ikahamishiwa Mbagala. RB ya kesi hiyo ina namba MBG/RB/8288.
“Walimwita kituoni akatoe maelezo naye alikwenda. Baada ya hapo nikawa naambiwa niende kesho hadi ikatimia miezi mitatu bila kupata haki yangu halali wakati nilishambuliwa,” anasema.
Anasema baada ya kuona anazungushwa bila mafanikio alikwenda kwa Mkuu wa Polisi wa Wilaya (OCD) wa Mbagala aitwaye Mfundo na kumweleza suala hilo.
“Nilimweleza malalamiko yangu akasema ushahidi hautoshi, nilishangazwa na jambo hilo wakati nilipigwa mbele ya serikali ya mtaa, hata hivyo alinieleza kuwa atalipeleka jambo hilo kwa wakubwa zake, baadaye nilipokwenda tena alinieleza kuwa faili langu lipo kwa Kamanda wa Polisi (RPC) wa Mkoa wa Temeke, Emmanuel Kandihabi.
“Nilijiuliza jambo hilo lina ukubwa gani hadi likashindwa kuamuliwa na Mkuu wa Kituo(OCS) au Mkuu wa Upelelezi wa Wilaya (OC CID) hadi liamuliwe na OCD?” anasema.
Anasema Novemba 18 alikwenda ofisini kwa RPC na alikuta faili lake likiwa huko tangu siku mbili zilizopita, alibainishiwa kuwa aende tena baada ya Januari 10 mwaka huu na alipokwenda alionana na RPC na alimweleza kuwa taarifa kutoka Kituo cha Mbagala zinaonyesha kuwa hakuna ushahidi.
“Nilipoambiwa hivyo nilimweleza kuwa hayo na mengine ndiyo yaliyonifanya niende kwake kuonana naye, alinitaka niende tena Machi 10 mwaka huu na nilipokwenda sikumkuta kwa kuwa alikuwa likizo, nilionana na msaidizi wake ambaye alinieleza kuwa faili langu limerudishwa Mbagala.
Sikuchoka, nilirudi Mbagala, nilipofika niliambiwa nionane na OC CID ambaye alinieleza kuwa faili hilo halikufika ofisini kwake. Siku nyingine nilikutana na OCD kituoni hapo, naye aliniambia kuwa faili langu lipo kwa OC CID, nilipokwenda aliniambia kuwa taarifa zilizoandikwa na RPC katika faili hilo ni kuwa ushahidi hautoshi, hivyo jalada lifungwe.
Badala yake RPC aliamua kuwa nishauriwe niende kufungua kesi ya masuala ya ardhi katika Mahakama ya Ardhi, nilijiuliza kuwa pamoja na kudai ardhi yangu, jingine lililonipeleka polisi ni juu ya kupigwa na askari polisi huyo lakini wananiambia ushahidi hautoshelezi, sasa wanataka niende kuwachota wapi?
“Nimepigwa mbele ya viongozi wa serikali ya mtaa na wao ni sehemu ya mashahidi wangu, nilichojiuliza ni sababu ya watu hao kunizungusha kwa miezi saba bila uamuzi, si siri, kwa hili wanalindana,” alisema Kivamba.
Anasema ingekuwa ni kupigwa tu alikofanyiwa angeachana na suala hilo lakini ameingiliwa na kuchukuliwa eneo lake, suala ambalo hawezi kuliacha lipotee. Anasema huo ni unyanyasaji.
“Nilipokuwa nakwenda polisi mara kwa mara nilijifunza mengi, niliona wenzangu wa kawaida ambao walishitakiana na wenzao kuhudumiwa na matatizo yao kumalizika lakini mimi kwa kuwa nilitendewa sivyo na askari niliachwa,” anasema Kivamba.
Analiomba Jeshi la Polisi kumsaidia ili kulimaliza jambo hilo, kwani cha muhimu anachohitaji ni kutendewa haki.
“Naomba IGP Mwema na viongozi wengine wanisaidie ili niweze kupata haki yangu, nimepigwa mbele ya viongozi wa serikali ya mtaa lakini suala hili limefumbiwa macho, je, ningekuwa peke yangu ingekuwaje?” anahoji.
Nasikitika kuona viongozi wa Jeshi la Polisi wanavyomtetea mtu mwenye makosa ya wazi, wanafanya hivyo kwa ajili ya mtu mmoja, nawashauri wajaribu kupima mambo ili kuleta ufanisi katika kazi, natetea haki yangu,” anasema Kavaramba.
Mwandishi wa makala hii anapatikana kwa simu namba: 0754 886 749 au barua pepe: helenpendo@yahoo.com