CHAMA cha Wananchi (CUF), kimeeleza kushtushwa, kusikitishwa na kukatishwa tamaa na tamko la Halmashauri Kuu ya Taifa (NEC) ya Chama Cha Mapinduzi la kukataa mapendekezo ya Kamati ya muafaka ya vyama hivyo viwili.
Mwelekeo huo wa CUF umebainishwa katika tamko rasmi la kwanza la chama hicho lililosomwa jijini Dar es Salaam jana mbele ya waandishi wa habari na Katibu Mkuu wa chama hicho kikuu cha upinzani visiwani, Seif Sharif Hamad.
Katika
tamko hilo, CUF imeuelezea uamuzi huo wa CCM kuwa ni usanii wa kisiasa na ambao chama hicho cha upinzani hakitakuwa tayari kushirikiana nao.
Akisoma tamko hilo, Maalim Seif alisema uamuzi uliofikiwa na CCM huko Butiama mbali ya kwenda kinyume na ahadi nyingi za matumaini zilizopata kutolewa na Rais Jakaya Kikwete siku zilizopita, zinaonyesha dhahiri dhamira ya chama hicho kurefusha muda wa mazungumzo ya kutafuta suluhu ya mpasuko kati yao hadi mwaka 2010 au kuyakataa mapendekezo yaliyotolewa.
“CCM imeamua kufanya usanii wa kisiasa kwa kutumia lugha ya mzunguko, ya ubabaishaji na ya upotoshaji, kwa lengo la kuendelea kurefusha muda hadi mwaka 2010 au kuyakataa makubaliano ambayo wajumbe wake wameshiriki kuyaandaa katika miezi 14 ya mazungumzo kati ya vyama vyetu viwili.
“Chama cha Wananchi (CUF), hakiko tayari kushirikiana na CCM kuwafanyia Watanzania usanii wa kisiasa. Huu si utaratibu wa CUF katika uendeshaji wa siasa; siasa si propaganda zilizopitwa na wakati, bali ni utumishi wa dhati na uliotukuka kwa umma, uliowaamini viongozi wake, kwa msingi huo CUF haitakubali kurejea katika mazungumzo kwa utaratibu wanaoutaka CCM,” alisema Maalim Seif wakati akisoma tamko hilo.
CUF katika tamko lake hilo iliitaka CCM kurejea nyuma na kuheshimu makubaliano waliyofikia katika mazungumzo yao, na kikahimiza haja ya utekelezaji wake kuanza mara moja.
Maalim Seif katika tamko hilo aliuelezea uamuzi wa CCM wa kutamka kwamba suala la muafaka linarejeshwa kwa wananchi kwa sababu ya kupigiwa kura ya maoni, unaonyesha mzaha katika kuendeleza amani ya nchi.
Alisema hoja hiyo ya wananchi kuamua hatima ya mpasuko wa kisiasa Zanzibar kwa kutumia kura ya maoni, haikuwa sehemu ya mambo waliyokubaliana katika kikao cha kamati ya pamoja cha mazungumzo yao yaliyochukua muda wa miezi 14.
Alieleza kushangazwa na madai kwamba hoja hiyo ya kutaka kura ya maoni iamue hatima ya suala la Zanzibar ilitolewa na kamati ya mazungumzo ya pamoja na si Halmashauri Kuu ya CCM, hatua aliyoielezea kuwa ni njama yenye ajenda moja tu aliyoielezea kuwa na nia ya ‘kuipiku CUF katika ubunifu wa kujenga’.
“Kitendo cha kamati ya CCM kuwasilisha kitu kipya nje ya makubaliano yaliyofikiwa ni upotoshaji mkubwa wenye lengo la kulifanyia usanii wa kisiasa suala kubwa kama hili linalogusa masilahi ya taifa na watu wake moja kwa moja”, alisema Maalim.
CUF katika tamko lake hilo ilisema pendekezo zima la kutaka kura ya maoni ifanyike limezongwa na vikwazo vingi vikiwamo kujua ni chombo gani kitakachoisimamia kura hiyo na orodha itakayotumika katika kuendesha zoezi hilo.
Chama hicho kilitoa dukuduku hilo kutokana na kuwapo kwa ukweli kwamba, hadi hivi sasa kumekuwa na mabishano kati ya vyama hivyo viwili kuhusu Tume ya Uchaguzi Zanzibar (ZEC) na Daftari la Kudumu la Wapigakura lililopo sasa.
“Hoja nyingine ni kwamba kura ya maoni hiyo itaendeshwa na chombo kipi na kwa utaratibu upi, hasa ikitiliwa maanani tayari CCM na CUF wamekubaliana kuwa, Tume ya Uchaguzi ya Zanzibar (ZEC) na Daftari la Kudumu la Wapiga kura vina matatizo ya msingi ambayo yanahitaji kurekebishwa?” inasema CUF katika tamko lake hilo.
Kutokana na hali hiyo, CUF ilisema maamuzi hayo ya NEC yamesababisha wao wavunjwe moyo na kukatishwa tamaa mno na Rais Jakaya Kikwete ambaye aliahidi kuupatia suluhisho la kudumu mgogoro wa kisiasa visiwani Zanzibar.
“CUF imevunjwa moyo sana na Mheshimiwa Jakaya Kikwete akiwa kama Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na Mwenyekiti wa CCM, imani tuliyokuwa nayo kwake kama kiongozi wa wananchi na ambayo tulibaki nayo hadi CCM inaelekea katika kikao cha Halmashauri Kuu ya Taifa, imetetereka sana.
“Kitendo cha Halmashauri Kuu ya Taifa ya CCM chini ya uenyekiti wake kukataa kupitisha makubaliano yaliyofikiwa na kamati ya mazungumzo ya CCM na CUF na badala yake kuja na hoja mpya za ajabu ajabu zenye lengo la “kuipiku CUF”, kisiasa kinamwonyesha Rais kikwete ama hakuwa mkweli na mwaminifu tokea mwanzo na kwamba alikuwa akifanya usanii wa kisiasa wakati alipotangaza kuwa anasononeshwa sana na mpasuko wa kisiasa Zanzibar au ni kiongozi dhaifu asiye na udhibiti wa chama anachokiongoza. Yote mawili hayampi sifa ya kiongozi ambaye nchi inamhitaji inapopita katika vipindi vigumu,” alisema Maalim Seif.
Katibu mkuu huyo aliendelea kusema, CUF imeshangazwa na kushindwa huko kwa Kikwete ambaye ndiye huyo huyo anayetajwa kuwa alifanikisha kufikiwa kwa suluhu ya kisiasa katika nchi jirani ya Kenya, kati ya vyama vya ODM na PNU.
“Inasikitisha zaidi kwa Rais Kikwete kuwatangazia Watanzania na ulimwengu kuwa, amefanikiwa kuwakutanisha Rais Mwai Kibaki na Mheshimiwa Raila Odinga wa Kenya na kufanikisha kufikiwa kwa makubaliano kati ya ODM na PNU nchini humo, lakini ameshindwa kulifanikisha hilo nchini mwake ndani ya chama anachokiongoza mwenyewe kati ya CCM na CUF,” alisema Maalim Seif.
Kutokana na hilo, CUF imetoa wito kwa jumuiya ya kimataifa kuingilia kati mgogoro huo kabla mambo hayajaharibika kama ilivyotokea katika nchi nyingine za Afrika.
Wakati huo huo wanasiasa na wasomi mbalimbali walioulizwa maoni yao juu ya mvutano wa CCM na CUF, wameunga mkono msimamo wa CUF, na kuwatahadharisha viongozi wa serikali na CCM kuwa wanachezea amani na utulivu wa taifa.
Akizungumza kwa njia ya simu, Mhadhiri Mwandamizi wa Sayansi ya Siasa katika Chuo Kikuu cha Dar es Salaam, Profesa Mwesiga Baregu, alisema uamuzi wa CCM wa kuingiza jambo jipya katika suala la muafaka kinyume na makubaliano kati yao na CUF, kuwa ni ufisadi wa kisiasa na kuonya kuwa hatua hiyo ni ya hatari kwa amani ya taifa.
“Huu ni ufisadi wa kisiasa. Hatua hii si nzuri kwa amani ya taifa letu, kwani ni kinyume na matumaini ya wananchi wa Zanzibar na Tanzania kwa ujumla.
Hali hii itawafanya wananchi wapoteze imani kwa viongozi wao wa serikali na kuwalazimisha kujichukulia sheria mkononi. Suala hili likiachwa bila kupatiwa ufumbuzi linaweza kuifikisha nchi yetu ilipokuwa imefika Kenya”, alionya Profesa Baregu.
Naye Mbunge wa Kigoma Kaskazini, Zitto Kabwe, aliuelezea uamuzi huo wa CCM kuwa ni kielelezo cha wazi cha kupwaya kiuongozi kwa Rais Kikwete na chama hicho tawala.
“Uamuzi wa CCM kuhusu muafaka ni hatari kwa taifa na ni ishara ya kufilisika kiuongozi. CCM imejenga msingi mbaya. Ni ishara kuwa Rais Kikwete ameshindwa kukidhibiti chama chake. Taifa linaelekea pabaya. Tunahitaji uongozi,” alisema Zitto.