WASHIRIKI wa kongamano lililoandaliwa na shirika lisilokuwa la kiserikali la Mbeya Women Poverty Eradication Association (MWEPEA), lililofanyika wiki hii mkoani hapa, wamependekeza kuwa wanaume wanaowapa mimba wanafunzi wa shule za msingi na sekondari wanastahili kuvyofolewa korodani zao.
Mapendekezo hayo pia yanaitaka serikali kuhakikisha kuwa kunakuwa na adhabu kali kwa wale wote wanaohusika na vitendo vya kuwarubuni wanafunzi na kufanya nao mapenzi na kisha kuwapa ujauzito.
Kongamano hilo liloshirikisha vikundi vya jamii zaidi ya 10 ambavyo washiriki wake kwa pamoja walikubaliana kuitaka serikali kutoa adhabu kali kwa wanaume wenye uchu na matamanio mabaya, yanayosababisha idadi kubwa ya wanafunzi wasichana kushindwa kuendelea na masomo yao kwa sababu ya kupata ujauzito.
“Tunashauri wanaume wanaowapa mimba wanafunzi waondolewe korodani au wafungwe kizazi ili liwe fundisho kwa wengine wenye tabia hizo…kama adhabu ya kifo bado ipo na inadaiwa kukiuka haki za binadamu, tatizo ni nini kwa wanaume kama hawa kuondolewa nguvu za kiume,” alisema mmoja wa washiriki wa kongamano hilo.
Washiriki wa kongamano hilo pia walieleza wasiwasi wao kuhusu Sheria ya Ndoa ya mwaka 1971 na Sheria ya Elimu ya mwaka 2002 kuwa zinakinzana na kuwapa ushindi wanaozikiuka.
Taarifa za wanafunzi waliopata mimba wakiwa shuleni mkoani hapa, zinaonyesha kuwa kuna wanafunzi 549 waliopewa mimba na kukatishwa masomo katika kipindi cha mwaka 2006 na 2007.
Akizungumza katika kongamano hilo, Mkurugenzi Mkazi wa Shirika la Kijerumani la Fredrich Ebert Stiftung, Peter Haussler, alisema ili kukabiliana na tatizo la mimba kwa wanafunzi, Mwepea haipaswi kuishia hapo bali vikundi vya kisheria na uelimishaji rika vinapaswa kwenda hadi ngazi za vijiji kutoa elimu zaidi.