“KWANI wewe unajua ni nani anayeishi Ikulu yetu ya Dar es Salaam?”
“Ndiyo najua, si ni Kikwete!”
“Hapana, sio Kikwete ni Waswahili wa Bagamoyo.”
“Kwani Rais Kikwete anaishi wapi, sio Ikulu?”
“Wewe husikilizi redio, leo Kikwete yuko Marekani kwa siku nane, mara yuko China, siku inayofuata yuko Misri, Afrika Kusini n. k. Unafikiri kwa mizunguko hiyo utaniambia kuwa anaishi Ikulu au huwa anapita tu? Miye ninavyojua wanaoishi Ikulu ni Waswahili wa Bagamoyo walio karibu na Kikwete na yule mwandishi wake.”
Huo ni mjadala nilioukuta kwenye stendi ya mabasi ya Magu mjini wilayani Magu juzi jioni, ukijumuisha kundi la vijana wapiga debe ambao wanategemea kituo hicho kujipatia riziki yao ya kila siku.
Ingawa sikufanikiwa kujua chanzo cha mjadala huo, lakini ni mjadala uliovuta hisia za watu wengi waliokuwepo eneo hilo, baadhi yao wakisubiri usafiri, wachuuzi wa bidhaa ndogondogo na wengine ambao walikuwa wakipita tu, ili mradi kulikuwa na kundi kubwa la wananchi wakibishana kujua ni nani hasa anayeishi kwenye Ikulu yetu ya Magogoni Dar es Salaam.
Kwa vile nilikuta mjadala umeshika kasi, niliamua kuwa msikilizaji mwenye nidhamu, ili nijue hatma ya ubishi huo ambao baadhi ya watu walidai kuwa hauna maana, huku wengine wakiuponda kuwa chanzo chake ni kukosekana kwa kazi ya kufanya kwa waliokuwa wakibishana na baadhi ya Watanzania waliokusanyika hapo wakidai kuwa kuna ukweli katika hoja hizo.
Jambo la msingi nililojifunza kutokana na mjadala huo ni kuwa watu wazima wenye akili timamu hawawezi kujadili kitu kisicho na maana hata kidogo. Hata kama suala lenyewe si la thamani kwa mitazamo ya baadhi ya wasilikizaji, lakini hoja yoyote inayoibuliwa na kuvuta hisia za watu wengi, lazima itakuwa na maana.
Sote tunajua kuwa Ikulu ni makao ya rais na kwa Tanzania, Ikulu ni makao ya Rais Jakaya Kikwete kama ilivyokuwa makao ya Julius Nyarere, Ali Hassan Mwinyi na baadaye Benjamin Mkapa. Lakini katika vipindi vitatu vilivyotangulia, hakuna mtu aliyeibuka na kuuliza swali kama hilo.
Kumekuwepo na kelele miongoni mwa Watanzania nchi nzima kuhusu umuhimu wa ziara ndefu zinazotekelezwa na Rais Kikwete, kwenye nchi mbalimbali za nje kila mara na umuhimu wake kwa taifa hili maskini linaojitutumua kujiondoa kwenye lindi la ufukara.
Wananchi wanahoji, si kwasababu hawampendi rais wao, lakini kwa sababu wanafikiri kuwa rasilimali nyingi za taifa zinateketea kupitia njia hiyo ambayo wanadai kuwa haina tija kwa taifa. Ukianzia gharama za kulipa posho na fedha za kujikimu kwa rundo la watu anaofuatana nao, gharama za ndege yake ya kifahari na kusimama kwa shughuli kwenye ofisi za hao wanaofuatana na rais.
Kwenda mbali zaidi, Watanzania wamehoji sababu za ziara za Kikwete mikoani kuchukua muda mrefu kiasi cha kumkosesha wasaa wa kutoa huduma zake kwa wananchi akiwa ofisini kwake Ikulu. Mbaya zaidi, ziara hizo za mikaoni huwahusisha pia mawaziri na watendaji lukuki ambao kwa kipindi chote hicho ofisi zao hazifanyi kazi kwa ufanisi.
“Hebu kumbuka enzi za Mwalimu Nyerere, alikuwa akiishi Ikulu na wananchi waliokuwa na shida naye walikuwa wakisafiri na kwenda Dar kuzungumza naye au wengine walikuwa wakimsubiri akienda Butiama kwenye mapumziko, lakini huyu utampata wapi kila leo yuko angani?” alidai mmoja wa wachangiaji hao.
Wasemaji mbalimbali wa serikali wamekuwa ‘wakizifagilia’ ziara hizi za rais nchi za nje kwa madai kuwa zina faida kubwa kwa taifa zaidi ya hasara na hivyo kuwataka wananchi wasiendelee kupiga kelele na kuwa na wasiwasi na kazi anazofanya Kikwete nchi za nje.
Waandishi wa habari wa vyombo mbalimbali vya habari ndio walikuwa wa kwanza kulalamikia wingi wa ziara za Rais Kikwete na ujumbe ‘mzito’ ambao amekuwa akiandamana nao kila leo na kuainisha gharama zinzotumika.
Kelele zao zimefikia mahali zikazimwa na kile kinachoelezwa kuwa ‘ofa’ kusafiri na kiongozi huyo wa taifa na mawaziri wa serikali yake hivyo wakanyamaza.
Leo mvutano unaoendelea miongoni mwa waandishi waandamizi wa vyombo vikongwe vya habari nchini kuhusu baadhi yao kuwapaka viongozi wa taifa matope na wengine wakidaiwa kuwasafisha viongozi hao ni matokeo ya ofa na rushwa zinazotolewa kwa waandishi, ili kuwanyamazisha kama walivyonyamazishwa kwenye hoja ya safari za Kikwete.
Tukubali kuwa baadhi ya waandishi wamenyamazishwa kufuatilia na kuibua hoja nzito kuhusiana na matumizi mabaya ya rasilimali za taifa katika ziara hizi zinazoitwa za kifahari na Watanzania. Lakini hoja sasa imetoka kwenye vyombo vya habari na kuingia mitaani kwa wapiga debe na watu wengine wa daraja la chini.
Wananchi wenyewe ndiyo sasa wanahoji kiini hasa cha ziara hizi ndefu za Rais Kikwete nchi za nje na tija yake katika kuboresha hali mbaya ya kiuchumi iliyopo miongoni mwa wananchi.
Licha ya viongozi kushangilia umuhimu wa ziara hizo lakini wao bado hawakubali na kuendelea kuhoji kiasi cha kufikia kuhoji ni muda gani anaoutumia Kikwete kukaa katika ofisi yake Ikulu na kutatua matatizo ya wananchi.
Kwa jinsi mfumo wa utawala ulivyojengwa katika nchi yetu, baadhi ya watu wanaweza kuhoji sababu za wananchi kutoka vijijini kwenda Ikulu kuonana na Rais wakati watendaji wa vijiji, kata, makatibu tarafa, wakuu wa wilaya, mikoa na hata mawaziri wapo kutatua matatizo yao; kwanini lazima uende kwa rais Ikulu?
Licha ya viongozi hao, ambao wamewekwa katika nafasi hizo na serikali na wengine kuteuliwa na rais mwenyewe kuwepo, lakini kuna matatizo mengine ambayo ni lazima ulazimike kusafiri mwendo mrefu hadi Dar es Salaam kuonana na kikwete baada ya njia nyingine hizi ‘kushindikana’ au kutokana na urasimu usikokuwa na sababu za msingi au kutokana na rushwa.
Nasema hivyo kutokana na hali halisi inayotokea na kuwasibu wananchi wanaoishi vijiji ambao viongozi hao huwaona kama washamba na kero kwao kutokana na uduni wa maisha wanayoishi. Hivyo kuamua kuwazungusha bila ya sababu za msingi.
Napenda kutoa mfano wa tatizo moja la mgogoro wa ardhi katika eneo la kijiji cha Yitwimila ‘A’ wilayani Magu, ambao serikali ya kijiji walitoa kwa kampuni ya ujenzi wa barabara ya lami ya Mwanza-Musoma na baada ya kampuni hiyo kumaliza kazi zake iliuza baadhi ya mitambo yake kwa mfanyabiashara mmoja mwenye asili ya kiasia na mfanyabiashara huyo kupitia njia zake, anadaiwa kujimilikisha eneo hilo bila ya ridhaa ya kijiji.
Mgogoro huu umekuwa chanzo cha kura kwa wabunge wanaoomba nafasi hiyo kwenye jimbo hilo, lakini kila mara hakuna anayefanikiwa kulitatua na kurejesha ardhi hiyo kwa serikali ya kijiji, ingawaje kila mara wanadai kuwa mmiliki huyo hana hati halali.
Katika mazingira ya ufisadi wa namna hii, kwenye mfumo wa utendaji wa serikali kisheria, njia pekee inayobakia kuwa msaada kwa wananchi ni kukimbilia kwa Rais wao ambaye kimsingi tunajua kuwa hana nafasi ya kuomba rushwa kutoka kwa wananchi wake.
Wazee wastaafu wa iliyokuwa Jumuiya ya Afrika Mashariki, walipoona kuwa hakuna idara ya serikali inayojali matatizo yao, waliamua kuhamia kwenye uzio wa Ikulu wakifikiri kuwa Kikwete atasikia kilio chao na kushughulikia.
Sina uhakika kama madai ya wazee hao hayana msingi na kuwa ni ya uongo, kwa sababu hakuna binadamu anayeweza kukubali kujitesa kwa miaka yote hiyo akifuatilia madai ya uongo, hayupo binadamu wa namna hiyo. Hivyo madai yao ni ya msingi na yanahitaji uangalizi wa rais, lakini…!
Kikwete kama kiongozi mkuu wa taifa analazimika kupata muda wa kutosha kufuatilia kwa karibu hali ya utendaji wa shughuli za maendeleo ya jamii katika utekelezaji wa miradi mbalimbali inayotekelezwa na serikali anayoongoza badala ya kupatiwa taarifa kila anaporejea kutoka safari zake ndefu hizo nje ya nchi.
Ninaungana na wapiga debe wale katika hoja ya kutokuwepo ulazima kwa rais Kufanya ziara ya siku saba, nane au kumi mfululizo kwenye mkoa mmoja. Kuna ulazima gani wa kuwa na ziara mkoani kwa zaidi ya wiki mfulululizo.
Kwa njia hii utakuwa unapata fursa ya kubaini makosa au pale unapodanganywa na wakuu wa mikoa husika?
Ni kwa nini asifanye ziara kwa siku tatu, nne hivi halafu arejee ofisini na kupata muda wa kutafakari aliyoyaona na kulinganisha na taarifa alizopewa, ili atakaporejea kumalizia aweze kujua kinachoendelea na wakati huo apate muda wa kusikiliza matatizo ya Watanzania?
Wananchi wanadai kuwa Kikwete amekuwa mzazi ambaye kila leo ‘mguu na njia,’ hali ambayo imetoa mwanya kwa wasaidizi wake kujifanyia mambo yao kama wanavyotaka.
Wanaotumia fursa hiyo kuingia mikataba feki na wawekezaji, wapo wanaotumia fursa hiyo kujijengea umaarufu wa kisiasa pia wapo na wale wanaotumia fursa ya safari nyingi za rais kujijengea ‘umiungu watu’ nao pia wapo tele kila kona.
Hali hii ni hatari. Washauri wa rais lazima waangalie upya na kuchukua hatua za kumshauri vyema kiongozi wetu, ili apate muda muafaka wa kufuatilia matatizo yanayolikabili taifa na kuibua mikakati ambayo ataisimamia mwenyewe kuitekeleza kwa manufaa ya wananchi.
Watendaji wa serikali wanapodai kuwa safari za Kikwete nje ya nchi zina tija kwa wananchi wakati wananchi wenyewe hawaoni matokeo ya safari hizo ni vema serikali ikubaliane na wananchi kwa sababu wao ndio walengwa na wanakerwa na safari hizo zinazomwondolea rais nafasi ya kutoa huduma kwao, kukaa nao na kucheza bao pamoja kwani yeye ni kiongozi wao.
Wananchi wanapopiga kelele kuhusu kukerwa na jambo fulani, serikali iliyo makini ni lazima isikilize, ili ijiepusha na madhara ya wananchi hao kukata tamaa kwani wanafuatilia hatua zinazochukuliwa na serikali yao kuhusiana na kashfa nyingi zinazozunguka utawala wa awamu ya nne na hawaoni kinachoendelea.
Ndiyo maana wanaamua kuchukua muda wao muhimu kujadiliana kuwa ni nani hasa anayeishi Ikulu?
0786 555 066
0713 091 109
osoropjn@yahoo.co.uk