HABARI MPYA KITAIFA DAR MIKOANI TAHARIRI MAKALA MICHEZO
jumatatu, 22 septemba 2008
Pekua Tovuti
Gazeti la Jana
Matangazo
Bei zetu
Wasiliana nasi
Tuma habari


Yanga mwendo mdundo 2008/9


na Ruhazi Ruhazi


IKIMCHEZESHA kipa wake Mzungu kwa mara ya kwanza, Obren Circovic, timu ya soka ya Yanga, jana ilivuna ushindi mnono wa mabao 5-0 dhidi ya Villa Squad ya Kinondoni, Dar es Salaam.

Shujaa wa mechi hiyo, alikuwa mchezaji wa kimataifa wa Kenya, Boniface Ambani, aliyekandamiza mabao matatu katika nyavu za Villa Squad, huku mengine yakifungwa na Mkenya mwenzake Bernard Mwalala na Shamte Ally.

Uishindi huo wa tano mfululizo unaifanya timu hiyo ya Jangwani kuwa na pointi 15 ikiongoza msimamo wa ligi hiyo inayodhaminiwa na Kampuni ya simu za mkononi ya Vodacom.

Kwa kuwa ligi hiyo inashirikisha timu 12 tu, bila shaka matokeo hayo yanatoa mwanga kwa Yanga kutetea taji hilo, ikiwa ni mara ya 20 tangu kuanza kwa ligi hiyo mwaka 1965.

Yanga ilianza kuhesabu bao la kwanza katika dakika ya 15 lililofungwa na Bernard Mwalala baada ya kumegewa pande na Ambani aliyempokonya mpira beki wa Villa.

Bao pili la Yanga lilifungwa na Ambani ambaye pia alipiga mabao ya nne na tano wakati bao la tatu, lilifungwa na Shamte Ally katika dakika ya 23.

Shamte alifunga bao hilo kwa kuunganisha mpira wa krosi iliyopigwa na Athuman Idd Chuji aliyeonyesha uwezo mkubwa katika mchezo huo.

Katika mchezo huo, Amani alifunga bao la pili katika dakika ya 20 baada ya kuunganisha krosi ya Shamte aliyegongeana vema na Mwalala.

Bao la nne alifunga katika dakika ya 56 wakati bao la tano alipega katika dakika ya 70 kabla ya kutoka nje kumpisha Jerryson Tegete.

Baada ya mchezo huo, Ambani alikabidhiwa mpira kwa ufanisi wake wa kupiga mabao matatu katika mchezo mmoja na Ofisa Tawala wa Shirikisho la Soka Tanzania, Iddy Mshangama.

Kocha Mkuu wa Yanga, Dusan Kondic, alifurahia mchezo huo, akisema kwamba timu yake ilicheza vile alivyoagiza kwa asilimia kubwa.

Terry Mholeli anayeinoa Villa kwa sasa, alisema: “Nakubali matokeo, tutajipanmga tusipoteza mechi zijazo. Yanga ni timu nzuri iliyotuzidi kimchezo.”

Villa ilikuwa ipate bao la kufutia machozi baada ya beki wa Yanga, Wisdom Ndlovu, kuunawa mpira ndani ya eneo la hatari.

Mwamuzi, Oden Mbaga alitoa penalti ambayo hata hivyo, kipa huyo Mzungu kutoka Serbia alipangua penalti hiyo katika dakika ya 77 iliyopigwa na Godfrey Taifa.

Kadhalika, kipa huyo mrefu, alitoa moja ya hatari golini baada ya kupangua shuti jingine katika dakika ya 80 hivyo mashabiki kumshangilia.

Yanga iliwakilishwa na Obren Circoviv, Fred Mbuna, Amir Maftah, Wisdom Ndlovu, George Owino, Godfrey Bonny, Shamte Ally, Athumani Idd ‘Chuji’/Vicent Barnabas, Boniface Ambani/Jerry Tegete, Bernard Mwalala/Kigi Makasi na Mrisho Ngassa.

Villa Squad: Peter Manyika, Godfrey Taita, Edd Zaharani/Andrew Carlos, Jamal Said, Saleh Hamisi, Emmanuel Memba, Francis Busungu/Chesido Mathew, Laurent Mugia, Iddy Moshi ‘Mnyamwezi’, Stamili Mbonde/Hassan Said na Lameck Dayton.


juu

Warning: mysql_connect() [function.mysql-connect]: Can't connect to local MySQL server through socket '/var/run/mysqld/mysqld.sock' (2) in /hermes/bosweb/web098/b983/glo.freemanm2/include/comment.php on line 9
I cannot connect to the database because: Can't connect to local MySQL server through socket '/var/run/mysqld/mysqld.sock' (2)