HABARI MPYA KITAIFA DAR MIKOANI TAHARIRI MAKALA MICHEZO
jumatatu, 22 septemba 2008
Pekua Tovuti
Gazeti la Jana
Matangazo
Bei zetu
Wasiliana nasi
Tuma habari


Mambo yanayopaswa kufanywa na Simba SC
 
Mwina Kaduguda


ALAMA za nyakati ambazo kwa bahati mbaya wengi wameshindwa kuzisoma, zinanionyesha kuwa huu ni wakati muafaka kukushauri au kukumbusha mambo muhimu yanayohusu maendeleo ya klabu ya Simba.

Baada ya hatua iliyochukuliwa na uongozi wa Simba S.C kwa shinikizo lako, ya kunisimamisha pasipo kufuata taratibu, niliamua kukaa kimya.

Niliamua hivyo, si kwa sababu ninaogopa au siwezi mapambano, la hasha, bali ni kwa vile sikuona umuhimu wa kulumbana na viongozi ambao waliokurupuka kutoa uamuzi ulijikita katika misngi ya chuki binafsi, fitina na majungu.

Lakini, la msingi zaidi niliwaheshimu wanachama na wapenzi wa Simba kwani malumbano na mgogoro ambao ungeendelea miongoni mwetu, usingesadia lolote katika maendeleo ya Simba bali kuibomoa.

1. Kwanini nimeamua kusema

Nimeamua kusema hivi sasa kwa sababu, imethibitika kwamba, takribani kipindi chote tangu lililotolewa tamko la kusimamishwa kwangu kihuni Me 12, mwaka huu, umekuwa ukitumia muda na nguvu nyingi kuwashawishi baadhi ya wanachama wanifukuze wakati wa mkutano (Septemba 21).

Kwa mujibu wa taarifa za uhakika zilizothibitishwa na viongozi wa Simba, ambao nimezungumza nao kwa nyakati tofauti, wewe umeapa kuhakikisha unaningoa Simba.

Kwa kile unachodai kuwa nimeshindwa kukubaliana na sera yako ya kuweka mbele msalahi binafsi na badala yake nimekuwa ninajifanya mtakatifu kwa kuweka maslahi ya Simba.

Kiongozi mmoja aliniambia “Dalali anasema kuwa ni lazima utengenezewe zengwe ili uondoke kwa sababu unaweza kutibua mipango yake ya kuondoka Simba na gari.”

Katika mazungumzo na kiongozi mwingine wa ngazi za juu wa klabu, alinithibishia kwamba, katika kikao cha Kamati ya Utendaji kilichofanyika Zanzibar, karibu wajumbe wote waliridhia nirejee madarakani, lakini Dalali alikataa na kutishia kujiudhulu endapo ningerudi.

“Inavoonekana Mwenyekiti amenogewa na shughuli za ufuatiliaji na uendeshaji wa kila siku ambazo zinawezesha kupata vijiposho vya kijungu hivyo anaogopa endapo utarejea utamzibia,” alisema .

Aidha, kiongozi mwingine alinieleza kwamba, kinachoniponza ni kweli na misimamo yangu kuhusu masuala muhimu ya maendeleo ya klabu.

2. Ushauri

Kwa upendo mkubwa ninakushauri wewe na viongozi wenzako msipoteze muda na nguvu nyingi kupanga mikakati ya kuhakikisha sirejei Simba, bali tumieni muda na nguvu hizo kushughulikia maendeleo ya klabu.

Aidha, ni vema mkatumia muda na nguvu hizo kushirikisha wadau mbalimbali wa klabu yetu kuweka mikakati mizuri ili timu yetu ifanye vizuri katika Ligi Kuu ya Vodacom inayoendelea hivi sasa.

Endapo busara ingekuwa inaazimwa, basi wewe na viongozi wenzako mngebaini kwamba, hatua ya katibu wetu kukaa kimya ni ustarabu na uungwana, lakini hivi sasa mnahangaika ili kuficha madhambi yenu kwa kuwa hamna sababu ya kimsingi ya kunisimamisha.

“Mwenyekiti kumbuka, kwamba ligi ya msimu huu ni fupi, hivyo viongozi msipokuwa makini baadaye mtatafuta mchawi wakati wakati mambo tayari yamekwisha haribika, kama ambavyo hivi sasa mmeamua kumtoa kafara Katibu Mkuu ili kuficha madhambi na udhaifu wenu .

3. Mambo muhimu ya kufanya

Kitu cha muhimu kinachopaswa kufanywa katika kuinusuru timu yetu kufanya vibaya katika Ligi Kuu ya Vodacom inayoendelea, ni kufanya yafuatayo:

  1. Uongozi wa uangalie upya na umakini wa hali ya juu uhusiano uliopo baina ya uongozi ulichaguliwa na wafadhili.
  2. Uongozi ufanye tathmini ya kina na uchambuzi kwa mapana na marefu kuhusu tofauti kati ya wafadhili au wadhamini ikiwa ni pamoja na umuhimu wao kwa vipindi vyote vya mgawanyo wa kiufundi wa maandalizi ya timu ya soka, kwa mwaka mzima, yaani off-season, preparation period na competition period.
  3. Uongozi upitie upya muundo wa benchi la ufundi la timu yetu, ikiwa ni pamoja na kuangalia undani mahusinao kati ya Kocha Mkuu, Mburgaria Krasmil Smilenov Bezinski na Msaidizi wake Jamhuri Kihwelo ‘Julio’.
  4. Ili tufanikiwe kutumia vema nafasi iliyobaki, ni vema pia uongozi ukaangalia mahusiano baina ya Makocha na wachezaji, makocha na viongozi, makocha na wafadhili .
  5. Uongozi uchukue hatua za haraka kukaa na wachezaji na kuzungumza nao kwa kina juu ya:
  6. Mahusiano kati yao, yaani wachezaji wakongwe na chipukizi.
  7. Muda na uharaka wa upatikanaji wa stahili zao na mahitaji yao muhimu yakiwemo yale ya ubinafsi.
  8. Uongozi ujitathmini wenyewe endapo kuna upendo, ushirikiano na kuaminiana kwa dhati ya moyoni baina ya viongozi.
  9. Wadau mbalimbali wakiwemo viongozi wa zamani, wachezaji wa zamani na wengine washirikishwe katika suala zima la maendeleo ya Simba husasan hili la hivi sasa la kuinusuru timu hata nafasi ya kuwakilisha nchi katika michuano ya kimataifa mwakani.

Kama haya yatapewa umuhimu na kufanyiwa kazi kwa kushirikisha wadau wa Simba basi naamini tutafanikiwa.

4. Chanzo cha matatizo:

Kwa maoni yangu, chanzo cha matatizo mengi yanayotokea ndani ya Simba, yanatokana na ubinafsi uliokithiri, muundo au mfumo uliopo, kukosekana kwa mipango na badala yake klabu kuendeshwa kwa mazoea kama vile chama cha kufa na kuzikana.

Kama utakumbuka vizuri, katika kikao cha kwanza cha kamati ya utendaji kilichofanyika Zanzibar 10/12/2006, baada ya kuingia madarakani Desemba 3, mwaka 2006, nilipendekeza mambo sita (6) ili kujenga msingi wa Simba kuanza kujitegemea katika miaka ya usoni.

Nilipendekeza yafuatayo:

  1. Uongozi uhakikishe Account yetu ya CRDB ina kiasi cha fedha zisizpongua 20,000,000/-, kila wakati ili kuwa na uwezo wa kulipa mishahara, kambi na dhanira ndogondogo za hapa na pale .
  2. Uongozi uweke mikakati kuhakikisha msimu wa 2007-2008, nusu ya wachezaji watakaosajiliwa, wasajiliwe na klabu ya Simba na si wafadhili kama ilivyo hivi sasa.
  3. Benchi la ufundi liboreshwe ili kukidhi malengo ya kujenga timu yenye ushindani wa kimataifa na siyo inayoshiriki tu.
  4. Pamoja na kutafuta wadhamini (sponsors), ni vema uongozi ukabuni na kuanzisha miradi inayoiingizia klabu chochote kuliko kutegemea mapato ya mlango kwa miaka nenda rudi .
  5. Uongozi uweke mikakati ya makusudi kuhakikisha jengo la zamani la klabu linafanyiwa ukarabati ili litumike kibiashara.
    Hali ambayo ingetupunguzia tatizo la mishahara ya wachezaji, wafanyakazi wetu na uendeshaji wa ofisi.
  6. Uongozi upambane kufa au kupona ikiwa na kuwashirikisha wadau wote wa Simba kuanzia wachezaji wa zamani, uongozi wa zamani, viongozi wa Serikali, wanasiasa na makampuni ya ndani na nje ili Simba ipate uwanja wake/kituo cha michezo.

Pamoja na kuwaletea 10,000,000/- za kambi, posho na mishahara ya wachezaji kutoka kwa wafadhili bila kudokoa hata senti tano, jambo ambalo liliwafanya kunipongeze kwenye kikao hicho, nilisikitika nilipoambiwa na wajumbe kuwa katiba ya Simba hainipi nguvu ya kuwa mtendaji mkuu, hivyo niachane na mipango ya muda mfupi na mrefu.

Aidha, nilitukanwa kama mtoto mdogo bila kosa lolote, jambo ambalo lilinifanya nipatwe na butwaa bila kujua nini kilikuwa kinaendelea.

Nilipatwa na wasiwasi zaidi nilipoona Mwenyekiti wangu haniungi mkono, lakini baadaye aligundua kwamba, wenzangu kwa kuwa mlitangulia mapema mjini Zanzibar, tayari mlikwisha panga jinsi ya kunikatisha tamaa kuhusu mapendekezo ya mpango wa maendeleo.

Pamoja na kauli za mara kwa mara za kunikatisha tamaa ndani na nje ya kamati ya utendaji, kama vile “programu zako peleka kwa wasomi wenzako chuo kikuu si Simba; sikukata tamaa.

Hata hivyo, mimi kama binadamu niliyeumbwa na nyongo, baadaye nilikataa na kugundua kuwa miongoni mwa viongozi saba (7) tuliochaguliwa Desemba 3, mwaka 2006 kuingoza Simba nimebaki pekee yangu ninayepigania maslahi ya klabu hali hiyo, ilitokana na jinsi Mwenyekiti ulivyopambana na mimi kuzuia amri yangu ya kumwamuru mhazini apeleke fedha benki baada ya kutoa mgawo wa wachezaji.

Ulipoulizwa na Mkurugenzi wa Fedha wa TFF, Silas Mwakibinga, kuhusu ama atekeleze amri yangu (katibu mkuu) au la, ulinishangaza, kunisikitisha na kunikatisha tamaa kabisa.

Ulisema: “Hela ya Simba huwa haipelekwi benki bali inagawiwa palepale kila mtu anaondoka na chake.

“Simba si Real Madrid wala Manchester United, tumekwisha kueleza mipango yako peleka kwa wasomi wenzako chuo kikuu, ulifoka kwa hasira mbele ya kadamnasi kwenye Hotel ya Oasis, Mjini Morogoro mara baada ya mechi ya Simba na Yanga ambapo tulishinda kwa penalti 8.

5. Utekelezwaji wa mpango wa muda mfupi/mrefu;

Jambo la kwanza, nililolifanya baada ya kuchaguliwa kuwa Katibu Mkuu wa Simba SC, ni kuandika mradi wa muda mfupi na muda mrefu.

Hata hivyo, kwa kuwa kazi ya kutekeleza mpango huo ilikuwa inategemea wenzangu wataupokea vipi na watatoa ushirikiano kwa kiasi gani, niliamua kusitisha, lakini niliendelea na utekelezaji wa mawazo ambayo yanatokana na mpango huo.

(i) Uboreshwaji wa benchi la ufundi

  • Tuliamua kuleta kocha, Mbrazil, Nielsen Elias.

(ii) Dhana ya kujitegemea

Tulimpa Elias dola za Marekani 15,000 zaidi ya Tsh 15,000,000 taslimu za Simba SC.

  • Tulilipia pango kwa muda wote atakaofundisha Simba 70,000 x 90 katika Hoteli ya Lamada bila mkopo.
  • Tulinunua gari aina ya CHESSER, namba T 229 AQX kwa ajili ya usafiri wa kocha.
  • Tulimpa Tsh 200,000 kila siku kwa ajíli ya mafuta ya gari na chakula.
  • Tulimnunulia simu NOKIA yenye thamani ya Tsh 500,000/- kwa ajili ya mafuta ya gari na chakula.

Yote hayo tuliyafanya kwa kutumia fedha ya Simba, hakuna mfadhili, mdhamini, mwanachama au mpenzi aliyechagia hata senti tano.

Hata hivyo, Nielsen aliondoka kufuatia mazingira ya Kiswahili na badala yake tulimchukua Twalib Hilal na tukafanikiwa kutwaa ubingwa wa Ligi Ndogo.

(iii) Ukarabati wa jengo la zamani

Baada ya kufanya mazungumzo ya kina na mdau mmoja wa Simba, ambaye pia ni mwanachama, hatimaye tulikutana naye uongozi mzima na alitusaidia kama ifuatavyo:

(i) Alitoa Tsh 80,000,000/- ambazo zilitumika kama ifuatavyo:

  • Kulipia deni lililoachwa na Friends of Simba kwa wachezaji msimu wa 2005-6 la Tsh 30,000,000
  • 40,000,000/- zilitumika kusajili wachezaji kwa msimu wa 2006-07
  • Dola za Marekani 11,000 zilitumika kusajili wachezaji wanne wa kigeni akiemo Said Kokoo, Sadiq Muhimbo, Moses Odhiambo na Ndikumana Hamad.

(ii) Alitoa pia ofa ya zaidi ya 100,000,000/- kukarabati jengo la zamani la Simba ili litumike kibiashara.

(iii) Nilishangaa na kusikitishwa na hatua ya kiongozi mwenzetu kuupora mradi au ofa hiyo kwa tamaa ya 10% na hatimaye kuvuga na kumkatisha tamaa mfadhili.

Nilikerwa zaidi na kitendo hicho baada ya kuona wewe mwenyekiti unashiriki katika kumlinda na kumkingia kifua kiongozi huyo kila tunapoitisha vikao vya kamati ya utendaji ili kumwajibisha.

(iv) Ununuzi wa ardhi kwa ajili ya ujenzi wa uwanja na kituo cha michezo cha Simba.

Kwa bahati nzuri, uongozi iliopita, ulikuwa tayari umefanya kazi nzuri kwa kushirikiana na mchezaji wetu wa zamani, Dan Manembe na wapenzi wengine waliopo wizarani.

Kwa kuwa serikali imekadiria bei ya ardhi hiyo kuwa ni zaidi ya Tsh 100,000,000, fedha ambazo si rahisi Simba kuzipata kwa mkupuo, niliongea na baadhi ya maofisa wa ardhi wakanipa ushauri.

Walishauri tutafute 20,000,000/- ili tulipe kama down payment ili tukabidhiwe ardhi na kiasi kilichobaki tutalipa taratibu kwa makubaliano maalumu.

Nilishauri zifanyike juhudi za kina za kutafuta 20,000,000/- ili zilipwe na hatimaye tukabidhiwe ardhi.

Baada ya kupata hati ya tutafute mwekezaji ndani au nje ya nchi ajenge Simba Sport Club Sports Complex na baada ya kukamilisha ujenzi aiendeshe kwa miaka 12 au 20.

Aidha, nilishauri miongoni mwa vipengere vya mkataba kiwe ni kutoa kiasi cha fedha kila mwezi kwa ajili ya mishahara ya wachezaji na wafanyakazi na pia kiasi fulani kwa kuendesha ofisi.

Baada ya miaka 15 au 20, akabidhi uwanja/kituo kwa Simba Sports Club.

Mwenyekiti, umekuwa ukiwalinda viongozi ambao wamekuwa wakihakikisha mwazo haya au mradi huu hautekelezwi na hata siku moja hujawahi kukemea kauli za kejeli za kukatisha tamaa kama vile:-

  1. Kaduguda utachelewa unatuletea mipango ya miaka 15 wakati sisi tunakaa madarakani miaka mitatu (3) tu.”

  2. Kaduguda wewe hutaki gari!”

“Kaduguda wewe ndiye Katibu Mkuu wa kwanza Simba kuingia bila kumiliki gari, usifikirie mipango ya miaka 15, changamka miaka mitatu si mingi.”

“Sisi tumeingia hapa kwa pesa kama wewe hukutoa kitu tuache sisi turudishe gharama zetu hatukuja Simba kutangaza dini, mbona waliotutangulia hawakuyafanya hayo, kwani hawayaoni?”

6: Kikao cha pamoja kati ya uongozi na Friends of Simba Regency Hotel-Msasani, Mei 11 mwaka 2008.

Kikao hiki kilichofanyika mara baada ya kwisha kwa Ligi Kuu ya Vodacom, ndicho kilichotoa picha halisi ya mahusiano yako mwenyekiti na kundi hilo.

Aidha, kilionyesha ni jinsi gani uongozi wetu umekabidhi madaraka kwa 100% kupitia kwako na sasa uongozi unaendeshwa kwa mfano wa TV na Remote.

Katika kikao hicho, ambacho mimi nilikuwa Katibu kwa maana ya kuandika minutes, kulikuwa na ajenda zifuatazo :-

  1. Tathmini ya Ligi ya Vodacom na michuano ya kimataifa.
  2. Utatuzi wa matatizoyaliyojitokeza msimu uliopita.
  3. Usajili kwa ajili ya msimu wa 2007-08
  4. Kadi za uanachama
    Napenda nikukumbushe mwenyekiti kwamba ajenda zilizozungumzwa na 1 na 2 .

Tulipofika kipengele cha uuzaji wa wachezaji, ndipo hoja zangu zilipokosa majibu kutoka pande zote mbili, yaani uongozi na Friends of Simba.

Kipengele hiki, kilikuwa ni uthibisho tosha kwamba Mwenyekiti yuko bega kwa bega kundi la Friends of Simba si uuzaji wa wachezaji tu bali kwa shughuli zote za kiutendaji bila katibu mkuu kujua.

  1. Kwa binadamu yeyote mwenye akili timamu, hoja nilizozitoa kuhusu kutocheza mechi hata moja kati ya 42 za Ligi ya Vodacom msimu uliopita na hayupo Dar es Salaam, Edwin Mukenya, ni ushahidi tosha kuwa katibu mkuu alikuwa anazungukwa makusudi na mwenyekiti kutokana na tamaa za kibinadamu.
  2. Suala George Owino kucheza raundi ya kwanza ya Ligi Vodacom na kutocheza kabisa hata mechi moja ya raundi ya pili, pia lilikosa jibu toka pande zote mbili na kukawa mwanzo wa kujengwa nongwa dhidi yangu.

Hii ni barua ya Katibu Mkuu wa Simba, Mwina Mohamed Kaduguda ‘Simba wa Yuda’ aliyoandika Septemba 19 kwenda kwa Mwenyekiti wake Hassan Dalali.

Barua hii iliandikwa siku mbili kabla ya mkutano mkuu wa wanachama wa klabu hiyo uliomrejesha madarakani baada ya kusimamishwa na Kamati ya Utendaji tangu Mei 12 mwaka huu.


juu

Warning: mysql_connect() [function.mysql-connect]: Can't connect to local MySQL server through socket '/var/run/mysqld/mysqld.sock' (2) in /hermes/bosweb/web098/b983/glo.freemanm2/include/comment.php on line 9
I cannot connect to the database because: Can't connect to local MySQL server through socket '/var/run/mysqld/mysqld.sock' (2)