HABARI MPYA LA JANA MATANGAZO BEI ZETU WASILIANA NASI TUMA HABARI
alhamis, 26 novemba 2009
Yaliyopita
Pekua Tovuti

Evander kuzichapa Uganda

•  Akwaana na Botha wa 'Sauzi'

na Mwandishi Wetu, KAMPALA, Uganda

 

BINGWA wa zamani wa masumbwi katika uzito wa juu duniani, Evander Holyfield wa Marekani amepanga kwenda Uganda kuzichapa na Francois ‘White Buffalo’ Botha wa Afrika Kusini.

Kwa mujibu wa waratibu wa pambano hilo la kimataifa, wababe hao watazichapa Januari 16, wakiwania mkanda wa dunia wa WBF.

Pambano hilo ambalo litavuta hisia za wengi, litapiganwa siku hiyo katika Uwanja wa Taifa wa Mandela, mjini Kampala, Uganda.

Kwa mujibu wa Jarida la Fight News, pambano hilo litafanyika chini ya uratibu wa kampuni tano ambazo ni Eddie Bazira & Baltic Pro Box Promotions, Real Deal Events LLC, SES Boxing, Fight Production na Risum Boxing.

Mabondia hao tayari wamesaini mkataba wa kuzichapa Januari 16 nchini Uganda, ingawa awali pambano lilikuwa lifanyike mwezi Desemba.

Kampuni ya Baltic Pro Box Promotions yenye maskani yake Sweden, imepanga kuanza kulinadi pambano hilo la kihistoria nchini Uganda na Afrika.

“Ni fahari kubwa kwetu kuwaletea pambano la kihistoria nchini Uganda na Afrika,” alisema Bazira alipozungumza na Jarida la Fight News na kuongeza:

“Holyfield, kama alivyo, ni bondia mahiri duniani kama ilivyo kwa Botha, ambaye ni bondia wa aina yake Afrika. Kwa kila mmoja amepania kushinda, litakuwa pambano lenye mvuto,” alisema.

Holyfield mwenye rekodi ya kutisha ulingoni, mara ya mwisho kupanda ulingoni ilikuwa dhidi ya Nicolai Valuev, Desemba mwaka jana.

Pambano hilo la WBA, liliisha kwa Valuev kupewa ushindi wa pointi, ambao ulilalamikiwa na Evander.

Evander mwenye rekodi ya 47-10-2, 27 KO, anaamini kama atamshinda ‘The White Buffalo’ aliye na rekodi ya 47-4-3, 28 KO, ataweza kumkabili bingwa wa dunia wa WBC, Vitali Klitschko baadaye mwakani.

Ni mara ya kwanza pambano kama hilo kufanyika Afrika baada ya miaka 35; mara ya mwisho ilikuwa ni kati ya Mohammed Ali na George Foreman, ambalo lilipigwa nchini DRC, wakati huo Zaire.

Celestino Mindra, ambaye ni Rais wa Kamisheni ya Ndondi za Kulipwa nchini Uganda, pia amethibitisha uwepo wa pambano hilo.

“Tunazo taarifa kuhusu pambano hilo tangu miezi miwili iliyopita ambalo awali lilikuwa lifanyike Desemba, lakini likasogezwa hadi Januari,” alisema Mindra na kuongeza:

“Ni heshima na tukio la kihistoria kwa Uganda kuandaa pambano kubwa kama hili, ni kitu ambacho tumekuwa tukipigania katika kuinua mchezo huu,” alisisitiza.

Holyfield ni bondia mwenye historia na rekodi ya aina yake katika ulingo wa masumbwi dunini, ikiwamo kuwahi kumchapa Mike ‘ Iron’ Tyson.



juu