HABARI MPYA LA JANA MATANGAZO BEI ZETU WASILIANA NASI TUMA HABARI
jumanne, 29 desemba 2009
Yaliyopita
Pekua Tovuti

Mrema aingia rasmi mtandao mpya wa JK


na Hellen Ngoromera na Humphrey Shao

 

MTANDAO mpya wa kumsafisha na kumjenga upya kisiasa Rais Jakaya Kikwete, huku ukiwasakama wanaomkosoa, unazidi kupanuka baada ya kuwanasa baadhi ya wanasiasa wa upinzani kuongeza nguvu ya wanaCCM katika azima hiyo.

Mbali na wengine waliojitokeza katika wiki chache zilizopita, jana ilikuwa zamu ya Mwenyekiti wa Chama cha Tanzania Labour (TLP), Augustino Mrema, ambaye aliwashambulia wakosoaji wa Rais Kikwete, hasa wanasiasa wastaafu na makada wa CCM waliojitokeza hadharani kumpinga katika kongamano la siku tatu lililoandaliwa na Taasisi ya Mwalimu Nyerere (MNF) mwezi uliopita.

Baadhi ya wanasiasa, waliojitokeza kuwashambulia washiriki wa kongamano hilo na kuisakama MNF kwa kumkosoa Kikwete, ni pamoja na aliyewahi kuwa Mwenyekiti wa CCM Mkoa wa Kagera, Pius Ngeze, ambaye aliwahi kujitangaza kuwa katika mtandao wa awali wa Kikwete kusaka urais mwaka 2005.

Wengine waliojitokeza hadi sasa ni Rais wa TADEA, John Chipaka, Mwenyekiti wa UPDP, Fahmi Dovutwa, Mwenyekiti Mwenza wa REDET, Dk. Benson Bana na Sheikh Yahya Hussein aliyeibuka hivi karibuni na kutisha wanaotaka kugombea urais kwamba watakufa ghafla kama watashindana na Rais Kikwete.

Mrema jana aliongezeka katika kuilaumu taasisi hiyo na wanaomsakama Rais Kikwete.

Katika kauli ya kutovumilia siasa za kukosoana ndani ya chama kile kile, Mrema aliongeza kuwa makada wa CCM wanaotaka kumkosoa rais wajiengue na kuanzisha chama chao.

Alisema iwapo watashindwa kufanya hivyo wajiunge na vyama vya upinzani ama kuzungumzia hayo katika vikao vya Kamati Kuu au Halmashauri Kuu ya Taifa.

Akizungumza na waandishi wa habari jana jijini Dar es Salaam, Mrema alisema vitendo vinavyofanywa na viongozi hao vinatishia na kuhatarisha amani, utulivu na usalama wa taifa.

“Kuongoza nchi si kazi rahisi, hivyo ikiwa wanaona sera za kupambana na ufisadi hazitekelezeki wasipinge wakiwa ndani ya CCM, basi wao ndio wanaotakiwa wafanye maamuzi magumu, ama kwa kuanzisha chama chao ama wajiunge na vyama vya upinzani kama mimi nilivyofanya, lakini kutoa kauli za uchochezi wakati bado ni wanachama wa CCM, wananchi hawatawaelewa,” alisema Mrema.

Kwa mujibu wa mwenyekiti huyo wa TLP, ambaye amewahi kushika nyadhifa nyingi serikalini zikiwamo uwaziri wa mambo ya ndani na unaibu waziri mkuu kauli zilizotolewa na makada hao wa CCM kuwa rais amezungukwa na kundi la wezi na kama anashindwa kuchukua maamuzi magumu atoswe, ikiwa zitaachwa zinaweza kuleta uchochezi.

“Kutokana na uzito wa kauli hizo na mahali zilipozungumziwa, mimi kama Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi na Naibu Waziri Mkuu Mstaafu ambaye pia nimewahi kuwa Mkuu wa Usalama wa Taifa wa Wilaya, naelewa wazi athari zake…nchi isitawalike. Ndiyo maana nimeona niwaiteni kuzungumza juu ya suala hilo. Wala sijatumwa na mtu yeyote.

“Wapo watakaosema kwamba nimeingilia mambo ya chama tawala wakati mimi si mwanachama wa CCM, lakini suala hili lisipokemewa linaweza kusababisha uvunjifu wa amani,” alisema Mrema.

Kwa mujibu wa Mrema anavyoelewa malengo ya Taasisi ya Mwalimu Nyerere ni kukuza amani na utulivu nchini na Afrika nzima, lakini wao walilitumia kongamano hilo kutoa kauli za uchochezi na uzandiki.

Mrema alisema kuwa waliosema rais kazungukwa na kundi la wezi wanamaanisha kwamba naye ni mwizi, jambo ambalo alilipinga.

Alisema kuwa kitendo cha kuchochea na kufanya uzandiki ni kuvunja sheria ya usalama wa taifa na kwamba adhabu yake iko wazi, hivyo ingefaa vyombo vya usalama vifanye kazi kuliko kuacha watu waendelee kuchafua amani kwa kisingizio cha demokrasia.

“Wengine watasema namfagilia rais au pengine nataka kurudi CCM. Mimi simfagilii wala sina mpango wa kurudi CCM isipokuwa rais ni mpambanaji katika vita ya ufisadi kama nilivyokuwa mimi wakati nilipokuwa Waziri wa Mambo ya Ndani na Naibu Waziri Mkuu, hivyo siwezi kuona rais wa nchi hii anaonewa nikanyamaza,” alisema Mrema.

Mrema aliongeza kuwa kama Rais Kikwete angekuwa madarakani wakati ule yeye asingefukuzwa kazi kwa sababu malengo yake ni sawa na ya rais kupambana na ufisadi, hivyo hamfagilii Kikwete na wala hana mpango wa kurudi CCM bali atagombea ubunge wa jimbo huko Vunjo kwa tiketi ya TLP bila msaada wa CCM na kwamba akiingia bungeni atashirikiana na rais yeyote yule iwe kutoka CCM au chama pinzani.

“Kuna watu wanasema kwamba najipendekeza ili CCM iniachie Jimbo la Vunjo na wengine wanasema mimi ni kibaraka wa CCM, lakini kama ni hivyo mbona CCM wameshawarubuni na kuwachukua wenyeviti wangu wa vijiji viwili wa TLP mara tu baada ya kuchaguliwa, hata kabla hawajaapishwa?” alihoji Mrema.

Mrema aliwasuta makada hao akisema wanataka rais achukue maamuzi gani magumu.

“…Ili makada hao waone, alikubali aliyekuwa Waziri wake Mkuu na swahiba wake, Edward Lowassa kujiuzulu kufuatia kuhusishwa na kashfa ya Kampuni tata ya kufua umeme wa dharura ya Richmond.

“Wengine waliochukuliwa hatua kwa kujiuzulu ni mawaziri wake wawili, Nazir Karamagi na Dk. Ibrahim Msabaha sambamba na kuwafikisha mahakamani viongozi wengine kwa kuhusishwa na sakata la EPA,” alisema na kuongeza kuwa EPA ilikuwapo tangu 1992.

Mrema alisema makada wanaomsakama Rais Kikwete kwa kushindwa kusisimamia vizuri sera nzuri za Mwalimu Nyerere kama vile vijiji vya ujamaa, madaraka mikoani, mashirika ya umma na nyingine, inashangaza sasa wanapomwandama na kumchafua rais wakati wao walishindwa na kuhoji kuwa pengine ni uchu wa madaraka hivyo wanataka kurudi madarakani kwa mlango wa uwani.

Alipoulizwa sababu ilivyomfanya azungumzie suala hilo jana wakati alikuwa mmoja wa walioudhuria kongamano la Mwalimu Nyerere, Mrema alimtupia swali hilo Katibu wa chama hicho Hamad Tao ili alijibu ambapo alisema kuwa alinyimwa nafasi ya kuzungumza kwa siku zote tatu za kongamano hilo pamoja na kunyoosha mkono kwa muda mrefu.

Zipo tetesi kwamba Mrema, ambaye afya yake imekuwa ikitetereka katika miaka ya karibuni, na ambaye sasa hivi anaonekana kuimarika upya, anatibiwa kwa gharama za serikali; na kwamba hiyo ni moja ya njia zilizotumika kumnasa, na sasa analipa fadhila kwa kuwashambulia wanaomkosoa Rais Kikwete.

Alipohojiwa na Tanzania Daima jana kwa njia ya simu, Mrema alisema serikali haijawahi kumgharamia matibabu yoyote na wanaoeneza maneno hayo ni waongo na wazushi.

“Juni 2009 nililazwa wiki moja katika hospitali ya KCMC ambayo ni hospitali ya serikali nikapatiwa matibabu ambayo hata hayafiki sh 100,000 na risiti ninazo. Sasa hapo nilichofadhiliwa na serikali ni kitu gani? Mbona watu ni wazushi na waongo? Huo ni unafiki, tutaendelea na mambo haya hadi lini?

“Kwa kifupi sijawahi kutibiwa kwa gharama za serikali, hivyo watu wasizushe mambo,” alisema Mrema.

Akizungumzia kuhusu kuhusishwa na serikali ya awamu ya nne, Mrema alikanusha vikali suala hilo na kusema ametoa kauli dhidi ya wanaomsakama Rais Kikwete kwa kuwa ni haki na wajibu wake kama mzalendo wa nchi hii.

“Sijaingia katika mtandao wa serikali, nimezungumza hayo leo kama mwananchi mzalendo, kwani kuna ubaya gani kusema hayo? Mtendeeni haki Rais Kikwete jamani,” alisema Mrema.

Alipoulizwa Mwandishi wa Habari wa Rais Msaidizi, Premmy Kibanga kuhusu serikali kumhudumia Mrema matibabu, alisema hafahamu yanayoendelea kwa kuwa yupo likizo.

“He! siku hizi rais ndio anapeleka watu hospitali? Waulize Wizara ya Afya, kwa sasa niko nyumbani likizo, sijui yanayoendelea,” alisema Premmy.

Tangu kuibuka kwa mtandao huo, watetezi wa Rasi Kikwete wamekuwa wakiwaita wakosoaji majina kama wehu, wahuni, genge na watu wenye wivu, huku baadhi ya wanasiasa na vyombo vya habari vikiishambulia Taasisi ya Mwalimu Nyerere kwa kuiita genge la Butiku.

Baadhi ya washiriki wa kongamano hilo walitoa kauli kali za kukosoa uongozi wa Rais Kikwete, huku Askofu Msaidizi Method Kilaini, akikemea kwa ukali ufisadi serikalini na kusema ‘nchi inatembea uchi’.

Waziri mstaafu Mateo Qares, ambaye pia aliwahi kuwa mkuu wa mkoa, alitoa rai kwamba kama rais atashindwa kushughulikia mafisadi, asigombee tena mwakani.

Wengine waliokosoa utendaji wa Rais Kikwete ni makada wa CCM, akina Fred Mpendazoe, Stephen Mashishanga, Nape Nnauye, Joseph Warioba na washiriki wengine walioonyesha kutoridhishwa na mwenendo wa serikali.



juu