JUZI mtandao wa Elimu Tanzania (TEN MET) kupitia mradi wa Uwezo Tanzania, umebaini kuwa asilimia 70 ya wanafunzi wa shule za msingi hawajui kusoma Kiswahili kwa ufasaha.
Kwa mujibu wa Kaimu Mkurugenzi wa mradi huo, Dk. Grace Soko, utafiti wao waliufanya kwenye wilaya 38 hapa nchini, ambao uliwahusisha watoto wenye umri wa miaka mitano hadi 16, ukiwa na lengo la kujua uwezo wa watoto kujifunza.
Utafiti huo umebaini asilimia 30 ya watoto wa shule za msingi ndio hufahamu kusoma hadithi za Kiswahili na somo la Kiingereza ni tatizo kwa watoto, kwani nusu ya wanaomaliza darasa la saba hawaliwezi.
Matokeo hayo pia yanaonyesha kuwa mhitimu mmoja kati ya wahitimu watano wa elimu ya msingi hawawezi kusoma Kiswahili cha ngazi ya darasa la pili huku wahitimu saba kati ya 10 wanaweza kufanya hesabu za ngazi ya darasa la pili.
Utafiti huo pia umebaini hadi darasa la tatu watoto saba kati ya 10 hawawezi kusoma Kiswahili cha msingi, watoto tisa kati ya 10 hawawezi kusoma Kiingereza cha msingi na watoto wanane kati ya 10 hawawezi kufanya hisabati za msingi.
Tunaamini kuwa matokeo haya yatashughulikiwa na watendaji wa serikali ili kunusuru taifa na kuwa na wanafunzi wanaomaliza elimu ya msingi bila ya kujua kusoma au kuandika.
Matokeo ya utafiti huu yanaonyesha sehemu zinazotakiwa kufanyiwa kazi kwa ukaribu zaidi na halitakuwa jambo la busara kama watendaji wa serikali wataanza kulumbana au kuyakana matokeo ya utafiti huu.
Tunaamini kuwa lengo la serikali ni kuhakikisha inatoa elimu bora kwa kila mwanafunzi, lakini lengo hilo halitaweza kufanikiwa kama matatizo yanayoonekana hivi sasa hayatapatiwa ufumbuzi.
Serikali inapaswa ikae na walimu, wanafunzi na wadau wa elimu ili kutafuta chanzo cha kuongezeka idadi ya wahitimu wa elimu ya msingi wasiojua kusoma na kuandika ili kutafuta mbinu madhubuti ya kulitatua.
Walimu wanaofundisha katika mazingira magumu ya kutokuwa na nyumba za kuishi, mishahara midogo, vifaa duni kamwe hawawezi kutoa wahitimu bora bali wataendelea kutafuna rasilimali za taifa bila kuwapo mafanikio.
Tunatambua jitihada kubwa za serikali katika kuboresha elimu ya msingi, sekondari, vyuo na ile ya watu wazima lakini jitihada hizo hazitakuwa na maana kama wahitimu wanamaliza madarasa badala ya kuwa na maarifa yaliyokusudiwa.
Tunaamini kuna mafanikio makubwa katika uandikishwaji wa watoto shule, ujenzi wa shule za sekondari na msingi, lakini jitihada hizi zitakuwa ni kupoteza fedha za walipa kodi kama serikali haitatupia macho tatizo la kuwapo kwa wahitimu wasiojua kusoma na kuandika.
Tulishangazwa na taarifa zilizotolewa na vyombo vya habari hivi karibuni kuwa kuna mwanafunzi alimaliza elimu ya msingi lakini hajui kusoma na kuandika.
Taarifa kama hizi ndizo zinazopaswa kufanyiwa kazi na serikali badala ya kila kukicha kuelezea mafanikio waliyoyapata kwa kujenga shule nyingi na kuongeza idadi ya walimu na mengineyo.
Tunaamini pia umefika wakati wa kuboreshwa kwa mitaala ya walimu pamoja na kuwafuatilia kwa ukaribu zaidi wawapo kazini, ili elimu wanayoipata iweze kuwa na msaada zaidi kuliko ilivyo hivi sasa, ambapo muda wa mafunzo si mwingi kama ilivyokuwa miaka ya nyuma.
Mafunzo ya muda mfupi yanayotolewa kwa walimu kwa namna moja au nyingine yamechangia kwa kiasi kikubwa ongezeko la wahitimu wasio na maarifa pamoja na kushuka kwa kiwango cha elimu.
Tunaamini matokeo ya utafiti huu wa Uwezo Tanzania na ya taasisi nyingine, yatafanyiwa kazi ili taifa lisije likawa tegemezi la wataalamu kutoka nje ya nchi.