HABARI MPYA LA JANA MATANGAZO BEI ZETU WASILIANA NASI TUMA HABARI
jumanne, 23 novemba 2010
Yaliyopita
Pekua Tovuti

Mamia wamzika Mkambi


na Ruhazi Ruhazi

 

MAMIA ya wadau wa soka, jana walijitokeza kuuzika mwili wa nahodha wa zamani wa Yanga, Juma Mkambi ‘Jenerali’, aliyefariki juzi asubuhi kwenye Hospitali ya Taifa ya Muhimbili baada ya kuugua kwa siku kadhaa maradhi ya tumbo.

Mkambi aliyezikwa jana kwenye makaburi ya Kisutu, jijini Dar es Salaam, ni kati ya wachezaji mahiri wa zamani aliyewahi kung’ara vilivyo na klabu kadhaa ikiwemo Yanga na timu ya soka ya Tanzania ‘Taifa Stars’.

Akizungumzia kifo hicho, Rais wa Shirikisho la Soka la Tanzania (TFF), Leodegar Chilla Tenga, alisema taifa limepoteza shujaa wa kweli katika soka aliyetoa mchango mkubwa katika maendeleo ya mchezo huo na kusema ameondoka huku mchango huo ukiwa bado unahitajika.

Alisema Mkambi alikuwa mtu mwenye kupenda maendeleo ya soka, hivyo hata baada ya kuacha soka, aliendelea kutoa ushauri wa nini kifanyike katika kuinua mchezo huo ambao aliupenda katika maisha yake yote.

Mkambi aliyezaliwa mwaka 1955, alianza kuichezea Yanga tangu mwaka 1978 na mwaka 1979, aliitwa kwenye kikosi cha Taifa Stars, akiwa kati ya walioshiriki fainali za Kombe la Mataifa ya Afrika mwaka 1980, Lagos, Nigeria.

Mkambi aliitumikia Yanga na Stars akiwa nahodha hadi alipostaafu mwaka 1987, na kugeukia ukocha ambao ameufanya hadi anafariki duniani juzi asubuhi.

Chama cha soka cha Pwani (COREFA) ambako alikuwa Mkurugenzi wa Ufundi wa timu za mkoa, imetoa pole ya sh 150,000 na Yanga wakitoa sh 500,000.

Aidha, Shirika la Elimu Kibaha limeahidi kushiriki kikamilifu katika kisomo kitakachofanyika mwishoni mwa wiki ijayo.

Naye Mkurugenzi wa Tanzania Stars, Mussa Kisoki, alitumia nafasi hiyo kuwaomba wadau wa soka kujaliana wakati wa matatizo akisema Mkambi angefurahi sana kama umati uliojitokjeza katika mazishi yake jana, ungekuwa ukifika hospitali kumjulia hali.

Kisoki alitoa wito kwa TFF kuangalia uwezekano wa kuwasaidia wachezaji wa zamani wa Stars ili kuboresha maisha yao kwani wengi wao, wanaishi katika maisha duni, hoja ambayo ilipokewa na Tenga.

Kati ya wadau waliojitokeza, ni aliyekuwa Naibu Waziri wa Habari Utamaduni na Michezo, Joel Bendera, Mwenyekiti wa zamani wa FAT (sasa TFF), Muhidin Ahmad Ndolanga.

Mwingine ni aliyekuwa Katibu Mkuu wa FAT, Ismail Aden Rage, ambaye pia ni Mwenyekiti wa Simba na Mbunge wa Tabora Mjini kwa tiketi ya CCM na Mkurugenzi wa michezo, Leonard Thadeo.

Walikuwepo pia viongozi wengine wa TFF, wabunge wa Ilala, Mussa Azan ‘Zungu’ na Kinondoni, Idd Azan, Makocha, wachezaji wa zamani hasa waliocheza na Mkambi kwenye miaka ya 1970 na 1980.



juu