HABARI MPYA LA JANA MATANGAZO BEI ZETU WASILIANA NASI TUMA HABARI
jumatatu, 9 februari 2009
Yaliyopita
Pekua Tovuti

Matokeo ya kidato cha nne

•  Shule za wasichana zaongoza tena kitaifa

na Edward Kinabo

 

MATOKEO ya mtihani wa Taifa wa Kidato cha Nne uliofanyika nchini Oktoba, mwaka jana yametangazwa na Baraza la Mitihani la Tanzania (NECTA), huku shule za sekondari za wasichana za St. Francis ya mkoani Mbeya na Marian ya Pwani zikiongoza tena katika orodha ya shule 10 bora zilizofaulisha vizuri.

Hii ni mara ya tatu mfululizo kwa shule za wasichana kufanya vizuri kuliko wavulana.

Matokeo hayo yanaonyesha kuwa jumla ya watahiniwa 168,420, sawa na asilimia 75.82, wamefaulu mtihani mwaka jana, uliotawaliwa na kosoro nyingi, ikiwemo kuvuja kwa somo la hisabati na kusababisha kurejewa tena kwa mtihani wa somo hilo.

NECTA pia imefuta matokeo ya watahiniwa 347 waliofanya udanganyifu na matokeo ya watahiniwa 50 wa shule na wawili wa kujitegemea, waliokiuka taratibu za usajili na kufanya mtihani huo bila ya kuwa na sifa zinazotakiwa.

Matokeo hayo yametangazwa na Katibu Mtendaji wa NECTA, Joyce L. Ndalichako, kupitia taarifa yake iliyotolewa jana kwa vyombo vya habari nchini.

Mbali ya St Francis na St Marian Girls’, taarifa hiyo ilizitaja shule nyingine bora zenye watahiniwa 35 au zaidi, kuwa ni St. Joseph – Kilocha Seminary (Iringa), Uru Seminary (Kilimanjaro), Dungunyi Seminary (Singida), Anwarite Girls’ S.S (Kilimanjaro), St. Mary Goreti S.S (Kilimanjaro), Feza Boys (Dar es Salaam), Don Bosco Seminary (Iringa) na Rosmini S.S (Tanga).

Kwa mujibu wa taarifa hiyo, shule nyingine kumi bora zenye watahiniwa chini ya 35 ni Scolastica S.S (Kilimanjaro), Feza Girls’ S.S (Dar es Salaam), Brooked S.S (Iringa), Bethelsabas Girls S.S (Iringa), Maua Seminary (Kilimanjaro), Rubya Seminary (Kagera), St. Marys Junior Seminary (Pwani), Katoke Seminary (Kagera), Kilomeni S.S (Kilimanjaro) na St. Carolus S.S. (Singida).

Taarifa hiyo pia ilizitaja shule kumi za mwisho zenye watahiniwa 35 au zaidi kuwa ni pamoja na Selembala S.S (Morogoro), Kilindi S.S (Pemba), Ngwachani S.S (Pemba), Michiga S.S (Mtwara), Ummussalama S.S (Pwani), Chunyu S.S (Dodoma), Busi S.S (Dodoma), Uondwe S.S (Pemba), Nala S.S (Dodoma) na Maawal S.S (Tanga).

Shule kumi za mwisho zenye watahiniwa chini ya 35 ni Juhudi Academy (Zanzibar), Mima S.S (Dodoma), Selenge S.S (Singida), Kijini S.S (Zanzibar), Kwamkoro S.S (Tanga), Kwala S.S (Pwani), Mtende S.S (Zanzibar), Ng’hoboko S.S (Shinyanga) na Mwadui Technical S.S (Shinyanga).

Kupitia taarifa hiyo, Ndalichako alisema kuwa jumla ya watahiniwa 165,136, sawa na asilimia 85.95, walifaulu mtihani huo mwaka juzi, hivyo kufanya kuwe na ongezeko la watahiniwa 3,284 waliofaulu mwaka jana, ikilinganishwa na idadi ya waliofaulu mwaka juzi.

“Hata hivyo, asilimia ya ufaulu inaonyesha kuwa chini kwa asilimia 10.13 kutoka asilimia 85.95 mwaka 2007 hadi asilimia 75.82 kwa mwaka 2008,” ilisema taarifa hiyo.

Taarifa hiyo pia inaonyesha kushuka kwa ufaulu wa madaraja, kuanzia daraja la kwanza hadi la tatu, ambapo mwaka jana walifaulu watahiniwa 41, 018 sawa na asilimia 18.47, ikilinganishwa na watahiniwa 44.348, sawa na asilimia 23.51 waliofaulu katika madaraja hayo mwaka juzi.

“Hivyo, kwa kutumia kigezo cha madaraja la kwanza hadi la tatu, ubora wa ufaulu wa mtihani wa Kidato cha Nne Oktoba, 2008 umepungua kwa asilimia 5.04,” ilieleza taarifa hiyo.

“Ufaulu kwa masomo unaonyesha kuwa watahiniwa wamefanya vizuri zaidi katika somo la Kiswahili ambapo asilimia 81.59 ya watahiniwa wa shule wamefaulu. Ufaulu katika somo la ‘Basic Mathematics’ upo katika kiwango cha chini, ambapo ni asilimia 24.33 tu ya watahiniwa wa shule waliofaulu somo hilo,” ilieleza taarifa hiyo ya NECTA.

Ndalichako aliitaja idadi ya watahiniwa wa shule waliofaulu mtihani huo mwaka jana kuwa ni 126, 617, sawa na asilimia 83.69 ya waliofanya mtihani na kupewa matokeo, kati yao wasichana wakiwa 55,285, sawa na asilimia 81.16 na wavulana 71, 332, sawa na asilimia 85.76.

Jumla ya watahiniwa wa shule 112,631, sawa na asilimia 89.90, walifaulu mtihani huo mwaka juzi, hivyo kufanya kuwe na ongezeko la watahiniwa wa shule 13,986, waliofaulu mwaka jana ikilinganishwa na waliofaulu mwaka juzi.

“Hata hivyo, asilimia ya waliofaulu mtihani huo imepungua kwa asilimia 6.21 kutoka 89.90 mwaka juzi 2007 hadi 83.69 kwa mwaka 2008,” alibainisha Ndalichako kwenye taarifa hiyo.

Kwa upande wa watahiniwa wa kujitegemea, alisema idadi ya waliofaulu mtihani huo ni 41,803 sawa na asilimia 59.01, wakiwemo wanawake 21,187, sawa na asilimia 55.86 na wanaume 20,616, sawa na asilimia 62.65.

Aidha, NECTA, imesitisha kutoa matokeo ya watahiniwa 5,135 waliofanya mtihani huo, kwa sababu ya kutolipa ada na kuahidi kuwa matokeo yao yatatangazwa mara watakapolipa ada wanayodaiwa.

Baraza hilo pia limesitisha matokeo ya watahiniwa 22 wa Shule ya Sekondari Upendo, kutokana na kutokuwa na alama za maendeleo ya kila siku.

Wakati huo huo baraza hilo limesitisha matokeo ya watahiniwa 4,808 wa mtihani huo, katika masomo ambayo hawakuwasilisha alama za maendeleo ya kila siku (CA data) na kuahidi kutoa matokeo yao mara baada ya wakuu wao wa shule kuwasilisha alama hizo ndani ya kipindi cha miezi sita kuanzia leo.

Baraza hilo pia limetangaza kufaulu kwa watahiniwa wa mtihani wa maarifa (QT), 5,653 sawa na asilimia 27.02, ikilinganishwa na asilimia 24.44 ya watahiniwa waliofaulu mtihani kama huo mwaka juzi.



juu