SIKU zinazidi kupita lakini bado nimeguswa na tukio la Mkuu wa Wilaya kuwacharaza viboko walimu wa shule za msingi Bukoba wiki iliyopita.
Ni tukio linalotupa taswira halisi ya Watanzania wanavyopigwa na kupigika kila siku. Na sababu kuu ni mbili - ubabe wa serikali na unyonge wa wananchi.
Ubabe wa serikali unatokana na ukosefu wa maarifa na mbinu mbadala za kuchochea maendeleo. Serikali bado inaamini katika mabavu ya kijima katika michakato ya maendeleo ya karne ya 21.
Watawala wanatumia mbinu za zima moto. Hawatafuti chanzo cha tatizo. Na katika hili la walimu, chanzo cha kushuka kwa elimu, utoro au kuchelewa kwa walimu kazini, na morari duni waliyo nayo walimu, ni serikali yenyewe.
Ina nyenzo za kuwahamasisha bila kuwachapa viboko na kuwadhalilisha mbele ya umma! Lakini wanaozitumia wana uwezo mdogo.
Na hii inatufanya pia tujadili aina ya viongozi tulio nao na mfumo unaowazalisha, hasa hawa wa kuteuliwa. Unapokuwa na taifa linaloongozwa na kundi la wanajeshi wastaafu kutoka Ikulu hadi wilayani (orodha ni ndefu); wanapogundua mambo yamekwama na wao hawana suluhisho, unatarajia nini kama si viboko na mateke?
Maana kinachofanyika sasa hivi ni mchakamchaka wa kuelekea uchaguzi mkuu mwaka kesho. Na kabla ya hapo kuna uchaguzi wa serikali za mitaa mwaka huu.
Kila kiongozi anaandaa orodha ya ‘mafanikio’ katika eneo lake la kazi. Akili zimekwama, wametanua misuli!
Si hili tu la Bukoba. Yapo mengi yanatendeka mikoani na wilayani – na hata kwenye kata - hayaripotiwi kwa uzito wake.
Na haya ni sehemu ya matunda na mfumo mfu. Wanaouonea huruma kidogo wanauita mfumo mkongwe na mchovu uliofumwa katika katiba nzee inayolalamikiwa kila siku.
Sikumbuki kama iliwahi kutokea kiongozi wa kuchaguliwa, kama mbunge, akashika fimbo na kuwachapa wananchi, watu wazima kama yeye.
Lakini DC amethubutu kuzivamia shule na kuamuru walimu wachapwe viboko. Tukio hili ni jeuri ya madaraka ya kupewa; kielelezo cha uwezo mdogo.
Hata baada ya semina elekezi za Ngurdoto na kwingineko, wateule wenye hulka za namna hii hawaelimiki na hawabadiliki. Na hata wakifukuzwa kazi, bila mfumo wenyewe kufumuliwa, na kuweka vigezo vipya vya kuwapata, tutaendelea kupigwa na kupigika.
Lakini la msingi ni mjadala mpana juu ya nafasi ya wakuu wa wilaya. Tumesema kwa zaidi ya miaka 15 sasa kwamba hatuhitaji wakuu wa wilaya.
Kazi zao zinaweza kufanywa na wakurugenzi wa halmashauri husika; ambao wanatarajiwa kuwa na elimu na taaluma ya uongozi, na uteuzi wao utazingatia vigezo muhimu vinavyoeleweka na kuelezeka.
Wakuu wa wilaya ni mzigo kwa wananchi. Ni wateule wa kisiasa, na wanafanya kazi za kisiasa, wakiwa na mamlaka makubwa kiutendaji kuliko viongozi wa kuchaguliwa na wataalamu.
Hii ndiyo sababu ya migogoro isiyoisha kati ya wakuu wa wilaya na wakurugenzi wao. Siasa zinaingilia taaluma. Maendeleo yanakwama.
Manono wanayolipwa, mamlaka waliyonayo na jeuri wanayopewa, ni kashfa katika nchi iliyo kwenye mchakato wa kujenga misingi ya utawala bora.
Ni vema huyu amefukuzwa kazi, lakini hoja kuu hapa si kumfukuza mmoja, bali kufuta cheo cha mkuu wa wilaya ili kuokoa pesa za walipa kodi zinazotunza mamia ya wakuu wa wilaya wasio na kazi ya maana kwa taifa. Tuelekeze nguvu kwenye ujuzi na utaalamu, ambao utakuwa msukumo kwa maendeleo.
Viboko vya Bukoba vinaweza kutusaidia kufufua mjadala wa hoja hii ambayo inazingatia pia ukweli kwamba sheria inayounda ofisi hii ni mojawapo ya sheria mbaya zilizoorodheshwa na Tume ya Jaji Francis Nyalali mwanzoni mwa miaka ya 90.
Kwa nini tunang’ang’ania kuongozwa na sheria mbovu? Tutapataje utawala bora chini ya sheria mbaya?
Kama kuna wanaotilia shaka hoja hii, wachunguze yanayotendeka katika wilaya zetu.
Wakuu wa wilaya ni vijimungu vidogo vya maeneo husika – vinavyolazimisha ibada kutoka kwa wananchi. Na tujiulize walivyopata ukuu wenyewe wa wilaya, na wanavyoutumia.
Pili, tuwajadili na walimu wenyewe waliopigwa. Tuwaonee huruma. Wamedhalilishwa. Adha zao tunazijua, na zimesababishwa na mwajiri wao (serikali). Tuwahamasishe wadai haki zao hadi zipatikane, na walipwe fidia ya kudhalilishwa.
Tuwaeleze walimu wetu waache unyonge. Serikali imekuwa inawaonea na kuwanyonga kwa sababu inajua wao ni wanyonge.
Wafike mahali waiambie serikali ‘inatosha.’ Wachukue hatua. Wajikomboe.
Kwa nini nasema hivi? Upo uwezekano mkubwa kwamba baada ya rais kumfukuza kazi ‘mbabe wao’ walimu wanaweza kunywea.
Badala ya kuendeleza harakati za kutafuta haki zao, kuibana serikali na kujikomboa; badala ya kuona na kutambua siasa inayofanywa na wakubwa kwa kutumia na hata kudhalilisha walimu, wakaanza kuisifu na kuandamana kumpongeza rais!
Unyonge wao ndio ulimpa DC mwenyewe jeuri ya ‘kupiga.’ Nina hakika walikuwa na uwezo wa kumgomea na kumtimua hadi mamlaka nyingine ziingilie.
Na kama ingewezekana, wao ndio wangempiga – yeye na askari wake mmoja aliyeambatana naye hadi ofisini kwao.
Walimu walikuwa na kila sababu ya kujitetea. Walipaswa kutambua kuwa DC huyo hakuwa na mamlaka ya kuwacharaza viboko.
Kama wangempiga, wangekuwa wanajitetea dhidi ya mvamizi. Wangekuwa wanamdhibiti asitumie vibaya mamlaka aliyopewa. Wangekuwa wanamsaidia asimdhalilishe rais wa nchi ambaye anawakilishwa na DC huyo katika eneo lake.
Sitetei shari, bali nasema hii ni haki yao. Walipaswa kuitumia. Naamini hata rais mwenyewe hawezi kwenda shuleni kuwapiga walimu viboko. Hakuna sheria inayomruhusu.
Kwa hiyo, kama walimu wangemdhibiti DC, wangekuwa wanamshughulikia kama jambazi yeyote tu. Na wangejenga heshima yao. Wakati mwingine najiuliza.
Na huu unyonge wa walimu ni kielelezo cha unyonge wa wananchi. Serikali inatunyanyasa kwa sababu inajua tu wanyonge. Tunaogopa kujitetea na kuidhibiti. Tunaogopa kuikosoa.
Si hivyo tu. Inajua kwamba walio wengi hatuelewi haki zetu na mipaka ya majukumu na mamlaka ya wenzetu.
Maana kama walimu tunaowategemea kuhamisha ujuzi na elimu kutoka vyanzo mbalimbali hadi kwenye vichwa vya watoto wetu (na sisi ni zao la mfumo huo huo) hawajui, itakuwaje jamii nzima iliyozalishwa na mfumo huo huo? Nayo itatarajiwa kuwa mbumbumbu, nyonge na dhalili!
Viboko vya Bukoba ni kielelezo cha viboko ambavyo serikali inawachapa wananchi kila siku, na hawajitetei.
Na kauli za baadhi ya wananchi walioshabikia dhuluma hii ni upofu mwingine wa kiakili unaotokana na mfumo ule ule unaowadumaza walimu na wanafunzi wao.
Na haraka ya walimu kuandaa maandamano kumpongeza rais kwa kumtimua DC ni kielelezo cha ziada jinsi walimu wanavyotumika kwa malengo ya kisiasa. Watasahau hilo leo. watabembelezwa kwa muda hadi uchaguzi upite, na baadaye watanyanyaswa tena.
Si hilo tu, ni kielelezo pia kwamba walimu wameshindwa kuchambua maana ya hatua na kauli za serikali – si katika hili la Bukoba tu, bali katika matukio mengi ya hivi karibuni.
Tukumbuke kuwa imebaki miezi 20 kabla ya Uchaguzi Mkuu ujao mwakani. Ndani ya siku zisizozidi 700 (kama hakutatokea mabadiliko au sababu zozote) tunatarajia kuwa na uongozi mpya kitaifa.
Hata kama watakuwa wale wale, watakuwa wamechaguliwa kwa kura mpya. Hizi ndizo zinazotafutwa kwa udi na uvumba.
Ndizo zinazoongoza matendo na kauli za wakubwa; mikutano wanayofanya, hoja wanazoibua au kuzima ndani na nje ya Bunge, ziara za wakubwa na matamko makali makali yanayotolewa, ahadi nyingine mpya mpya; na wengine wanasema hata baadhi ya matukio ya huko mahakamani. Ni sehemu ya siasa za kuelekea 2010.
Miaka mitatu ya kazi imekwisha. Imebaki miwili ya uchaguzi – serikali za mitaa (2009) na uchaguzi mkuu (2010).
Kilichowashinda kimewashinda. Sasa wanaandaa orodha ya ‘mafanikio’ watakayotumia kuomba ridhaa ya kuchaguliwa tena. Wakiweza kutuhadaa tena, watarejea madarakani kwa kishindo. Na baada ya hapo, viboko vinaanza tena!
Walimu (na wananchi kijumla) walipaswa kujua kwamba huu si wakati wa kulala na kuchapwa viboko vingine, bali ni wakati wetu wa kuicharaza serikali, iwajibike.
Walipaswa kujua kwamba serikali ile ile inayowazuia wao kuwachapa wanafunzi, haiwezi kumruhusu DC awachape wao.
Na kama wapo wananchi wanaotetea dhana ya kuchapana viboko, huku wakitoa mifano ya mabavu yalivyosaidia kusukuma mbele maendeleo wakati fulani, ni vema sasa tukubaliane nao kwamba viboko hivyo tusipigwe sisi wananchi.
Ipigwe serikali kwa sababu yenyewe ndiyo inayokusanya kodi, na ndiyo inayosababisha dhiki na ugumu unaotafuna jitihada za wananchi maskini wanaojitahidi kujikwamua.
Na hata kama kuna watu wanastahili kupigwa viboko katika nchi hii, si walimu. Wanafanya kazi nzito kuliko ya wanasiasa. Wanastahili heshima yao. Lakini wanaikosa kwa sababu nao wamejinyenyekeza mno kwa wanasiasa.
Naamini sasa wameshaelewa; kwamba wana nguvu, uwezo na mbinu za kuwacharaza viongozi wababe (wanasiasa) ndani ya siku 700 zijazo.