HABARI MPYA LA JANA MATANGAZO BEI ZETU WASILIANA NASI TUMA HABARI
jumapili, 15 machi 2009
Yaliyopita
Pekua Tovuti
Wasiliana na Mwandishi
+447984584292
ansbertn@yahoo.comTuma barua-pepe
www.ngurumo.blogspot.comTembelea blogu
Kadhi atawatafuna wakubwa 2010

Ansbert Ngurumo

 

KATIKA miaka mitatu iliyopita CCM wameshindwa kumaliza mgogoro wa kisiasa Zanzibar kwa sababu kuu moja. Walikipenda chama chao kuliko nchi yao.

Wanajua chanzo cha matatizo ya Zanzibar. Mengine wameyasababisha wenyewe. Kwa hiyo, wanaweza kuyamaliza kama watataka.

Lakini matatizo ya Zanzibar yamewasaidia na yanaendelea kuwasaidia CCM kuwa madarakani. Kwa hiyo, mtu yeyote mwenye akili timamu hawezi kukubaliana nao kwamba wana nia ya kuyamaliza.

Ndiyo maana sisi wengine tumekuwa tukitilia shaka matamshi ya viongozi wa CCM kuhusu hali ya kisiasa Zanzibar, na kile kinachoitwa ‘nia ya Rais Jakaya Kikwete’ kumaliza mgogoro huo.

Hakuna nia. Kama ipo haijulikani kwa wengine; au si nia njema. Isingewezekana kwamba Kikwete huyuhuyu tunayemjua amgeuke Rais Amani Karume huyuhuyu ambaye alishiriki ‘kumtafutia urais wa Zanzibar’ uliosaidia pia nguvu ya Zanzibar kumuunga Kikwete zamu yake ilipofika.

Wanaojua siasa za Halmashauri Kuu ya CCM (NEC) na jinsi Karume alivyopenya kwenye tundu la sindano mwaka 2000 kuwapiku wagombea wenzake ndani ya CCM, wanajua ninachosema.

Hapo ndipo nguvu ya ‘mtandao’ ilianza kuonekana. Ndipo wazo la ‘vijana’ wa CCM kupata madaraka makubwa lilipoanza kukomaa.

Na wanaojua mchango wa Karume kwa urais wa Kikwete watakubaliana nami kwamba tangu awali Rais Kikwete alitumia kauli za kidiplomasia kujadili suala hili, lakini hakuwa na nia ya dhati ya kumaliza mgogoro wa Zanzibar. Walau si katika kipindi cha uongozi wa Rais Karume.

Ndiyo maana baada ya ‘makubaliano’ ya wajumbe wa Kamati ya Mwafaka kati ya vyama viwili (CUF na CCM) lilijitokeza suala la ‘pendekezo’ kutoka kwa Rais Karume.

Pendekezo hili liliibuliwa Butiama kwenye kikao cha NEC ambacho kiliwadhihirishia Watanzania kwamba nia ya awali ya CCM na viongozi wake ilikuwa kuwachezea akili wanachama na viongozi wa Chama cha Wananchi (CUF).

Wengine walidhani kwamba Rais Kikwete ni mjinga au ni dhaifu kiasi cha kumwachia Rais Karume avuruge mwenendo wa Kamati ya Mwafaka kiujanja ujanja. Kikwete hakuwa mjinga.

Wala tusidhani Karume alimzunguka Kikwete. Hoja yake isingesikilizwa. Kwa mamlaka makubwa aliyonayo kama mwenyekiti wa CCM na Rais wa Tanzania, Kikwete akitaka mgogoro wa Zanzibar uishe leo, utaisha.

Kwa sisi tunaomjua, Rais Kikwete ni bingwa wa kuahirisha mambo magumu. Hapendi lawama, lakini zitakuja tu. Hili la mwafaka limeshaahirishwa. Halitatafutiwa ufumbuzi wowote utakaomkuta Karume madarakani. Tayari amemsaidia.

Wale waliozuzuliwa na maneno matamu ya rais wakati akihutubia Bunge mara ya kwanza baada ya kuapishwa Desemba mwaka 2005, sasa wajihesabu kwamba wameliwa.

Hawakumjua; yeye aliwajua. Ndiyo maana hadi leo bado wanafikiri kwamba kuna lolote litakalofanyika kabla ya uchaguzi mkuu wa 2010. Yeye anajua kwamba halipo!

Si hilo tu. Katika miaka mitatu hii, Rais Kikwete ameahirisha pia jambo jingine nyeti – Mahakama ya Kadhi Mkuu. Mashabiki wa ahadi na maneno matamu matamu ya wakubwa bado wanachekelea na kunawa mikono mbele yake.

Wanasubiri ukamilifu wa mchakato wa ‘maoni ya wananchi.’ Nilishawaonya – wengine hawakunielewa – kwamba hili nalo litaahirishwa; si tu hadi 2010, bali linaweza kusubiri hadi Kikwete aondoke madarakani.

Ameishasoma alama za nyakati. Ameshajua maoni ya wananchi. Kuna kundi analoogopa kugombana nalo. Kama kawaida, hataki lawama, na haonekani kama yuko tayari kuwaruhusu Waislamu waendelee na hoja yao, waanzishe ofisi yao bila kuitumia serikali na bila kuwashirikisha waumini wa dini nyingine zisizohusika nalo.

Ndiyo maana alishakiri mbele ya maaskofu kwamba ingawa ndiye alilinadi suala hilo kwa wananchi wakati akiomba kura, si yeye aliyeliingiza kwenye Ilani ya Uchaguzi!

Lakini ndiye aliyepigiwa kura na kupewa nguvu ya kufanya maamuzi magumu. Na hakusema kama ndiye aliyeingiza masuala yote mengine kwenye Ilani hiyo!

Alichomoa hilo kwa sababu anajua unyeti wake, anasikia kelele zinazopigwa kuliunga mkono na kulipinga; na hataki kuwajibika au kuwa mkweli kwamba atalitekeleza au la.

Amelirusha kwa wananchi ili kujikosha mikono, aweze kusema hitimisho lolote litakalofikiwa si lake bali la wananchi. Kwa hiyo, wanaosubiri uamuzi wa Rais Kikwete kuhusu Mahakama ya Kadhi Mkuu, wamechelewa. Alishaufanya.

Kinachosubiriwa ni muda upite, munkari wa wananchi ushuke, na wananchi tusingiziwe.

Sitashangaa iwapo suala hili litasukumwa hadi mwisho wa awamu yake ya utawala. Hizi ni dalili kwamba yawezekana uamuzi ulishafanyika kimya kimya: Mwafaka wa Zanzibar baada ya Karume, na Mahakama ya Kadhi Mkuu baada ya Kikwete. Tusubiri.

Watawala wetu ni waoga. Wamekosa ujasiri wa kutekeleza uamuzi mgumu kwa ajili ya taifa; ama kutimiza au kuvunja ahadi.

Lakini jambo la uhakika ni kwamba ahadi hizi zitawatafuna wao na warithi wao; na kwa hakika warithi wao wataonewa kwa sababu watakuwa ‘wamebambikiwa.’

Ulishatolewa ushauri pia kwamba kama hoja hii inawashinda wasione aibu kuzingatia hoja za wananchi, waiondoe serikali katika mchakato huo, waurudishe kwa Waislamu wenyewe, waunde mahakama yao.

Wao wameona kuahirisha uamuzi ndiyo njia ya kukabiliana na madai ya waumini, ambao ipo siku nao watagundua kwamba wanapigwa danadana ile ile ambayo wamepigwa wadau wa CUF. Je, watakuwa tayari kusubiri hadi Kikwete aondoke?

Tukubaliane. Tabia ya wakubwa kushindwa kusema ukweli unaouma ndiyo inayoleta chokochoko na kuvunja misingi ya amani wanayohubiri.

Kwa mfano, wanashindwa nini kukiri ukweli kuhusu ushiriki wao katika mgogoro wa kisiasa Zanzibar, wakaamua kuumaliza mara moja na kurejesha amani?

Ndiyo, inaweza ikawanyima baadhi yao ulaji ndani ya chama; lakini itajenga imani kwa umma na amani kwa taifa. Umoja utaimarika.

Wanafurahia nini kuongoza Zanzibar iliyogawanyika hivi? Hata wakisingizia ‘sababu za kihistoria,’ wenye akili watawahoji: mmekosa akili za kuondoa sababu hizo za kihistoria? Au mmependa kuendeleza urithi huo wa kihistoria?

Kama Rais Kikwete angekuwa mkweli na makini katika hili, Rais Karume na kundi lake wangenuna, lakini Zanzibar ingeimarika. Hata hivyo, wangefika mahali wakatulia maana wanajua kwamba madaraka yenyewe waliyo nayo waliyapata kwa ujanja.

Na wangeheshimika kwa kukiri makosa ya ujanja huo na kuweka misingi imara ya uongozi wa Zanzibar baada ya kustaafu kwao.

Lakini sasa tuna uhakika gani kwamba mrithi wa Kikwete ndiye atakayeweza? Kwanini naye asijifunze mbinu ya mtangulizi wake ya kuahirisha?

Na kwa nini tusione kwamba mbinu hii inachochea zaidi migogoro kwa sababu wananchi hawa hawa wasiotilia shaka nia yake kwa sasa ndio watakuwa wakali siku waking’amua janja ya wakubwa?

Kwa nini CCM inashindwa kuwaumiza wachache kwa ajili ya mustakabali wa taifa zima? Upo wapi ujasiri wa uongozi tulioahidiwa? Ipo wapi Tanzania yenye amani na umoja usiotetereka?

Sitashangaa; kwa kutoona mbali, watawala wanaweza kudhani kwamba sisi tunaojadili masuala haya tunachochea wananchi na kuhatarisha amani. Ndivyo walivyozoea. Lakini wataona umuhimu wetu pale tu watakapoamua kufikiri kwa kina, wakachunguza dhamiri zao na kutazama mbali ya pua zao.

Ni vema wajue kama tunavyojua sisi kuwa Tanzania haiishii kwenye madaraka na mamlaka yao. Wala haikomei pale walipo. Tuna amani leo kwa sababu kuna wachache waliumia huko nyuma.

Na tunahatarisha amani ya nchi miaka 50 ijayo kwa sababu tunaogopa kuumia leo kwa ajili ya waungwana wengi.

Leo Waislamu wanapozana na kushauriana ‘waipe muda’ serikali itoe uamuzi kuhusu suala linalowahusu. Wanaambizana kwa upole kwa sababu bado wana imani kiasi na nia ya serikali.

Kushauriana na kupozana huku hakutakuwapo tena siku wakigundua janja inayotumika kuahirisha suala nyeti lililotumika kama kete ya kuwaomba kura mwaka 2005.

Tulishawashauri serikali kuhusu jambo hili. Wao ndio wana uamuzi wa mwisho. Lakini nawahakikishia. Wanaweza kupuuza la Mwafaka wa Zanzibar, wakaliahirisha hadi baada ya 2010.

Hili la Kadhi Mkuu lina mvuto na mguso wake kwa wanaolitaka na wanaolipinga; wanaohusika na wasiohusika. Wakubwa wasipojihadhari litawasumbua na litawatafuna kabla ya Oktoba 2010.



juu