HABARI MPYA LA JANA MATANGAZO BEI ZETU WASILIANA NASI TUMA HABARI
jumapili, 22 machi 2009
Yaliyopita
Pekua Tovuti
Wasiliana na Mwandishi
+447984584292
ansbertn@yahoo.comTuma barua-pepe
www.ngurumo.blogspot.comTembelea blogu
Watawala wanaandaa magaidi

Ansbert Ngurumo

 

MBINU za watawala na mifumo wanayoitumia vimegeuka vitalu vya kuzalishia magaidi. Si magaidi wa kujilipua kwa mabomu bali wanaharakati waliokata tamaa na wasio na imani tena katika mfumo wa kidemokrasia unaosimamiwa na watawala hawa hawa.

Wanatafuta njia ya mkato na ya haraka ya kupata kile ambacho kimezingirwa na mabavu ya watawala. Heri watawala wa Afrika wangeshtuka sasa, wakajua kuwa wananchi wamebaki na imani kidogo sana katika siasa za masanduku ya kura.

Katika zama ambapo tulikuwa tunapaswa kukomaa kidemokrasia na kusahau mageuzi ya kisiasa yanayoshirikisha nguvu za kijeshi zilizodumaza bara letu kwa miongo kadhaa, watawala wa sasa wanaonekana kudhamiria kuturejesha huko kwa sababu moja tu; hawataki kukua na kukomaa!

Taratibu, baadhi ya makundi ya wanaharakati na wanasiasa wanaanza kuzoea kuwa dhana ya mapinduzi ndiyo njia mbadala ya kuwaondoa watawala mafisadi, wazembe na wababe walioziba masikio yao wasisikie sauti ya umma.

Pole pole, wananchi (hasa katika nchi zisizo na historia ya kupinduana) wanaanza kukusanya kumbukumbu na kujiridhisha kwamba si kila mapinduzi ni mabaya. Wana orodha ndefu ya nchi za Kiafrika zinazojivunia utawala wa ‘kidemokrasia’ uliotokana na mapinduzi ya kijeshi.

Bahati mbaya ni kwamba Tanzania ni nchi mojawapo inayotoa mfano huo ‘mbaya’ kwa wengine ambao wanaitazama nchi yetu kutokea Zanzibar.

Nakumbuka katika makala yangu ya Agosti 12, 2007, nilijadili kiini cha Mapinduzi ya Zanzibar na msingi wa kauli mbiu ya ‘Mapinduzi Daima’ ambayo imeendelea kutumika Zanzibar kama kibwagizo cha kisiasa.

Nilisisitiza kwamba Wazanzibari waliamua kupindua utawala uliokuwapo wa Sultan Jamshid ibn Abdullah kwa sababu waligundua kwamba njia za kidemokrasia zimeshavurugwa na watawala hao hao. Walichoka kuona watawala wanashindwa kwa kura lakini wanapata madaraka kwa ujanja.

Kwa wale ambao hawakusoma makala hiyo, au wale waliosahau au wanaotaka kujikumbusha kwa kifupi, niliandika hivi:

‘Walau tukianzia uchaguzi wa Juni 1957, utaona kwamba ASP kilifanyiwa dhuluma nyingi na watawala, kikawa kinashinda na kunyimwa madaraka. Juni 1957 kilishinda kwa asilimia 61.14 dhidi ya 21 za Zanzibar Nationalist Party (ZNP) na asilimia 16.89 za Muslim Association (MA). Watawala wakasema, ‘mtashinda nyie, tutatawala sisi.’

Kikavuta subira na kurejea ulingoni Januari 1961. Kikashinda tena; zamu hii kwa asilimia 43.19 dhidi ya asilimia 38.52 za ZNP na 18.29 za Zanzibar and Pemba People’s Party (ZPPP).

Wakasema tena ‘shindeni nyie, tutatawala sisi.’ Ukazuka mgogoro hadi kukalazimika kufanyika uchaguzi mwingine Juni 1961. ASP kikashinda tena kwa asilimia 49.39 kikiwa na viti 13 kati ya 23. ZNP kikapata asilimia 35.50 ya kura zote, na viti 10; ZPPP kikapata asilimia 13.89 ya kura zote, na viti 3. Bado ASP ikafanyiwa mizengwe na kushindwa kutawala kwa sababu ZNP iliungana na ZPPP kuunda serikali ya mseto ili kukinyima fursa ASP.

Hali hiyo ilijirudia Julai 1963 ambapo ASP kilishinda viti 13, dhidi ya 12 vya ZNP na sita (6) vya ZPPP, lakini kikanyimwa tena fursa ya kuunda serikali kwa ujanja ule ule. Ndipo kikagundua kwamba kwa staili hii ya kuingia kwenye uchaguzi, kushinda na kunyimwa fursa, kisingeweza kutawala kamwe.

Hiki ndicho kiini cha mapinduzi ya Zanzibar dhidi ya Sultani Jamshid ibn Abdullah.

‘Mapinduzi Daima’ wanayoimba wana CCM, yana asili yake katika kukataa kutawaliwa na watu walioshindwa. Lakini sasa wameyageuza kuwa silaha ya kutawala hata kwa kulazimisha. Rejea uchaguzi wa 1995, 2000 na 2005.’

Hili ni somo kutoka ASP, urithi wa CCM, jeuri ya Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar. Wanaokerwa na dhana hii ya mapinduzi wamekuwa wanakerwa pia na jina hilo la serikali. Wamekuwa wanashauri iitwe Serikali ya Zanzibar.

Watawala hawataki kusikia wala kukubaliana na hoja hii kwa vile inatolewa na wapinzani wao. Wanajivunia na kudumisha dhana ya mapinduzi huku wakisisitiza utawala wa kidemokrasia.

Nimeyakumbuka mapinduzi haya kwa sababu kuu mbili. Kwanza, ndani ya miezi minne iliyopita Afrika imeshuhudia mapinduzi katika nchi za Guinea (Desemba 2008) na Madagascar (Machi 2009).

Pili, watawala wa Afrika kupitia umoja wao (AU), wakiungwa mkono na Umoja wa Ulaya, Marekani na Ufaransa, wamekemea na kulaani mapinduzi hayo. Sababu kubwa inayotolewa na wanaolaani mapinduzi hayo ni kuwa ‘demokrasia imepuuzwa katika kuondoa utawala uliokuwapo.’

AU imekwenda mbali na kukataa kutambua utawala mpya wa Madagascar, huku nchi nyingine zikitamka kuitenga na hata kuiwekea vikwazo vya kiuchumi.

Kila mtu anayefuatilia masuala ya kidiplomasia duniani anaelewa kiini cha msimamo huu na mantiki yake. Ni jitihada njema tu za kuiepusha dunia na mabalaa yawezayo kutokana na mapinduzi ya kijeshi.

Ni jiitihada za makusudi za kuwarejesha wananchi, wanasiasa na wadau wote katika kuzingatia misingi ya kidemokrasia na utawala bora. Ni jitihada takatifu.

Nakubaliana na watawala hawa katika dhamira yao ya kusimika misingi ya demokrasia. Lakini sikubaliani nao katika jambo moja - maana na mifumo ya demokrasia wanayoisimika katika nchi zao.

Siamini kwamba demokrasia ni kufanya uchaguzi tu. Na siamini kwamba uchaguzi ni kupiga kura tu. Zaidi ya hayo, siamini kwamba nchi zetu zinaongozwa kidemokrasia.

Sana sana watawala wetu ndio wanaovunja misingi ya kidemokrasia na kuwafungia wengine milango; wanalazimisha wananchi kutafuta mbinu mbadala, na hata kurejea mbinu kongwe kama hizi za kupinduana.

Tuna mifano mingi, lakini tuanzie kwetu; tutazame mabavu na hila za watawala katika mchakato wa uchaguzi wa Zanzibar 1995, 2000 na 2005. Kama hii ndiyo demokrasia ambayo watawala wanaitetea, tutakubaliana kwamba hawajui wanachotetea, na kwamba kwa mabavu hayo wanandaa magaidi.

Tuwe wakweli. Nguvu kubwa ya kijeshi inayotumika katika chaguzi zetu hizi, ni sawa na ugaidi wa dola dhidi ya umma. Inaufanyaje uchaguzi kama ule na matokeo yake visiwe sawa na mapinduzi ya kijeshi?

Tuliona kilichotokea Kenya katika uchaguzi wa 2007. Hadi leo tunajua kwamba mshindi hakutawala. Chaguo la wananchi lilitupwa na wenye dola waandaaji na wasimamizi wa mfumo wa uchaguzi. Majeshi yalitumika kukamilisha wizi wa madaraka.

Ushindi wa Rais Mwai Kibaki unatupatia funzo gani la kidemokrasia? Ni nani anaweza kuitamani demokrasia ya aina hiyo? Na kama hiyo inaitwa demokrasia, iko wapi tofauti yake na mapinduzi ya kijeshi?

Na kama hii ndiyo demokrasia tunayowafunza wananchi na vyombo vya dola, tutayalaani majeshi hayo siku yakiamua kutumia ‘demokrasia’ hiyo kuwasikiliza wananchi na kuwaondoa watawala wale wale?

Twende Zimbabwe. Tulishuhudia yaliyotokea katika uchaguzi wa mwaka jana (2008); na majeshi yakijiapiza kuwa kama si Robert Mugabe hayako tayari kuona mshindi mwingine akiingia Ikulu. Tulishuhudia vitisho vilivyotumika kuvuruga uchaguzi hadi Mugabe akagombea tena bila mshindani na akatangazwa mshindi!

Na tunajua kuwa wanajeshi wanaosema haya ni wale wakubwa walioshiba pamoja na watawala; si vijana wa kazi, wapambanaji wanaopigika, wasio na kiinua mgongo cha kutegemewa.

Ushindi wa Mugabe una tofauti gani na mapinduzi ya kijeshi? Ni halali watawala kupindua umma lakini umma usiwapindue ukipata upenyo?

Kwa mantiki ya demokrasia kama utawala wa watu, utokanao na watu kwa ajili ya watu, kuna la kujivunia katika mazingira haya ya uchaguzi, ushindi na utawala wa kihuni?

Wananchi wana haki ya kugomea watawala waliopatikana kwa misingi hii. Wana haki ya kutowatambua, kuwasumbua na kuwapindua.

Watawala wanaopatikana kwa kunajisi demokrasia hawapaswi kutuhutubia juu ya uzuri wa demokrasia. Hawa nao wanastahili kutengwa na kuwekewa vikwazo.

Ni aibu kama Umoja wa Afrika unawaheshimu na kuwatukuza akina Muammar Gadhafi (aliyepindua na kukaa madarakani kwa miaka 40 sasa), Paul Kagame (aliyeingia baada ya umwagaji damu uliokithiri na amekaa madarakani kwa zaidi ya muongo mmoja), Joseph Kabila (aliyeingia kwa mapinduzi yaliyomuingiza na kumuondoa baba yake na amekaa madarakani kwa takribani muongo mmoja sasa) na Yoweri Museveni (aliyeingia madarakani kwa mtutu na sasa anazeekea Ikulu kwa ushindi wenye utata kila uchaguzi), lakini umoja huo huo unashindwa kutambua harakati za wananchi wa Madagascar chini ya kiongozi wao Andry Rajoelina.

Hata kama baadhi yao wameshaweka mazingira mapya na mifumo mipya ya utawala katika nchi zao, waliingia kwa mitutu kama huyu huyu anayewekewa vikwazo; ambaye naye sasa anaandaa mazingira ya ‘uchaguzi huru’ kama wao.

Ikumbukwe kuwa mapinduzi ya Madagascar yamefanywa na wananchi dhidi ya uongozi ulioshinda kwa kura lakini ukashindwa kutawala.

Nguvu ya kijeshi imetumika kuunga mkono jitihada za wananchi na kudhihirisha uasi wao dhidi ya watawala. Hiki ndicho kinawauma wakubwa, maana wanahisi kuwa kama yametokea kwingine yanaweza kutokea kwao.

Viongozi wengi wa Afrika ni watawala walioshindwa kazi lakini wanaweza kudumu madarakani kwa kuwa wana vyombo vya dola vinavyotumika kuwatisha wananchi.

Ni vema tuelewane hapa. Harakati zozote za kubomoa misingi ya kidemokrasia zinapaswa zikemewe. Lakini kukemea huko hakutakuwa na maana kama hatujengi misingi ya demokrasia inayosimama katika haki na utawala bora.

Tutazame mbele zaidi. Watawala wa Afrika ndio wanaojenga mazingira ya kuchukiwa, kugomewa, kupuuzwa, kusumbuliwa na hata kupinduliwa.

Watawala wetu ndio wanaojenga mazingira ya kuidharaulisha demokrasia. Wao hawaiheshimu, na wanatumia mabavu kupata watakacho, hata kama wananchi wamefanya uamuzi tofauti.

Wamejenga na kusuka mifumo ya uchaguzi ambayo haiweki mazingira sawa ya ushindani. Hapa hakuna demokrasia.

Na chochote kinachoingia madarakani kwa misingi hii ni kichafu, na kinaweza kuondolewa kwa misingi yoyote itakayokubalika na wale wanaokiondoa.

Na hata kama uongozi umechaguliwa kidemokrasia, ukifika mahali ukashindwa kutimiza wajibu wake, wananchi wakataka kuwajibisha watawala nao wakatunisha misuli na kuendekeza dharau, tusiwalaumu wananchi watakapoamua kuitokomeza misingi mibovu ya demokrasia.

Na hili si tatizo la Afrika tu. Septemba 2006, jeshi lilimpindua aliyekuwa Waziri Mkuu wa Thailand, Thaksin Shinawatra. Liliingilia kati baada ya mgogoro mkubwa wa kisiasa uliodumu kwa mwaka mzima kutokana na ufisadi uliokithiri wa kiongozi huyo.

Na ulikuwa umebaki mwezi mmoja kabla ya uchaguzi mwingine ambao walijua tu kuwa ungetumika kuhalalisha utawala mbovu, kuidhalilisha demokrasia na kudumisha ufisadi. Wakamtimua. Sasa hivi anajibu mashtaka ya ufisadi.

Binafsi, supendi tufike mahali pa kupinduana kijeshi. Lakini utashi wangu hauwezi kuzuia mapinduzi kama watawala wenyewe wanajiandaa kupinduliwa.

Niliwahi kuonya huko nyuma - na nitaonya tena – kwamba Afrika yetu ikiendekeza uongozi huu wa ushindi wa kulazimisha, wizi wa kura na kejeli dhidi ya wanaotoa mawazo mbadala, inakaribisha tena miongo kadhaa ya balaa ya mapinduzi ya kijeshi.

Tujifunze katika historia ya mapinduzi ya kijeshi, walau katika Afrika huru. Togo (1963, 1967); Algeria (1965); Congo (1961, 1997, 2000); Sudan (tangu 1964); Nigeria (kwa muda mrefu tangu 1966); Afrika ya Kati (1966); Ghana (1966), Libya (1969); Rwanda (1976 na 1994); Uganda (1971, 1986) na nyingine.

Na tusisahau kwamba Zanzibar yetu imekuwa mfano wa kuigwa kwa wengine; maana kati ya mapinduzi yanayosifiwa na yaliyodumu kwa muda mrefu hapa Afrika ni ya Libya (1969) na ya Zanzibar (1964).

Watawala wetu wanapotoa kauli dhidi ya utawala mpya wa Madagascar si kwamba wanakerwa kwa dhati na dhana ya mapinduzi. Ni kwamba wanaogopa nguvu ya umma inayoanza kuwazunguka na kutoroka mifumo yao ya uchaguzi.

Wanahisi kwamba zamu yao haipo mbali, na iwapo watakaa kimya, haya yakiwafika watakosa mtetezi.

Kama kweli wangekuwa na uwezo na uadilifu wa kutosha kukemea watawala wenzao, wangeanza na Kibaki na Mugabe; wangewatenga hao kwanza.

Na wasingeona kwamba demokrasia ya Zanzibar, Kenya, Zimbabwe, Libya, Rwanda, Uganda na Jamhuri ya Kidemokrasi ya Congo ni bora kuliko ya Madagascar.

Najua kila mapinduzi yana tofauti na mengine, na yana msukumo tofauti; hivyo yangestahili kupatiwa maelezo tofauti. Lakini msingi wa yote ni wakubwa kujisahau, kulewa madaraka, kushindwa kazi waliyoomba na kupuuza sauti ya umma.

Mapinduzi ni njia ya waliokata tamaa, ambao hata dhana yenyewe ya demokrasia haina maana tena kwao. Na yana gharama kubwa ambayo wakati mwingine inalipwa na wasiohusika.

Lakini naona kama mienendo ya kibabe ya viongozi wa sasa wa Afrika inajenga makundi ya magaidi na inakaribisha mapinduzi.

Huyo wanayemtenga leo hana jipya; anarudia historia ya mchoko wa kisiasa, na ipo siku watamkubali katika klabu ile ile ya kina Museveni, Kagame na Gadhafi.

Na kwa sababu ameshaanza, naye anaweza kupinduliwa hata kesho. Lakini ana kosa gani kubwa kuliko hao wanaomlaani na kumtenga?



juu