HABARI MPYA LA JANA MATANGAZO BEI ZETU WASILIANA NASI TUMA HABARI
jumatatu, 28 mei 2012
Yaliyopita
Pekua Tovuti

DC adaiwa kudhalilisha Kanisa


na Mwandishi wetu, Tarime

 

MCHUNGAJI wa Kanisa la Pentecostal Evangelistic Fellowship Africa (PEFA), Kijiji cha Kewanja wilayani Tarime, Mkoa wa Mara, Elia Magutu, amewataka viongozi wa serikali kuwa na kauli za busara wakati wanapowahutubia wananchi kwenye mikutano ya hadhara.

Kauli hiyo imekuja baada ya mchungaji huyo kudai kwamba, Mkuu wa Wilaya (DC) ya Tarime, John Henjewele akiwahutubia wanakijiji wa Kewanja, alilikashifu kanisa hilo na kusema halipo kihalali.

Henjewele alidai lengo la kuanzishwa kwa kanisa hilo ni kutaka lijumuishwe na kufanyiwa tathimini ya malipo katika zoezi la kuwahamisha wakazi wa Kitongoji cha Gonsarara wanaozunguka mgodi wa dhahabu wa North Mara linalofanywa na kampuni hiyo.

“Ilikuwa Mei 3 mwaka huu mkuu wa wilaya hii akiwa katika mkutano wa hadhara Gonsarara, alisema kuna kanisa limeibuka la kitapeli lisilojulikana…limetegeshwa ili nalo lifanyiwe tathimini ya malipo.

“Kauli hiyo ilitushangaza kwa sababu katika hicho kitongoji kuna kanisa moja tu ambalo ni la PEFA, hivyo alikuwa anatulenga sisi,” alisema Magutu na kukanusha madai ya mkuu huyo wa wilaya na kusema kanisa hilo lipo tangu mwaka 1996 na kwamba kauli hiyo ya Henjewele ina lengo la kulidhalilisha kanisa.

“Hili kanisa halijajengwa leo, limeanzishwa mwaka 1996 wakati huo tukiwa tunasali shuleni Nyabigena-Kewanja, ilipofika mwaka 2002 tukanunua eneo Gonsarara tukajenga nyumba ya nyasi kulingana na uwezo tuliokuwa nao, wakati huo tukaendelea kusali tukiongozwa na mzee Dishon Ghati.

“Baadae tukajenga nyumba ya bati na sasa tunaendelea na ukarabati, hadi sasa kanisa linao waumini zaidi ya 100,” alisema mchungaji huyo huku akimtaka mkuu huyo wa wilaya kuliomba radhi kanisa la PEFA.

Mwenyekiti wa kanisa hilo wilayani hapa, Mchungaji Samson Msabi alithibitisha kuwepo kwa kanisa hilo lililowekwa wakfu mwaka 2008.

Kwa upande wake, Henjewele alikiri kuwepo kwa kanisa alilodai kutofahamu jina lake, na kusisitiza kwamba si kanisa halali, limeibuka na kutegeshwa kwa lengo la kufanyiwa tathimini na mgodi huo.



juu