HABARI MPYA LA JANA MATANGAZO BEI ZETU WASILIANA NASI TUMA HABARI
jumatatu, 28 mei 2012
Yaliyopita
Pekua Tovuti

Mapigano ya wakulima, wafugaji yanukia Morogoro


na Joseph Malembeka, Morogoro

 

WAKULIMA Patrick Sengyumva (17) na Moses Melama wa Kijiji cha Mbwade, Kata ya Bwakila chini wilayani hapa, wamenusurika kufa baada ya kupigwa na wafugaji jamii ya kimasai wakidaiwa kuzuia ng’ombe kuingia kwenye shamba la alizeti.

Kwa nyakati tofauti, wakulima hao waliwaeleza waandishi wa habari kwamba, vitendo hivyo vimeanza kuzoeleka hali waliyoonya kwamba inaweza kuanzisha machafuko.

Akisimulia mkasa uliomkuta, Sengyumva alisema: “Ilikuwa Mei 14 mwaka huu kwenye saa nne hivi, mfugaji Saning’a Lekweta alileta ng’ombe wake shambani kwetu… nilipowaona nikawauliza kwanini wanaingiza kwenye shamba lenye mazao, akasema wamepewa na uongozi.”

Kwa mujibu wa mkulima huyo baada ya majibu hayo, mfugaji alimsogelea na kuanza kumpiga kwa fimbo na rungu alilokuwa nalo hali iliyomsababishia kupoteza fahamu na maumivu makali kabla ya kuokolewa na mwanakijiji aliyepita eneo hilo kisha kupelekwa Kituo cha Afya Duthumi kwa matibabu.

Wakati Sengyumva akisema hayo, mkulima mwenzake, Melama alidai kunusurika kifo cha aina hiyo Aprili 18 mwaka huu ambapo mfugaji huyo alikamatwa na kufikishwa Kituo cha Polisi Kisaki na kuwekwa rumande kwa muda mfupi kabla ya kuachiwa huru.

Ofisa Mtendaji wa Kijiji cha Mbwade, Fakina Matosa alikiri kupokea kesi hiyo na kusema Kamati ya Ulinzi na Usalama ya kijiji inalitafutia ufumbuzi tatizo hilo na kuepusha migogoro baina ya wakulima na wafugaji.



juu