KATIKATI ya vuguvugu la mabadiliko ya kisiasa hapa Tanzania, ambalo kwa sasa ni dhahiri, jambo mojawapo ambalo linafurahisha kutoka kwa wapinzani, ni harakati zao za kukiweka chama katika mikono ya wananchi. Kitendo cha kukusanya mchango kidogo kidogo, lakini kutoka kwa wafuasi wengi, ni jambo la maana sana.
Mtaalamu mmoja wa saikolojia alipotembelea jumuiya ya wanafunzi, na akataka kuwasaidia waliokuwa na hitaji la huduma yake, aliwaambia kwamba lazima wachangie kidogo huduma yake. Akasema wazi kwamba, anajua yeye ni tajiri kwa kuwa kazi hiyo inamlipa sana huko kwao Amerika, na akasema anajua pengo la kiuchumi baina yake na wanafunzi wale. Lakini akasema lazima wachangie.
Kwa nini wachangie? “Nikitoa bure kabisa huduma hii, wateja wangu wanaweza wasichukulie kwa uzito unaostahili huduma hii. Wanaweza wakafikiri ni porojo tu”. Kwa kuchangia, japo kidogo, mtu hujiona kwamba ameshiriki katika kazi ya maana.
Kadhalika katika kazi ya kisiasa. Haidhuru, hata kama chama kina wafadili wakubwa, haina maana kuwaacha wengine wengi wasichangie, na wakaachwa wale wakubwa tu. Watu lazima wajione kwamba kuwezesha kazi za siasa, ni kazi yao. Naamini kuwa, viongozi wa upinzani kwa vyovyote wanafahamu kuwa, kwa tendo lao jema la kuwashirikisha wananchi katika uenezi wa mabadiliko, yaani kuwashirikisha kiuchumi, katika kuchangia chama, wananchi watakuwa na uchungu zaidi na chama chao, lakini pia wajue ni changamoto kubwa ya kuhakikisha wanajiongezea wajibu kwa watu waliochangia chama.
Tena kuna sababu nyingine ya maana katika zoezi hili la kuwashirikisha wanachama wa kawaida katika kuchangia chama. Baadhi yetu huenda tunasubiri tu muujiza wa kuwa matajiri utokee, pale nchi itakapotawaliwa na hawa walio wapinzani kwa sasa. Sasa wananchi wanafundishwa kuchangia, ni namna pia ya kuwaandaa baadaye wajue kuwa, pamoja na hitaji la uongozi mbadala, uongozi huo bado utahitaji mchango wa wananchi wake.
Watu wajue kwamba, kutoka kwa viongozi wapya, si kwamba kitakuja chakula cha bure, au elimu ya bure, au makazi ya bure. Bali kutokana na viongozi wasio wezi, na viongozi wenye dira, nguvukazi ya wananchi haitapotea bure. Haidhuru, huko mbele ya safari, kulingana na utajiri wa maliasili tulionao, na ikiwa itasimamiwa vema, ni wazi gharama za maisha zaweza kushuka, na hata serikali ikawa na mapato ya kuwezesha watu wake katika mambo mengi, na hata kuweza kuwapa ruzuku.
Na kwa kweli ruzuku hiyo, itakuwa imetoka kwa wanachi wenyewe, pato la kazi ya mikono yao itawarudia. Haya yamefanyika katika nchi nyingi, na hakuna sababu kwamba hapa haiwezekani. Lakini pamoja na hayo daima heshima ya mtu ni kazi. “kazi yako ndio jina lako”.
Kwa hiyo, ni vizuri wananchi pia wakaelimishwa kuwa kazi hiyo njema waliyoianza, itatakiwa kuendelea hata baada ya lengo lao (la kushika dola) kutimia.
Na kwa maono yangu, wanachokifanya wapinzani wakuu kwa sasa, ni kufukua kile chema ambacho kilifanywa na Mwalimu Julius Kambarage Nyerere, lakini kikafukiwa na viongozi wabinafsi, ambao hawakutaka nchi iwe ya kila mtu. Ile alama ya jembe na nyundo bado inaakisi kile alichokusudia mwalimu?
Kuna kitu kilichokuwa kinaitwa matembezi ya mshikamano, (sijui kama bado yapo, na kama bado yapo, sijui kama yanabeba maana ile ile ya zamani.) Matembezi haya, pamoja na mapungufu ambayo labda yalikuwepo, yalikuwa ni namna ya kuwaonyesha wananchi kwamba chama ni chao.
Uzuri wa chama tawala unapotea, kwa sababu watu wamenyang’anywa chama chao. Kwamba matajiri ndio wanachangia kisha msimu wa uchaguzi maskini wanahongwa kwa hali dhalili kabisa, ni namna ya kuwaambia wananchi kuwa hicho chama si chao.