SERIKALI imeanzisha mradi wa ujenzi wa daraja la Mbutu lenye ukubwa wa kilometa tano ambalo litajengwa na makandarasi wazalendo.
Hayo yalisemwa jana jijini Dar es Salaam na Waziri wa Ujenzi, John Magufuli, wakati akifungua mkutano wa mwaka wa mashauriano wa makandarasi.
Alisema mradi wa daraja hilo litakalokuwa na madaraja madogo madogo saba, utagharimu sh bilioni 13 na kwamba makampuni 13 ndiyo yaliyopewa kazi hiyo.
Alisema tayari makampuni hayo yameshalipwa fedha za awali kwa ajili ya kuanza shughuli hiyo na kwamba huo utakuwa mwanzo wa uwakilishi mzuri wa makandarasi wazalendo kufanya kazi hiyo kwa pamoja.
Aliwataka kufanya kazi kwa kuungana pamoja na kwa kufuata maadili bila kuoneana wivu na hivyo serikali haitasita kuwasaidia.
Pamoja na mambo mengine Waziri Magufuli alisema mchakato wa ujenzi wa daraja la Kigamboni umeshakamilika na utaanza wakati wowote.
Alisema tayari mkandarasi ameshamaliza upembuzi yakinifu na ujenzi utakaogharimu sh bilioni 240.
Naye Mwenyekiti wa Bodi ya Makandarasi (CRB), Consolata Ngimbwa, alieleza changamoto ambazo bodi yake inakumbana nazo kuwa ni upatikanaji wa zabuni kwa makandarasi katika halmashauri kutokana na kugubikwa na rushwa.