HABARI MPYA LA JANA MATANGAZO BEI ZETU WASILIANA NASI TUMA HABARI
ijumaa, 8 juni 2012
Yaliyopita
Pekua Tovuti

Ilala kuanzisha TIKA


na Irene Mark

 

MANISPAA ya Ilala jijini Dar es Salaam imeahidi kuharakisha upitishwaji wa sheria ndogo na hati rasmi kwa ajili ya kuanzisha utaratibu wa Tiba kwa Kadi (TIKA) ili kuboresha huduma ya afya kwa wakazi wake.

Akizungumza wakati wa mafunzo ya mchakato wa uanzishwaji wa TIKA kwa madiwani wa manispaa hiyo yaliyotolewa na Mfuko wa Taifa wa Bima ya Afya (NHIF), wenye dhamana ya kusimamia Mfuko wa Afya ya Jamii (CHF), Mstahiki Meya wa Ilala, Jerry Slaa, alieleza umuhimu wa afya kwa ustawi wa jamii bora.

Alisema kuwa suala la matibabu limetekwa na wafanyabiashara wanaotaka kuifanya afya kuwa biashara na kwamba pasipo kuwa na umakini gharama za matibabu zitapanda kila kukicha kwa visingizio mbalimbali.

“Wanapojitokeza wadau kama NHIF kusaidia suala hili hatuna budi kuwaunga mkono na kushirikiana nao katika hatua hii muhimu ili utaratibu huu uanze mara moja, tiba kwa kadi ndiyo mtindo wa kisasa,” alisema Slaa.

Kuhusu faida za TIKA, alisema inawashirikisha wananchi kwenye usimamizi wa huduma za matibabu na kumaliza tatizo la rushwa katika vituo vya huduma za afya hususan kwa wagonjwa wa malipo ya papo kwa papo.

Naibu Mkurugenzi Mkuu wa HNF, Hamis Mdee, alisema umuhimu wa TIKA ni kumaliza changamoto za upatikanaji wa rasilimali fedha katika utoaji wa huduma kwa wananchi na uhakika wa matibabu kwa wakazi wa Ilala.

“Huu ni mpango wa hiyari unaohitaji uwajibikaji… wanufaika wa mradi huu ni wanafamilia ambao kila mmoja huchangia kiasi fulani cha pesa mara moja kwa mwaka kisha anapata huduma za matibabu mwaka mzima,” alisema Mdee.



juu