HABARI MPYA LA JANA MATANGAZO BEI ZETU WASILIANA NASI TUMA HABARI
ijumaa, 8 juni 2012
Yaliyopita
Pekua Tovuti

IGP Mwema aimarisha polisi jamii


na Said Kopwe, Manyara

 

MKUU wa Jeshi la Polisi Tanzania, Inspekta Jenerali (IGP), Said Mwema katika kutekeza mpango wa Polisi Jamii na Ulinzi Shirikishi amewahamishia wakaguzi wasaidizi wa jeshi hilo katika kila tarafa nchini kwa ajili ya kusimamia programu hiyo.

Katika programu hiyo, pia vimeanzishwa vikundi vya ulinzi kwa kuwashirikisha raia wa kila mtaa, ili kulisaidia jeshi hilo kupambana na uhalifu nchini.

Aidha, IGP Mwema mwanzoni mwa wiki hii, amewatuma wasaidizi wake kwenda mikoani kukagua kila kata, ili kujua maendeleo na changamoto zinazokabili programu hiyo.

Mkoani Manyara, Kamishna Msaidizi Mwandamizi wa Polisi (SACP), Basilio Mathei, ambaye ni Mkuu wa Kitengo cha Polisi Jamii Makao Makuu ya Polisi Tanzania, alipokea taarifa kutoka kwa kikundi cha ulinzi shirikishi cha Kata ya Bagara, wilayani Babati, ambako kikundi hicho kilishukuru ushirikiano mkubwa unaooneshwa na Mkuu wa Polisi wa wilaya hiyo, Mrakibu Msaidizi Mwandamizi wa Polisi (SSP), Mussa Taibu, pamoja na askari wa kata hiyo, PC Ombeni na WP Grace.

Walisema kwa ushirikiano huo, wameweza kudhibiti uhalifu na hata kuwafikisha mahakamani watuhumiwa wa mitaa ya Oysterbay, Ngarenaro na wengine kuhukumiwa miaka 10 jela.

Mbali na hilo, vikundi kutoka Wilaya ya Kateshi vilieleza changamoto mbalimbali wanazokabiliana nazo kama ukosefu wa vifaa vya ulinzi, zikiwamo tochi, makoti na filimbi kwa ajili ya kujulishana wanapokutana na wahalifu nyakati za usiku.

Akijibu changomoto hizo, Kamanda Basilio, alisema hadi sasa hakuna bajeti iliyotengwa kwa ajili ya vikundi hivyo, isipokuwa wanatakiwa kuchangishana mtaa kwa mtaa ili kujiwezesha katika mahitaji hayo, kwani suala la ulinzi ni la wote.



juu