HABARI MPYA LA JANA MATANGAZO BEI ZETU WASILIANA NASI TUMA HABARI
jumanne, 12 juni 2012
Yaliyopita
Pekua Tovuti

Tanzania yamwomboleza Saitoti


na Hellen Ngoromera

 

TANZANIA imeeleza kushtushwa na kifo cha Waziri wa Usalama wa Ndani wa Kenya, Prof George Saitoti, na naibu wake, Orwa Ojode.

Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa, Bernard Membe, alieleza hayo jana katika viwanja vya Ikulu jijini Dar es Salaam baada ya kumalizika kwa hafla ya kuapishwa kwa mabalozi, akisema kuwa serikali imeshtushwa na vifo hivyo kwani Saitoti alikuwa mashuhuri na mwenye busara.

“Kwa niaba ya Watanzania napenda kutoa pole kwa serikali ya Kenya kufuatia vifo hivyo kwani hata Afrika Mashariki kwa ujumla imepoteza mwanasiasa mashuhuri, Saitoti alikuwa ni mtu mwenye akili na busara,” alisema Membe.

Akimwelezea zaidi Saitoti, waziri huyo alisema aliwahi kufanya naye kazi kwa karibu mwaka 2011 baada ya kuteuliwa kuwa Kaimu Waziri wa Mambo ya Nchi za Nje wa Kenya, walipokutana naye mara kwa mara hasa kwenye mikutano.

Viongozi hao walifariki katika ajali ya ndege juzi baada ya kuondoka na kuteketea kwa helikopta ya polisi waliyokuwa wakisafiria kuelekea eneo la Sotik kwa mkutano usalama.

Katika hatua nyingine, Rais Jakaya Kikwete, amewaaapisha wakurugenzi wapya wa Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa ambao pia watakuwa na hadhi ya kibalozi.

Walioapishwa ni Vincent Kibwana ambaye amekuwa mkurugenzi Idara ya Afrika, Naimi Aziz, mkurugenzi Idara ya Ushirikiano wa Kikanda, Balozi Celestine Mushy ambaye anakuwa mkurugenzi, Idara ya Ushirikiano wa Kimataifa.

Wengine ni balozi Yahya Simba ambaye amekuwa mkurugenzi Idara ya Mashariki ya Kati, Bertha Somi anayekuwa mkurugenzi Idara ya Diaspora, Irene Kasyanju, mkurugenzi Kitengo cha Sheria, Dorah Msechu anayekuwa mkurugenzi Idara ya Ulaya na Amerika.

Pia wapo Balozi Mbelwa Kairuki anayekuwa mkurugenzi Idara ya Asia na Australia na Silima Haji ambaye ameteuliwa kuwa Mkurugenzi Idara ya Mambo ya Nje, Zanzibar.



juu