WANANCHI wilayani hapa, mkoani Manyara, wamehakikishiwa kuondolewa tatizo la migogoro sugu ya ardhi inayoendelea kati ya wakulima na wafugaji.
Kauli hiyo ilitolewa na Mkuu wa Wilaya, Christine Mndeme hivi karibuni kwenye ziara iliyoandaliwa na Mbunge wa Hanang’, Dk. Mary Nagu alipotembelea na kufanya mikutano ya hadhara katika vijiji kadhaa.
Mndeme alisema pamoja na tatizo la migogoro ya ardhi kuwa la muda mrefu katika wilaya hiyo, atahakikisha anawajibika kwa kushirikiana na wananchi hao ili kupata urahisi wa kuisululisha.
Aidha, Mndeme akiwa katika Kijiji cha Bassutoghang, viongozi wa kijiji hicho walimwonesha uharibifu mkubwa wa chanzo cha maji uliofanywa na wananchi wa Kijiji cha Mara, huku ikielezwa kwamba umetokana na viongozi wa kata na wilaya kushindwa kuwajibika ipasavyo.
“Ni marufuku kulima na kuchunga kwenye vyanzo vya maji, si kwa hapa Bassutoghang pekee, bali ni kwa wilaya nzima ya Hanan’g kwa kuzingatia sheria iliyowekwa ya kuhifadhi ardhi na mazingira,” alisema Mndeme.
Pia aliwahakikishia wananchi wa kijiji hicho kuwafikisha kwenye vyombo vya dola wale wote waliohusika na uharibifu katika chanzo hicho cha maji.
Kwa upande wake, Mbunge wa Hanan’g, Dk. Nagu alisema tatizo la uharibifu wa mazingira mara nyingi lmesababishwa na wageni wanaoingia katika maeneo ya wafugaji, huku wakijifanya kuwa ni wafugaji, lakini baada ya siku kadhaa wanabadilika na kuanza shughuli za kilimo.