HABARI MPYA LA JANA MATANGAZO BEI ZETU WASILIANA NASI TUMA HABARI
jumamosi, 16 juni 2012
Yaliyopita
Pekua Tovuti
Maadili stahiki yametoweka -2

Mwandishi wetu

 

WIKI iliyopita nilieleza maana ya maadili. Hivyo jamii ni lazima iwekwe pamoja kwa maadili stahiki. Sasa endelea.

Si nia yangu kuleta ubaguzi wala kusema ni makosa kufanya ndoa za mchanganyiko wa makabila, la hasha! Bali kwa kiasi kikubwa vijana wetu wanakosa yale mafundisho maalumu ya maadili ya makabila yao.

Kila kabila lina utamaduni wake mzuri unaomjengea kijana au mtoto taswira ya malezi bora ya ki-kwao. Enzi hizo toka vijijini vijana tulifundishwa kwanza kuheshimiana kati yetu wenyewe kutokana na rika tofauti, kuwachukulia wazee au wazazi wote pale kijijini kama wazazi wako, na sisi wenyewe kama ma-kaka na ma-dada, na kupendana kwa dhati.

Lugha na misemo ya vijana na hata wazee wakati huo, vilionesha hasa ni jinsi gani wana-jamii hao walivyo wastaarabu; na lugha za matusi zilikuwa ni shida sana kuzisikia zikitamkwa waziwazi tofauti na nyakati hizi; ambapo hasa mijini unaweza kumsikia mzazi anamtolea mtoto wake tusi ambalo wewe mwenye staha huwezi kulitamka.

Au watoto kwa watoto wanavyorushiana matusi na inaonekana ni lugha ya kawaida tu, na hata vijana kuwakebehi, kuwadharau na hata kuwatusi watu waliowapita umri ati si wazazi wao. Hali hii inatisha na kusikitisha ikionesha mmomonyoko wa maadili kwa kizazi cha sasa.

Jambo hilo la kutoweka kwa maadili mema linachangia hata maendeleo duni shuleni na vyuoni, na ukitaka kujaribu kukemea, ni lazima kwanza uwe na ‘kichwa cha mwendawazimu’ maana litakupa shida kupata mapokeo sahihi mara moja.

Tuangalie mahusiano kati ya vijana wa sasa na wazazi wao. Nadhani wazazi wengi hivi sasa wanawalea watoto kwa uhuru wa kupitiliza, na pengine kutaka kuwaonesha wanawapenda sana kiasi cha kutokuwa na mapenzi ya kweli.

Kwa maana ya kuwa aliye na upenzi wa kweli, hatadiriki kumwachia kijana wake ajiamulie kufanya mambo ya hovyo atakavyo wakati wowote. Kwa mfano, wengi wao hawafuatilii kabisa mienendo yao ya siku kwa siku; maendeleo yao ya masomo shuleni; kijana anarudi nyumbani wakati anaotaka mwenyewe, uhuru wa matembezi ya usiku mzazi asiyoyajua kaenda wapi, kwa sababu gani na ni kwa tija gani kwa familia.

Uvaaji usio wa heshima na hata kumuona mtoto ana vitu vya thamani bila ya kutaka kujua amevipataje; na haya yanajenga au kuzusha tamaa na kuharibika kwa watoto wetu, na hasa wasichana; vile vile kuwa ni chimbuko la kutofanya vizuri shuleni na hata kukatiza masomo.

Enzi hizo, unywaji wa pombe kwa vijana haukuwepo kwa kiasi kikubwa hivi, pia haukuwa wa wazi wazi; vijana waliwaogopa wanajamii kwa tabia hiyo ya unywaji wa pombe.

Hivi sasa unywaji wa pombe, uvutaji sigara hadi dawa za kulevya si jambo la siri, na tena ni jambo la kawaida, vijana wanaangamia mno. Kijana anakutana na mzazi wake baa na amtumia bia mbili-tatu za fasta fasta na mzazi nae anarudishia ofa, ilhali kijana huyo hajaanza kujitegemea, na pengine bado anaishi na wazazi wake.

Enzi hizo ukimuona mtoto wa mwenzako hata kama humjui, akiwa anafanya vitendo viovu, unaweza kumkanya na kumfokea, naye atakusikia na akatubu na kukuomba msamaha.

Hivi sasa wala usijaribu, maana majibu utakayoyapata utaomba bajaj itokee ghafla urukie na kupotelea mbali. Hali hii si nzuri kabisa, vijana na wazazi tubadilike. Hivi sasa kijana na hasa mabinti wanavaa nguo au ‘viwalo’ vya nusu-uchi, matiti yanakaribia kutolewa nje, wenyewe wanaita ‘heavy-breasts out fashion’ (mtindo wa maziwa nje nje), na wanakwenda kujiunga na wanajamii wengine mitaani bila woga wala soni. Wanakwenda hivyo hadi kwenye nyumba za ibada.

Tujiulize, watoto hao mabinti wamewezaje kutoka majumbani kwao? Jibu nikuwa, wazazi wao wameridhia uvaaji huo.

Ni aibu. Wazazi huo sio upendo wa kweli, naasa turudi kwenye baadhi ya maadili mema ya mila, jadi na desturi za makabila yetu, tutafaidika na kujenga kizazi chenye ustaarabu wa kweli na maadili stahiki kwa wakati wote.

Wazazi ndio wa kulaumiwa.



juu