MBUNGE wa Singida Mjini, Mohammed Dewji, amewahimiza vijana wanaojihusisha na biashara ya kusafirisha abiria kwa kutumia pikipiki (bodaboda) mkoani Singida kuanzisha vikundi, ili waweze kukopeshwa.
Dewji alitoa ushauri huo mwishoni mwa wiki alipowakabidhi pikipiki 10 zenye thamani ya sh milioni 20 vijana hao.
Taarifa kwa vyombo vya habari iliyotolewa jana na msaidizi wa mbunge huyo, Hassan Mazala, ilieleza Dewji alikabidhi pikipiki hizo alipofanya ziara jimboni humo na kukagua miradi mbalimbali ya maendeleo na kusema faida za kujiunga kwenye vikundi ni nyingi ikiwamo ya kuwa nafasi nzuri ya kupata mikopo mbalimbali kutoka kwenye taasisi za kifedha.
“Mtu mmoja mmoja akitaka kukopa fedha benki ni ngumu kutokana na masharti yaliyowekwa na taasisi za kifedha…siku zote umoja ni nguvu, utengano unachangia kulegevu unaozaa udhaifu, hivyo ni vizuri mkajiunga kwenye vikundi,” alisema Dewji.
Kuhusu pikipiki alizotoa msaada, alisema lengo ni kila kikundi kitaitumia pikipiki kwa ajili ya kukiongezea kikundi mapato ambayo endapo yatatunzwa vizuri, ipo siku kila mwanakikundi anaweza akamiliki pikipiki yake.