KAMATI za Ulinzi na Usalama zilizoundwa katika kila mtaa zitahusika kupitia maombi ya watu wote watakaojaza fomu za maombi ya kupewa vitambulisho vya taifa.
Hayo yamebainishwa jana na Kaimu Mkurugenzi Uzalishaji Vitambulisho vya Taifa, B Joseph Makani, katika mahojiano na ITV yaliyohusu kuanza kwa usajili mkoa wa Dar es Salaam.
Alisema mbali na Kamati za Ulinzi na Usalama, NIDA itashirikiana kwa karibu na Idara ya Uhamiaji, ambayo itakuwa na jukumu kubwa la kuisaidia mamlaka kuhakiki wageni wanaoishi nchini kihalali ili zoezi la utoaji vitambulisho liwe rahisi na kila kundi kupewa stahili zake.
“Vitambulisho viko vya aina tatu, kitambulisho cha raia, mgeni na mkimbizi. Ndio maana tunashirikiana na Idara ya Uhamiaji na Serikali za Mitaa katika kubaini nani raia, mgeni na mkimbizi,” alisema.
Akielezea changamoto za zoezi la usajili linaloendelea mkoani hapa, alisema kubwa ni wananchi kutoelewa vizuri zoezi la usajili kuwa limeanza na kwamba maafisa usajili wamekuwa wakipita nyumba kwa nyumba kusajili idadi ya watu katika kaya kwa lengo la kutengeneza daftari la makazi litakalomilikiwa na Serikali ya Mtaa zitakazosaidia ujazaji wa fomu za usajili unaokusudiwa kuanza hivi karibuni baada ya kukamilisha ujazaji wa madaftari ya wakazi, na taarifa za wakazi wote katika mkoa kuwa zimeingia katika kumbukumbu.
Usajili katika mkoa wa Dar es Salaam ulianza rasmi Juni 22 mwaka huu, siku 15 za kwanza ni usajili wa makazi nyumba kwa nyumba.
Baada ya kuisha siku 15 ndipo ujazaji wa fomu za usajili na utambuzi zitaanza na kuwataka wananchi kuandaa nakala ya vielelezo vitakavyowatambulisha kama vile, cheti cha kuzaliwa, pasi ya kusafiria, kadi ya kupigia kura, kadi ya Mfuko wa Hifadhi ya Jamii au Bima ya Afya, na kadhalika, ili wakati wa kujaza fomu unapowadia isichukue muda mrefu.