HABARI MPYA LA JANA MATANGAZO BEI ZETU WASILIANA NASI TUMA HABARI
jumatano, 4 julai 2012
Yaliyopita
Pekua Tovuti

Wasioona waomba halmashauri iwasaidie


na Julieth Mkireri, Kibaha

 

CHAMA cha wasioona wilayani Kibaha, mkoani Pwani kimeiomba serikali ngazi ya halmashauri kuona umuhimu wa kutenga fedha kwa ajili ya kukiwezesha chama hicho kutoa huduma stahiki kwa wanachama wao wanaoishi na virusi vya ukimwi.

Akizungumza katika mdahalo wenye lengo la kujadili sheria ya kuzuia na kudhibiti ukimwi ya mwaka 2008 ulioandaliwa na chama hicho na kushirikisha wadau mbalimbali wilayani humo, mratibu wa chama cha wasioona Kibaha Robert Bundala, alisema ipo haja ya serikali kutenga fedha hiyo ili kusaidia walemavu hao ambao wengi wao hawana uwezo.

Bundala alisema halmashauri hizo zikitenga fungu hilo itawasaidia wanachama wao walioathirika kuwapatia angalau lishe inayoshabihiana na masharti ya dawa za kupunguza makali ya ukimwi ARVs.

Aidha alibainisha kuwa mashirika na baadhi ya taasisi zinazotoa huduma hizo zimekuwa haziwafikii wasioona kwa kudhani wao hawahusiki na janga hilo hivyo kuomba lipatiwe ufumbuzi.

Awali akifungua mdahalo huo mkuu wa wilaya ya Kibaha Halima Kihemba alikemea tabia iliyojengeka katika jamii ya kutuma watoto chini ya miaka 14 baa ama dukani nyakati za usiku hali inayosababisha watoto hao kubakwa.

Kihemba aliwataka wazazi na walezi kutambua wajibu wao wa kuwalinda na kuwalea watoto kwa maadili yaliyo mema.

Wiki mbili zilizopita watoto watatu walio kati ya umri wa miaka 7 walibakwa katika maeneo tofauti wilayani kibaha kutokana na kutumwa usiku kununua vifaa vya matumizi ya nyumbani.



juu