HABARI MPYA LA JANA MATANGAZO BEI ZETU WASILIANA NASI TUMA HABARI
jumatano, 4 julai 2012
Yaliyopita
Pekua Tovuti

Walimu Mbeya waigeuzia kibao CWT


na Gordon Kalulunga, Mbeya

 

WALIMU waliojiendeleza elimu zao na kupandishwa vyeo bila mishahara, wamesema kuwa hawako tayari kuigomea serikali pekee, bali wako tayari kufanya hivyo kuigomea kwa pamoja serikali na Chama cha Walimu Tanzania (CWT) kwani kimekuwa kikinyonya fedha zao.

Waliyasema hayo jana walipokuwa wakizungumza na waandishi wa habari ambapo walidai kuwa hadi kufikia mwezi Septemba 2011, CWT ilikuwa inakusanya zaidi ya sh bilioni 40 kwa mwezi kutokana na vitega uchumi na makato ya mishahara ya walimu, huku viongozi wakiwa na usiri mkubwa juu ya mapato na matumizi ya fedha za chama hicho.

Walisema CWT wamenogewa na utamu wa fedha sasa wanaanzisha benki ambayo kwa jina itaitwa benki ya walimu pasipo kuwashirikisha walimu, kujenga maghorofa kila mkoa bila kuwashirikisha walimu, kuanzisha na kuendesha kampuni ya kibiashara inayoitwa Teachers Develoment Company Limited iliyoanzishwa 2005, kampuni ambayo walimu hawajui mahali ilipo.

Mwalimu Meshack Kapange ambaye ni kiongozi wa chama kipya cha walimu kijulikanacho kama Chama cha Maafisa Elimu Tanzania (UMET) alisema kuwa lengo la chama ni kumuwezesha mwalimu kuwa na kipato na uchumi mzuri kwa kumkopesha lakini CWT imewapotosha kwa kuendelea kuwajengea mawazo na fikra za kukopa kwa kuanzisha saccos zinazokopa mitaji kutoka mabenki kama vile CRDB badala ya kutumia fedha kinazokusanya.

“Je uliwahi kuona au kusikia madaktari, wanasheria, maafisa ugani wa kilimo na mifugo, askari polisi na wanajeshi na kada nyingine wanakopa kopa kama walimu?

“Madeni humuondolea mtu uhuru na kumfanya mtumwa na mkimbizi wa mazingira.

“CWT inawafanya walimu wawe watumwa wa madeni. Hatutaki utumwa, tunataka uhuru wa kipato na mahitaji,’’ alisema Mwalimu Kapange.

Alisema CWT imedhoofisha nguvu za walimu kwa kuwagawa na kuvunja matawi yaliyokuwa katika ngazi ya kata na shule ili walimu wasiweze kukutana na kufanya vikao vya pamoja kwa lengo la kujadili juu ya matatizo yao, badala yake kimewaweka wawakilishi wa mahali pa kazi ambao wanahudhuria vikao vya Baraza la Wilaya mara moja kila baada ya miaka miwili na nusu (miezi 30), na kuwafanya walimu wasiwe na mahali pa kutolea mawazo na kero zao.

Aliongeza kuwa pilika pilika za CWT za kuandaa mgomo zimeanza rasmi Juni 5, 2012 kwa kuitisha kikao cha ghafla mjini Dodoma, baada ya kuona UMET unaendelea na harakati za kidemokrasia za kupigania na kudai haki za walimu nchini na kufanya mazungumzo na mamlaka mbalimbali za serikali kuhusu haki na madai ya walimu kwa kuanzia Bungeni Januari 28, 2012 mpaka Februari 09, 2012, ambapo UMET kilipeleka hoja zake Ofisi ya Waziri Mkuu Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (TAMISEMI), Wizara ya Elimu na Mafunzo ya Ufundi na Wabunge mbalimbali bila kujali itikadi za vyama vyao.

Sanjari na hayo alibainisha kuwa Mei 28, 2012, UMET, ulifanya kikao na Kamati ya kudumu ya Huduma za Jamii ya Bunge kwenye Ofisi ndogo za Bunge jijini Dar-es-Salaam na kuwasilisha hoja za madai ya walimu zipatazo 19 ambapo katika kikao hicho CWT waliitwa na wakaamua kuchukua hoja tatu tu ambazo walishiriki kuzitengeneza na ndizo wanazoziandalia mgomo.

“CWT na serikali wanagombana kwenye vyombo vya habari lakini wakiitana ofisini wanamalizana na kuwaacha solemba walimu. Safari hii tutawaaminije? Ningependa kuishauri CWT kuwa kiwe cha kwanza kuachilia haki za walimu ndipo kiitishe mgomo, walimu tunayo haki ya kugoma kama tukiamua kugoma, lakini tuwagomee wote wawili, CWT na serikali wote ni wabaya wetu na waporaji wa haki za walimu,’’ alisema Mwalimu Kapange.



juu