RAIS wangu hapa ulipotufikisha sipo. Turudishe ulikotukuta! Dini ya viongozi wetu sasa imekuwa ni vyama vyao vya siasa. Tunaanza kuuana kwa visingizio ya vyama! Hatukuwa hivi! Kugombana kwa sababu ya tofauti zetu za vyama vyetu vya kisiasa ni ujinga uliokubuhu!
Ndugu Rais katika maisha ya mwanadamu chama ni nini? Kiwe chama cha michezo, chama cha kuweka na kukopa au chama cha siasa ni pamoja na majengo yake, magari, bendera na mali zingine pamoja na wanachama. Duniani hakuna chama bora Tanzania kitapatikana vipi? Ndugu Rais, duniani hakuna chama kibovu Tanzania kitapatikana vipi?
Wanachama wa chama fulani hasa viongozi wengi wakiwa waadilifu tunasema chama kizuri. Wengi wakiwa wahuni au wezi tunasema chama kibaya hakifai. Ndiyo tuanze kuuana kwa kisingizio cha kutetea chama! Hapana! Hapana baba, alichofanyiwa dk Steven Ulimboka ni ushenzi! Turudishe ulikotukuta.
Rais wangu umezungumza lililo jema lazima tukusikilize wewe si ndiyo baba! Lakini mgomo wa madaktari umeitia nchi katika majaribu makubwa. serikali yako inahaha kutafuta maneno ya kusema ili ieleweke, haieleweki. Waziri Mkuu ameeleza bungeni wananchi wamemsikia, ukiwauliza hakuna aliyemwelewa.
Baba umelielezea zogo hilo kwa ufasaha kabisa taifa limekusikia. Lakini lazima tukubali ukweli kuwa tukio la kusikitisha lililomsibu Dk. Steven Ulimboka limeitikisa nchi na kuiacha ikiwa katika wasiwasi mkubwa. Hatujamjua aliyetenda unyama huu lakini ni unyama umetendeka, kama hatukulilia wewe tumlilie nani?
Ndugu Rais jambo hili ni zito. Matokeo yatakayofuatia tukio hili ndiyo yanayotisha zaidi. Historia inayo yote katika uwazi.
Ulimboka ameteswa kitaalamu. Hakuumizwa kama wanavyoumizwa vibaka au hata majambazi wanavyosulubiwa na wananchi wenye hasira kali mpaka kuuawa hata kwa kuchomwa moto. Waliokuwa wakimtesa Steven Ulimboka hawakuwa na hasira moyoni mwao. Wanaonekana kama walikuwa wanafanya kazi kama wafanyakazi wengine wanavyofanya kazi zao. Huwezi kuwaweka katika kundi la wahuni au majambazi. Utesaji ule lazima uwe umefunzwa!
Tumefikaje hapa? Kwa hili wanahistoria hawawezi kumkumbuka Kwame Nkurumah, watamkumbuka Iddi Amin Dada. Hawawezi kumkumbuka Nelson Mandela, watamkumbuka Mobutu Sese Seko. Watawakumbuka watesi!
Rais wangu kukana kuhusika sawa maana watesi wake hatujawajua! Hakikisha agizo lako la kuwasaka waliotenda unyama huu linaheshimiwa na wahusika wanakamatwa. Hili ni muhimu sana kwasababu Steven Ulimboka alikuwa katika ugomvi mkubwa na serikali yako, wananchi kudhani serikali inahusika hawakosei. Kumbe wamhisi nani? Hizi ndizo sheria za maumbile ya mwanadamu.
Hivyo bila watu hawa kukamatwa imani ya wananchi kuwa serikali imehusika itakuwa ngumu kutoka katika vichwa na ndani ya mioyo yao. Serikali ikichukiwa na wananchi, rais ndiye anayechukiwa! Hakuna jambo la hatari kwa rais yeyote duniani, kama kuchukiwa na wananchi wake! Sitakubali rais wangu achukiwe na watu wake. Wagoni wa kisiasa wanaodhani wanaitetea serikali kwa kubwata hovyohovyo hadharani na hata bungeni ndiyo wanaozidisha chuki na hasira za wananchi dhidi ya serikali, dhidi ya Rais wangu. Ndugu rais sitakubali rais wangu apigwe mawe kwa upuuzi wa watu wachache!
Waliosoma vema kitabu cha Mwalimu Mkuu wa Watu watasema mbegu imerutubishwa kwa damu ya Ulimboka mti wa uzima sasa utachipua, mjinga atasema hili fundisho watu waniogope. Wanaosema kitabu cha Mwalimu Mkuu wa Watu ni utabiri, sigombani nao ingawa bado naamini kuwa ni hesabu tu za mcheza bao hodari.
Rais wangu Ulimboka amepelekwa nje kutibiwa kwa sababu tu Muhimbili haina vifaa vya kumtibia. Madaktari bingwa wa kuweza kumtibu pale Muhimbili wapo. Hawana vitendea kazi. Hili ni moja kati ya madai ya madaktari ambalo kila serikali inapozungumzia mgomo wa madaktari hailitamki.
Muhimbili ndiyo hospitali kubwa kuliko zote nchini, haina hata mashine ya kuzifanya figo tu zifanye kazi yake. Hapa ndipo wengine tunapopata taabu kuwajibu wanaotuona tu wajinga kupindukia kufuja mabilioni ya shilingi eti kusheherekea miaka 50 ya uhuru. Kuna uhuru gani bila afya njema?
Wanasema hakuna hata hospitali moja nchini yenye mashini ya skena wakati bei ya mashini moja ya skena ni sawa na bei ya shangingi moja. Kuna mashangingi mangapi serikalini?
Rais wangu pamoja na kueleza vyema lakini watu wako wanajiuliza ilikuwaje moyo wako wa huruma uliowazoesha haukuonekana katika hili? Una moyo mkubwa katika kuhudhuria misiba na kuwatembelea wagonjwa.
Mwanamwema Saed Kubenea alipomwagiwa tindikali na kulazwa Muhimbili ulifika kumjulia hali. Mcheza michezo ya kuigiza alipopatwa na mauti katika mazingira ya kutatanisha ulifika mpaka nyumbani kwake, Sinza Vatican. Wananchi wakaambiwa kuna ubani, milioni kumi zilitolewa.
Nilisema wewe ni baba yetu wote. Unachofanya kwa mmoja wetu kama baba hakikisha na kwa wengine utakifanya. Kwa sheria za maumbile hivyo ndivyo anavyopaswa kuwa baba mwema. Tukio la Steven Ulimboka limelishtua Taifa, baba haukufanya kama kawaida yako! Kutokwenda Muhimbili kumjulia hali kama ulivyowazoesha watu wako kunatoa fursa kwa wananchi wetu kutufikiria hivi wanavyotufikiria. Kumbuka huyu alikuwa katika mzozo mkali na serikali unayoiongoza.
Tuna maswali mengi ya kujiuliza. Tunakwenda wapi? Je, mgomo wa madaktari utamalizika kwa staili hii? Madaktari wakibaki ngangari nini kitafuata? Tujiangalie, yawezekana katika hili tukawa tunatumia misuli zaidi, wanaoumia ni wananchi. Tumefikaje hapa? Tutatokaje hapa? Au ni upepo unavuma?
Tukubali nchi imefika kwenye fundo. Tufanyeje? Ukweli unapotuumbua tuukubali. Mfumo wa utawala tulionao hauwezi kurekebishika. Tunahitaji kuufumua wote na kuusuka upya. Nani wa kuongoza zoezi hili? Nchi inahitaji busara sasa kuliko wakati mwingine wowote.
Rais wangu waelekeze Watanzania katika imani ya ‘nchi yangu kwanza’ Tunahitaji umoja na mshikamano sasa kuliko hata kipindi kilichopita. Tunahitaji Jukwaa la Mwalimu. Mahali pekee ambapo hakuna uchama wala udini. Wote tu wana wa mama mmoja tunagombea nini? Tusitoe nafasi kwa roho za shetani kutawala. Nchi ni yetu wote. Vyama vilikuja, vyama vitapita nchi itabaki. Mwalimu Forum-MWAFO, Nchi yangu kwanza!