KATI ya mambo wanayopenda sana kuyazungumza watu wa Chama Cha Mapinduzi ni ule msemo wa Mwalimu Nyerere kwamba bila CCM madhubuti, nchi itayumba. Lakini bahati mbaya wananukuu msemo huo nje ya muktadha uliotolewa na aghalabu kwa kufanya hivyo hupotosha umma kwamba Nyerere alimaanisha kwamba bila chama tawala iwe ni CUF, CHADEMA, TADEA , PONA au chama kingine chochote kitakachokuwa madarakani lazima kiwe imara.
CCM wamekuwa kama watu wenye imani ambazo wengine huziita kali za dini lakini ukweli ni imani zilizobabuliwa bila kuiva, ambao husoma mistari kutoka vitabu vitakatifu na kuushikilia mstari huo huo bila kusoma maana nzima inayopatikana katika aya au hata sura ya kitabu husika. Ni kama maindi yaliyochomwa kwenye moto wa karatasi ambapo kwa juu huonekana yameiva lakini kimsingi bado ni mabichi.
Kinachothibitika sasa ni kwamba CCM si chama imara na sasa hivi wanaofikiri wanakipenda badala ya kukisaidia kiimarike, wanakifichia udhaifu wake lakini kwa namna ambayo haitasaidia. Inakuwa ile hadithi ya mbuni kujaribu kuficha kichwa kwenye mchanga akiamini mwili uliobaki hauonekani! Ndivyo bunge linavyojaribu kufanya kwa kutumia wingi wa wabunge wa CCM ambao inawezekana kabisa umetokana na udhaifu mkubwa wa wapiga kura.
Sasa tuna serikali na CCM inayookolewa na miongozo lakini ukweli kinachofanyika ni kuficha tu kichwa kwenye mchanga. Ukwerli unaonekana wazi wazi. Mnadhimu Mkuu wa kambi ya watwala amekuwa akifanya kazi kubwa kuhakikisha mambo ya ufundi yanashinda hoja. Na hii haiwasaidii sio serikali wala chama tawala. Spika au wenyeviti wametumia kanuni za Bunge kusaidia kuibeba serikali iliyochoka ya CCM.
Watu wanaachia masikio wazi na kusikiliza kwa makini ukidhani wanasikiliza hoja, kumbe wanasikiliza maneno yaliyotumika ili waangalie kama kwa tafsiri yao ni maneno ya kuudhi. Lakini watunzi wa kanuni hizo za bunge sijui kama waliufahamu msemo maarufu wa Kiswahili kwamba ukweli unauma! Ukisikiliza vingi kati ya hivyo vinavyoitwa lugha ya kuudhi ni ukweli unaouma. Tiba ya mambo haya si kuwataka watu wafute kauli bali kurekebisha palipoharibika. Namkumbuka sana marehemu Phares Kabuye aliyekuwa mbunge wa Biharamulo Magharibi, aliyewahi kutamka kwamba wabunge walioko bungeni wameingia kwa rushwa. Alilazimishwa afute kauli ile. Bila shaka ilikuwa moja ya kauli za kuwaudhi kabisa waheshimiwa! Mwenyewe aliifuta lakini akisistiza ujumbe ulikuwa umefika.
Hata pale wabunge wa upinzani wanatakiwa kuthibitisha hoja zao au kufuta hoja zao au kutolewa nje, huwa wanakuwa wameshafikisha ujumbe maana hata waimba taarabu wanatuambia maneno yakishatamkwa hayarudi tena mdomoni. Salama ya serikali ya CCM sasa dhidi ya hoja za wapinzani imekuwa miongozo na maamuzi ya spika. Kuna maamuzi ambayo hayakuwahi kutolewa na wenye kuchanganya mbongo zao wanaamini kwamba hoja za ukweli zilikuwa zimezidi jazba za kutaka uthibitisho!
Siku ya Jumatatu wiki hii nilimsikia Tundu Lissu akitaka mwongozo na akisoma vifungu vya kanuni za bunge ambavyo vilihitaji majibu ya mwenyekiti. Mwenyekiti akaamua kuacha hoja na kumwonya Lissu asitafute umaarufu kwa Watanzania. Mungu wangu! Kwanza Tundu tayari kwa utundu wake ni maarufu lakini la pili Mwenyekiti alipaswa ajibu hoja ya vifungu kwa vifungu. Kilichokuwa kinaelezwa na Lissu ilikuwa jambo dhahiri. Kwamba aliyenyanyuka na kudai Sugu kadanganya Bunge angepaswa kwanza kuthibitisha uongo wa Sugu ndipo kiti kimtake Sugu kuthibitisha kauli yake. Hakukuwepo jibu la kanuni hisika badala yake jibu dhaifu kabisa kwamba Lissu anataka umaarufu.
Lakini akizungumza mtu kwamba ipo siku watarushiana ngumi, hiyo ni hoja. Akitokea mtu akatoa hoja za nani yuko nyuma ya mgomo wa madaktari hiyo ni hoja nzuri kwa CCM kama wanaotuhumiwa ni wapinzani. Hivi tatizo la mgomo linaweza kumalizwa kwa kumtafuta mchawi? Inawezekana CHADEMA ndio walioishauri serikali ya CCM kwa miaka hamsini ya uhuhru ishindwe kuwa na vitanda vya kutosha kwa wagonjwa lakini iwe na magari ya kifahari kwa watawala? Inawezekana CHADEMA ndio walioishauri serikali ya CCM ishindwe kuweka mashine ya CT Scan kwenye Hospitali ya Taifa? Inawezekana wapinzani ndio walioishawishi serikali ya CCM ishindwe kununua mashine za X-ray kwa kila wilaya ? Ni wapinzani wanaokausha vidonge hospitalini na wagonjwa wakiandikiwa dawa wanarudi nyumbani na karatasi la cheti badala ya dawa?
Hayo maswali hapo juu yangeweza kujadiliwa na bunge bila kuathiri kesi tunayoambiwa iko mahakamani. Lakini Bunge kwa kisingizio cha kuwepo kwa kesi mahakamani, ikazuia mjadala muhimu kuhusu hali ya afya kwa watanzania. Lakini rais yeye hakuliona hilo la kesi mahakamani, katika hotuba yake akajadili kwa kina mgogoro huo na kuwatangazia Watanzania nani mkorofi. Mahakama ina jipya tena la kuamua hapo? Na hata rais keshazungumza kuwaondoa hata upande unaotuhumiwa mtaani na baadhi ya watu kuhusika katika sakata la kumteka Dk. Ulimboka wakati tayari kuna tume inaundwa kuchunguza tukio hilo. Kwa nini rais hakusubiri hoja ya kutekwa na kuumizwa kwa Dk. Ulimboka kujadiliwe baada ya tume huru kufanya uchunguzi wake?
Kwa mwendo huu tusitarajie maendeleo kwa kutumia serikali hii ya CCM ambayo kazi yake kubwa ni kujikwamua kutoka katika shutuma na tuhuma badala ya kuleta maendeleo. Leo serikali wanahaha kuonyesha kwamba madaktari ndio wakorofi na wanashindilia hoja zote kwenye dai la posho na mishahara, wako kimya kuhusu vifaa tiba. Wabunge wanaoapaswa kuiamsha serikali leo wanaisaidia kuficha kichwa kwenye mchanga.
Bahati mbaya sana maneno matupu hayavunji mfupa. Wanapochangia bajeti na kuipamba kwamba ni nzuri haiwi nzuri kwa sababu ya tambo na mbwembwe za wachangiaji. Wanapowabeza wapinzani kwamba wanatafuta sifa, hawawezi kuzuia masikio na macho ya Watanzania timamu kuona pumba ni zipi na mchele ni upi. Na ukweli na uongo hujitenga kama maji na mafuta. Watanzania wa leo si wale wa muongo mmoja uliopita.
Wabunge wanapaswa kuwasaidia wananchi kuikaba koo serikali itimize wajibu wake sio kujaribu kuzuia jua lisiwake kwa kutumia viganja vya mkono. Na katika michango kama hii ya wabunge hivi kweli tunahitaji wabunge wengi kiasi hiki? Pengine sasa tutafute ushauri wa kitaalamu wa kujua kiwango cha hoja za wabunge na kufanyia utafiti wa kisayansi tuone kama inawezekana wabunge watoke mmoja kila mkoa. Ukiwa na vichwa vizuri kulingana na idadi ya mikoa yetu, serikali inaweza kabisa kusimamiwa kitaalamu kuliko kuchukua wabunge kutokana na ukada wao bila uwezo wa kuainisha na kujenga hoja. Sasa tuna wabunge wengi lakini sina hakika kama kilichotazamiwa kwa kuongeza huo uwakilishi kama kimefikiwa maana hata Waswahili wanasema ukubwa wa pua sio wingi wa kamasi. Ama kwa hakika ukifuatilia haya yote utagundua kwamba serikali ya CCM inaponea bungeni kwa maombi ya mwongozo na si hoja za ushawishi.